Kategoria: MICHEZO

  • MWISHO WA ENZI: Pep Guardiola Kuiaga Manchester City, Enzo Maresca Atajwa Kurithi Mikoba Yake

    MWISHO WA ENZI: Pep Guardiola Kuiaga Manchester City, Enzo Maresca Atajwa Kurithi Mikoba Yake

    Kocha mkuu wa Manchester City, Pep Guardiola, anatarajiwa kuachia ngazi majira ya joto mwaka huu, hatua itakayohitimisha moja ya vipindi vya mafanikio makubwa zaidi katika historia ya Ligi Kuu ya England (Premier League).

    Vyanzo mbalimbali vya habari vilivyo karibu na klabu hiyo vinaeleza kuwa, Guardiola anajiandaa kuondoka mwishoni mwa msimu huu ambao tayari kikosi chake kimeshatwaa makombe ya Carabao na FA.

    Ushindi wa Jumamosi dhidi ya Chelsea umemhakikishia kocha huyo mwenye umri wa miaka 55 taji lake la 20 kubwa ndani ya kipindi cha miaka 10 aliyodumu kunako dimba la Etihad.

    Kufuatia taarifa hizo, aliyekuwa kocha wa Chelsea, Enzo Maresca, anapewa nafasi kubwa ya kwenda kuchukua mikoba ya kuinoa miamba hiyo ya soka. Maresca anatarajiwa kupewa jukumu hilo zikiwa zimepita miezi minne pekee tangu aondoke Chelsea, huku Manchester City ikisalia kwenye nafasi nzuri ya kuweza kutwaa ubingwa mwingine wa Ligi Kuu msimu huu.

  • Lewandowski Aweka Hatma yake Barça Rehani, Fc Porto Waingia kwenye Mbio za Usajili.

    Lewandowski Aweka Hatma yake Barça Rehani, Fc Porto Waingia kwenye Mbio za Usajili.

    Ripoti mpya kutoka Hispania zinaeleza kuwa mshambuliaji nyota Robert Lewandowski huenda akaondoka FC Barcelona katika dirisha lijalo la usajili wa majira ya kiangazi.

    Inaelezwa kuwa nyota huyo wa Poland amepoteza nafasi yake ya kudumu katika kikosi cha kwanza cha kocha wa Barça, hali inayochochea tetesi za kuondoka kwake Nou Camp.

    Kwa muda mrefu AC Milan imekuwa ikipewa nafasi kubwa ya kumsajili mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 37, lakini sasa klabu ya FC Porto imejitokeza kama mshindani mpya wa kushtua.

    Mabingwa hao wa Liga Portugal wanadaiwa kuwa na nia ya dhati ya kumleta Lewandowski nchini Ureno kabla ya msimu mpya kuanza.

    Iwapo dili hilo litakamilika, huenda ikawa sura mpya na ya mwisho katika maisha ya soka ya mshambuliaji huyo nguli barani Ulaya.

  • Pezeshkian Ahamasisha Wachezaji wa Iran Kung’ara Kombe la Dunia.

    Pezeshkian Ahamasisha Wachezaji wa Iran Kung’ara Kombe la Dunia.

    Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian, ametembelea kambi ya timu ya taifa ya mpira wa miguu ya Iran kabla ya kuondoka kuelekea Kombe la Dunia, akiwahimiza wachezaji na benchi la ufundi kujituma kikamilifu ili kuiletea nchi heshima.

    Katika ziara hiyo iliyofanyika Jumatano kwenye kituo cha mazoezi cha timu ya taifa, rais huyo alikutana na wachezaji, makocha pamoja na viongozi wa shirikisho la mpira wa miguu la Iran. Katika mazungumzo yake, alisisitiza umuhimu wa umoja na mshikamano wa kitaifa, pamoja na kuonyesha hadhi na nguvu ya watu wa Iran katika jukwaa la kimataifa kupitia michezo.

    Akilihutubia kikosi hicho, Pezeshkian alisema jambo muhimu ni juhudi za dhati, uwajibikaji na kutumia uwezo wote uliopo kwa ajili ya kuleta fahari kwa taifa. Aliongeza kuwa wananchi wa Iran wanatarajia wachezaji wao kusimama kwa heshima na kupambana kwa nguvu zote wanapokuwa uwanjani.

    Rais huyo pia alieleza kuwa michezo, hususan mpira wa miguu, ina nafasi muhimu katika kuimarisha mshikamano wa kitaifa, kuongeza mtaji wa kijamii na kuleta fahari miongoni mwa wananchi.

    Katika hafla hiyo, Pezeshkian alikabidhiwa jezi namba 12 ya timu ya taifa ya Iran, ambayo kwa kawaida huwakilisha mashabiki wa timu hiyo.

