Lebo: Ebola

  • Kenya Yathibitisha Kisa cha Kwanza cha Ebola

    Kenya Yathibitisha Kisa cha Kwanza cha Ebola

    Wizara ya Afya nchini Kenya imethibitisha kisa cha kwanza cha Ebola, kikihusisha raia wa Kenya aliyekuwa akiishi Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kabla ya kusafiri hadi Nairobi kupitia Uganda.

    Waziri wa Afya, Aden Duale, amesema mgonjwa huyo alifariki Jumatatu baada ya kuugua, huku mamlaka za afya zikianza ufuatiliaji wa watu waliowahi kuwa karibu naye.

    Kwa mujibu wa wizara, hadi sasa watu 28 waliokuwa na mawasiliano ya karibu na mgonjwa huyo wametambuliwa na wanaendelea kufuatiliwa na wataalamu wa afya.

    Mamlaka pia zinaendelea kuwatafuta watu wengine 27 ambao walikuwa katika safari moja na mgonjwa huyo wakati akisafiri kuelekea Nairobi.

    Wizara ya Afya imesema juhudi za ufuatiliaji na udhibiti wa maambukizi zinaendelea, huku wananchi wakitarajiwa kupewa taarifa zaidi kadri uchunguzi unavyoendelea.

    Chanzo: Wizara ya Afya Kenya.

  • Ufaransa yathibitisha kisa cha kwanza cha Ebola kutoka Congo

    Ufaransa yathibitisha kisa cha kwanza cha Ebola kutoka Congo

    Serikali ya Ufaransa imethibitisha kisa chake cha kwanza cha ugonjwa wa Ebola kinachohusiana na mripuko unaoendelea nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Kisa hicho kimebainika baada ya daktari mmoja, aliyekuwa akirejea nchini humo akitokea katika misheni ya kutoa misaada ya kibinadamu, kupimwa na kukutwa na virusi vya ugonjwa huo.

    Mgonjwa huyo tayari amewekwa chini ya uangalizi maalum na ametengwa (isolation) ili kuzuia maambukizi zaidi. Wakati huo huo, mamlaka za afya nchini Ufaransa zimeanza mchakato wa kuwatafuta na kuwafuatilia watu wote waliokuwa karibu au kugusana na daktari huyo (contact tracing).

    Pamoja na kutokea kwa kisa hicho, maafisa wa afya wametoa wito wa utulivu, wakieleza kuwa hatari ya kusambaa kwa ugonjwa huo kwa idadi kubwa ya watu barani Ulaya bado ni ndogo sana kutokana na mifumo imara ya afya iliyopo.