Lebo: Austria

  • “Hatupokei wachochezi” Austria yampiga marufuku waziri wa Israel, Itamar Ben-Gvir

    “Hatupokei wachochezi” Austria yampiga marufuku waziri wa Israel, Itamar Ben-Gvir

    VIENNA, AUSTRIA – Shinikizo dhidi ya viongozi wenye msimamo mkali nchini Israel limezidi kupamba moto barani Ulaya baada ya nchi ya Austria kutangaza kuunga mkono pendekezo la kupigwa marufuku kwa Waziri wa Usalama wa Taifa wa nchi hiyo, Itamar Ben-Gvir, kuingia barani humo.

    Kwa mujibu wa ripoti iliyochapishwa na gazeti la Kronen Zeitung, idadi ya wanasiasa mashuhuri ndani ya Umoja wa Ulaya (EU) wanaotaka kuwekewa vikwazo kwa wajumbe wa baraza la mawaziri la utawala wa Israel imeendelea kuongezeka. Hatua hiyo inakuja kutokana na mfululizo wa ghasia na ukandamizaji unaofanywa dhidi ya Wapalestina katika eneo la Ukingo wa Magharibi (West Bank).

    Katika msimamo mkali zaidi, mwanasiasa mashuhuri wa Austria, Beate Meinl-Reisinger, amejitokeza waziwazi kupinga vitendo vya Waziri Ben-Gvir, ambaye anajulikana kwa sera zake kali za mrengo wa kulia.

    Akizungumza siku ya Jumatatu pambezoni mwa mkutano wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Umoja wa Ulaya uliofanyika mjini Luxembourg, Meinl-Reisinger alibainisha kuwa mienendo ya waziri huyo haikubaliki. Alisisitiza kuwa msimamo huo unatokana na dharau na tabia za kikatili ambazo Ben-Gvir amekuwa akizionesha, hususan dhidi ya wahudumu na washiriki wa misafara ya kutoa misaada ya kibinadamu kuelekea Ukanda wa Gaza.

    “Mtu huyu hakaribishwi hapa kwetu,” alikaririwa Meinl-Reisinger, akionyesha msisitizo wa Austria katika kuungana na mataifa mengine wanachama wa EU yanayotaka kuwajibishwa kwa viongozi wanaochochea uvunjifu wa haki za binadamu.

    Hatua hii ya Austria inatajwa kuwa pigo kadiplomasia kwa serikali ya Israel, ikizingatiwa kuwa mataifa mengi ya Ulaya sasa yanaanza kuchukua hatua madhubuti za kivitendo badala ya kutoa matamko ya kulaani pekee.

  • CHOKOCHOKO AU KUKOSEA NJIA? Austria Yaonyesha Misuli kwa Ndege za Marekani Zilizovamia Anga Yake

    CHOKOCHOKO AU KUKOSEA NJIA? Austria Yaonyesha Misuli kwa Ndege za Marekani Zilizovamia Anga Yake

    VIENNA, AUSTRIA — Katika tukio ambalo limezua hisia za kiusalama, Jeshi la Austria limelazimika kurusha ndege zake za kivita aina ya Eurofighter kwa siku mbili mfululizo, kufuatia ndege za Jeshi la Anga la Marekani (USAF) kugundulika zikiendesha shughuli zake ndani ya anga ya Austria bila kuwa na vibali halali vya kupita.

    Hatua hii imechukuliwa kwa uzito mkubwa ikizingatiwa kuwa Austria ni taifa ambalo halifungamani na upande wowote kisiasa na kijeshi (neutral).

    Kwa mujibu wa taarifa rasmi, tukio la hivi karibuni lilishuhudiwa siku ya Jumapili ambapo ndege mbili za Marekani aina ya U-28A — ambazo ni toleo la PC-12 zinazotumiwa mahususi kwa oparesheni maalum za kijeshi — zilinaswa zikiruka juu ya eneo la milima ya Totes Gebirge, lililopo jimbo la Austria Juu.

    Inaarifiwa kuwa, mara baada ya ndege hizo za Marekani kunaswa na kukabiliwa na ndege za kivita za Austria, zililazimika kugeuza mwelekeo mara moja na kurejea jijini Munich, nchini Ujerumani.

    Msemaji wa Jeshi la Austria amethibitisha kutokea kwa tukio hilo kupitia taarifa aliyoitoa kwenye mtandao wa kijamii wa X (zamani Twitter).

    Serikali ya Austria imeongeza kuwa, masuala yote yanayoibuka kufuatia ukiukwaji huo wa anga yatashughulikiwa na kufuatiliwa zaidi kupitia njia rasmi za kidiplomasia kati ya mataifa hayo mawili.