  • Crystal Palace yatinga fainali ya Conference League Ulaya baada ya kuifunga tena Shakhtar Donetsk

    Crystal Palace yatinga fainali ya Conference League Ulaya baada ya kuifunga tena Shakhtar Donetsk

    Crystal Palace imefanikiwa kutinga fainali ya Ligi ya Mkutano Ulaya baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Shakhtar Donetsk ya Ukraine katika mchezo wa marudiano wa nusu fainali uliochezwa Alhamisi.

    Timu hiyo ya England ilionyesha ubora wake tena baada ya pia kushinda mchezo wa kwanza kwa mabao 3-1, hivyo kufuzu kwa jumla ya mabao 5-2 katika michezo yote miwili.

    Katika mchezo huo, bao la kwanza la Crystal Palace lilipatikana dakika ya 25 kufuatia Pedro Henrique wa Shakhtar kujifunga.

    Ismaïla Sarr aliiongezea Palace bao la pili dakika ya 52 na kuimarisha matumaini ya timu hiyo kufuzu.Shakhtar Donetsk walipata bao lao pekee dakika ya 34 kupitia kwa Eguinaldo, lakini halikutosha kuizuia Crystal Palace kusonga mbele hadi hatua ya fainali.

    Kwa ushindi huo, Crystal Palace sasa itakutana na Rayo Vallecano ya Hispania katika fainali ya michuano hiyo, itakayochezwa tarehe 27 Mei mjini Leipzig, Ujerumani.

  • Mvutano wazuka Real Madrid: Valverde na Tchouaméni wadaiwa kupigana mazoezini

    Mvutano wazuka Real Madrid: Valverde na Tchouaméni wadaiwa kupigana mazoezini

    Klabu ya Real Madrid imekumbwa na taarifa za sintofahamu baada ya ripoti kutoka vyombo mbalimbali vya habari vya kimataifa kudai kuwa viungo wa timu hiyo, Federico Valverde na Aurélien Tchouaméni, walihusika kwenye ugomvi mkubwa uliotokea katika uwanja wa mazoezi wa Valdebebas.

    Kwa mujibu wa taarifa hizo, mvutano kati ya wachezaji hao ulianza kabla ya mazoezi kufanyika na baadaye kuendelea hadi ndani ya vyumba vya kubadilishia nguo baada ya mazoezi kumalizika.

    Ripoti zinaeleza kuwa hali ilikuwa mbaya kiasi cha baadhi ya wachezaji na maofisa wa benchi la ufundi kulazimika kuingilia kati ili kuwatenganisha wawili hao.

    Vyombo vya habari vya Ulaya vimeripoti kuwa Federico Valverde alipata jeraha eneo la kichwa katika tukio hilo na baadaye kupelekwa hospitali kwa uchunguzi zaidi. Hata hivyo, taarifa zinaeleza kuwa hali yake si mbaya sana.

    Chanzo cha mgogoro huo bado hakijawekwa wazi rasmi, lakini baadhi ya ripoti zinaonyesha kuwa kulikuwa na hali ya mvutano ndani ya kikosi hicho kufuatia matokeo yasiyoridhisha ya timu katika kipindi cha hivi karibuni.

    Real Madrid imekuwa chini ya presha baada ya kutolewa kwenye michuano ya UEFA Champions League pamoja na kupoteza nafasi muhimu katika mbio za ubingwa wa La Liga dhidi ya wapinzani wao FC Barcelona.

    Taarifa zaidi zinaeleza kuwa viongozi wa juu wa Real Madrid waliinisha kikao cha dharura kujadili tukio hilo huku uchunguzi wa ndani ukiendelea kubaini chanzo halisi cha mgogoro huo pamoja na hatua zinazoweza kuchukuliwa dhidi ya wahusika.

    Mpaka sasa, Real Madrid haijatoa tamko rasmi lenye kuthibitisha kwa undani tukio hilo, jambo ambalo limeendelea kuongeza mjadala mkubwa miongoni mwa mashabiki wa soka duniani.

    Iwapo taarifa hizi zitathibitishwa rasmi, tukio hilo linaweza kuwa miongoni mwa migogoro mikubwa kuwahi kutokea ndani ya kikosi cha Real Madrid katika miaka ya karibuni.

  • Didier Drogba Tanzania

    Didier Drogba Tanzania

    Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akisalimiana na Mshambuliaji wa zamani wa Timu ya Taifa ya Ivory Coast na Timu ya Chelsea ya Uingereza Didier Drogba mara baada ya kuwasili Ikulu Chamwino mkoani Dodoma, tarehe 05 Mei, 2026.