Blog

  • Mfumuko wa Bei ya Mafuta Waingia Hatua Mpya Marekani: Kampuni ya Walmart Yatoa Onyo Zito

    Mfumuko wa Bei ya Mafuta Waingia Hatua Mpya Marekani: Kampuni ya Walmart Yatoa Onyo Zito

    Mfumuko wa bei ya mafuta nchini Marekani umeingia katika hatua mpya, huku ukizidi kutishia uchumi wa wananchi wake.

    Kampuni kubwa ya rejareja nchini humo, Walmart, imetoa onyo ikieleza kuwa kupanda kwa bei ya nishati hiyo, kufuatia mgogoro wa Mlango wa Bahari wa Hormuz, kumeongeza msukumo na mzigo mzito wa kimaisha kwa kaya nyingi za Wamarekani.

    Kwa mujibu wa takwimu, bei ya galoni moja ya mafuta nchini Marekani imepaa kutoka takriban dola $3 hadi dola $4.56. Kufuatia hali hii, kampuni ya Walmart imetabiri kuwa ukuaji wa mauzo yake utashuka katika miezi ijayo.

    Aidha, wakurugenzi wa kampuni hiyo wametoa tahadhari kuwa endapo mgogoro huo utaendelea, unaweza kusababisha kupanda zaidi kwa bei za vyakula na hatimaye kupunguza uwezo wa manunuzi kwa walaji nchini Marekani.

  • Juhudi za Kusaka Amani: Ujumbe wa Iran Wawasili Qatar Kujadili Usitishaji wa Vita

    Juhudi za Kusaka Amani: Ujumbe wa Iran Wawasili Qatar Kujadili Usitishaji wa Vita

    DOHA, QATAR- Katika hatua muhimu ya kidiplomasia, ujumbe rasmi kutoka nchini Iran, ukiongozwa na Mohammad Bagher Ghalibaf, umewasili jijini Doha, Qatar hivi leo, kwa mujibu wa ripoti kutoka shirika la habari la serikali.

    Ziara hii inatajwa kuwa ni muendelezo wa mchakato wa kidiplomasia unaoendelea kwa kasi. Hatua hizi zilianza katika wiki za hivi karibuni chini ya upatanishi wa serikali ya Pakistan, zikiwa na lengo kuu la kutafuta suluhu na kuhitimisha vita vilivyolazimishwa.

    Wakati wa ziara hii, ujumbe huo wa Iran unatarajiwa kufanya mazungumzo na mashauriano ya kina na viongozi wa ngazi za juu wa serikali ya Qatar. Taarifa zinaeleza kuwa mazungumzo hayo yatajikita katika kujadili vipengele muhimu vinavyohusiana na mchakato wa amani na mikakati ya kukomesha kabisa vita hivyo.

  • Yanayojiri kuhusu vita vya Iran: Trump anasema ‘makubaliano na Iran yamekaribia kukamilika’

    Yanayojiri kuhusu vita vya Iran: Trump anasema ‘makubaliano na Iran yamekaribia kukamilika’

    Yanayojiri:

    Donald Trump amesema katika mahojiano kwamba amegawanyika “50/50” kati ya kufikia makubaliano ya amani na Iran na kuanzisha tena mashambulizi ya kijeshi.

    Iran na Pakistan zimewasilisha pendekezo lililorekebishwa kwa Marekani la kusitisha vita.

    Mkuu wa Jeshi la Pakistan, Munir, ameondoka Tehran baada ya mfululizo wa mikutano, ikijumuisha mikutano miwili na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Araghchi na Rais Pezeshkian.

    Misimamo ya Marekani na Iran “imekuwa ikikaribiana” katika wiki iliyopita, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema.

    Viongozi kadhaa wa Mashariki ya Kati walifanya mazungumzo ya simu na Trump wakati wa juhudi za kuongeza kasi za kupatanisha makubaliano.

    Araghchi alithibitisha yaliyomo kwenye barua aliyotuma kwa Hezbollah ambamo aliwaahidi kwamba Iran “haitaacha kamwe kuisaidia” kundi hilo lenye silaha.

    Shambulio la Israel karibu na hospitali nchini Lebanon Kusini limewajeruhi wafanyakazi 25 wa afya.

  • Senegal Yakaza Uzi Dhidi ya Mapenzi ya Jinsia Moja, Waziri Mkuu Ashutumu Mataifa ya Magharibi

    Senegal Yakaza Uzi Dhidi ya Mapenzi ya Jinsia Moja, Waziri Mkuu Ashutumu Mataifa ya Magharibi

    DAKAR, SENEGAL – Waziri Mkuu wa Senegal, Ousmane Sonko, ameyashutumu vikali mataifa ya Magharibi kwa kile alichokieleza kuwa ni jaribio la kulazimisha vitendo vya mapenzi ya jinsia moja katika taifa hilo la Afrika Magharibi.

    Kiongozi huyo alitoa matamshi hayo alipokuwa akihutubia Bunge la Taifa siku ya Ijumaa. Katika hotuba yake, Bw. Sonko alitetea sheria mpya kali zinazolenga kudhibiti mapenzi ya jinsia moja nchini Senegal, hatua ambayo imeendelea kuvutia ukosoaji mkubwa kutoka kwa wanaharakati wa haki za binadamu.

    “Kuna aina fulani ya ubabe unaofanywa. Kuna wanadamu bilioni nane duniani, lakini kuna kikundi kidogo kinachoitwa Magharibi ambacho, kwa sababu kina rasilimali na kinadhibiti vyombo vya habari, kinataka kuulazimisha ulimwengu uliosalia kukubali [ushoga],” alisema Sonko.

    Sheria hiyo mpya, iliyoanza kutekelezwa rasmi mwishoni mwa mwezi Machi, imeongeza adhabu ya kifungo jela maradufu kwa wale watakaopatikana na hatia ya kujihusisha na vitendo vya mapenzi ya jinsia moja, kutoka miaka mitano hadi miaka 10.

    Vilevile, sheria hiyo inafanya kuwa kosa la jinai kitendo cha kufadhili mahusiano hayo, pamoja na kile kilichoelezwa kwenye sheria kama “kutukuza matendo yasiyo ya asili”, kipengele kinachojumuisha kuhamasisha au kujihusisha na vitendo hivyo.

    Awali, Mkuu wa Shirika la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa, Volker Turk, alimtaka Rais wa Senegal, Bassirou Diomaye Faye, kutoidhinisha sheria hiyo, akiielezea kuwa inatia “wasiwasi mkubwa”.

    “Sheria hii inawaweka watu katika hatari ya kufanyiwa uhalifu wa chuki, unyanyasaji, ukamataji holela, utapeli, na ubaguzi ulioenea katika sekta za elimu, afya, ajira na makazi,” alisema Turk wakati huo. Aliongeza kuwa sheria hiyo inazuia kazi halali za watetezi wa haki za binadamu, vyombo vya habari, na uhuru wa kujieleza kwa kila raia nchini Senegal.

    Kupitishwa na kutekelezwa kwa sheria hii mpya kunakuja wakati kukiwa na ripoti za ongezeko la ukamataji wa watu wanaodaiwa kujihusisha na mapenzi ya jinsia moja nchini humo.

  • Iran Yasisitiza Kuiunga Mkono Hezbollah, Yadai Usitishaji Vita Lebanon Katika Makubaliano Yoyote ya Amani.

    Iran Yasisitiza Kuiunga Mkono Hezbollah, Yadai Usitishaji Vita Lebanon Katika Makubaliano Yoyote ya Amani.

    Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Seyed Abbas Araghchi, amewasilisha ujumbe maalum kwa Katibu Mkuu wa Hezbollah, Sheikh Naim Qassem, akisisitiza msimamo thabiti wa Tehran wa kuendelea kuliunga mkono kundi hilo na msisitizo wa kusitisha vita nchini Lebanon.

    Katika ujumbe huo, Waziri Araghchi amebainisha kuwa Iran itaendelea kutoa ushirikiano na kuunga mkono vuguvugu la kutafuta haki na uhuru, hususan Hezbollah. Ameeleza kuwa msimamo huo ni muendelezo wa ahadi ya kihistoria iliyoachwa na Imamu shahidi na ni utekelezaji wa agano kwa Kiongozi Mkuu wa nchi hiyo, Grand Ayatollah Seyed Ali Khamenei.

    Kuhusu masuala ya kidiplomasia, taarifa hiyo imeweka wazi sharti kuu la Iran katika mchakato wowote wa amani. Imesisitizwa kuwa, tangu mwanzo wa majadiliano, Iran imesimama kidete kuwa makubaliano yoyote yanayohusisha Marekani lazima yaende sambamba na usitishaji vita nchini Lebanon. Hoja hii imeelezwa kuendelea kuwa kipaumbele na takwa la msingi la Serikali ya Jamhuri ya Kiislamu na wananchi wake.

    Aidha, ujumbe huo umefichua taarifa kuhusu juhudi za hivi karibuni za kidiplomasia. Imebainishwa kuwa katika pendekezo la hivi punde lililotolewa na Iran kupitia kwa wasuluhishi wa Pakistan, ambalo linalenga kusitisha vita kwa kudumu, suala la kuijumuisha Lebanon katika makubaliano ya kusitisha mapigano limesisitizwa kwa uzito mkubwa.

    Ujumbe huu wa kidiplomasia unathibitisha wazi msimamo wa Iran kuhusu mshirika wake mkuu nchini Lebanon, Hezbollah, na unaashiria kuwa Tehran inaichukulia Lebanon kama kipengele kisichoweza kutenganishwa katika kutafuta suluhu ya kudumu ya usalama na amani katika ukanda huo.

  • 90 waaga dunia na wengine kadhaa kujeruhiwa kwenye mgodi China

    90 waaga dunia na wengine kadhaa kujeruhiwa kwenye mgodi China

    TAKRIBAN watu 90 walifariki kufuatia mlipuko katika mgodi wa makaa ya mawe [coal kwa Kimombo] kaskazini mwa China, kulingana na vyombo vya habari vya serikali ya nchi hiyo.

    Mlipuko huo wa gesi ulitokea katika Mgodi wa Makaa ya Mawe wa Liushenyu unaomilikiwa na kampuni ya Tongzhou Group katika Mkoa wa Shanxi.

    Mamia ya waokoaji walitumwa katika eneo hilo huku watu 27 wakiripotiwa kulazwa hospitalini wakipokea matibabu, mmoja akiwa katika hali mahututi.

    Operesheni za uokoaji bado zinaendelea.Mlipuko huo ulitokea usiku Ijumaa katika mgodi huo uliokuwa na wafanyakazi 247 waliokuwa kazini wakati wa ajali hiyo.

    Mmoja wa wachimbaji waliojeruhiwa, Wang Yong, aliambia televisheni ya serikali kuwa hakusikia mlio wowote wakati mlipuko ulipotokea bali aliona moshi mzito ukitanda ghafla.

    “Nilinusa harufu kama ile ya milipuko. Nikaanza kuwapigia watu kelele wakimbie.

    Tulipokuwa tunakimbia niliona watu wakianguka kutokana na moshi huo. Baadaye nami nikapoteza fahamu,” alisema.

    Aliongeza kuwa alikaa chini kwa karibu saa moja kabla ya kuzinduka na kumwamsha mwenzake waliyetoroka pamoja kutoka mgodini.Baada ya mkasa huo, Rais wa China Xi Jinping aliagiza juhudi zote zifanywe kuwahudumia majeruhi na kutafuta manusura. Pia aliitaka serikali kuchunguza chanzo cha ajali hiyo na kuwachukulia hatua waliohusika.Vyombo vya habari vya serikali vilisema maafisa wanaosimamia mgodi huo wamezuiliwa huku uchunguzi ukiendelea. Hata hivyo, chanzo rasmi cha mlipuko huo bado hakijatangazwa.

    Ripoti zinaonyesha viwango vya gesi ya kaboni, ambayo ni sumu kali isiyo na harufu, vilipatikana kuwa juu ya kiwango kinachoruhusiwa.

    Wizara ya Usimamizi wa Dharura ya China ilituma wafanyakazi 345 kutoka vikosi sita vya uokoaji kusaidia shughuli hizo.

    Mnamo mwaka 2024, mgodi wa Liushenyu ulitajwa na Mamlaka ya Kitaifa ya Usalama wa Migodi ya China kuwa miongoni mwa migodi yenye “hatari kubwa za usalama”.

    Kampuni ya Tongzhou Group pia ilipewa adhabu mbili za kiutawala mwaka 2025 kutokana na masuala ya usalama.