Lebo: Ghalibaf

  • Iran Yaikatilia Marekani: “Hatutanunua Bidhaa Zenu kwa Fedha Zetu Zilizokuwa Zimezuiliwa.”

    Iran Yaikatilia Marekani: “Hatutanunua Bidhaa Zenu kwa Fedha Zetu Zilizokuwa Zimezuiliwa.”

    TEHRAN, IRAN

    Spika wa Bunge la Iran, Mohammad Bagher Ghalibaf, amekanusha vikali madai yaliyotolewa na serikali ya Marekani (Washington) kwamba Iran inapanga kutumia fedha zake zilizokuwa zimezuiliwa kwa ajili ya kununua bidhaa za kilimo kutoka nchini Marekani.

    Akijibu madai hayo kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa X (zamani Twitter), Ghalibaf alitumia lugha ya dhihaka na picha kuelezea uhusiano wa sasa kati ya mataifa hayo mawili.

    Ghalibaf aliandika: “Inashangaza. Zao pekee tunalovuna sasa hivi ni lile mlilopanda ninyi wenyewe: miongo kadhaa ya kutoaminiana.”

    Kiongozi huyo aliendelea kufafanua kuwa “zao” hilo la kutoaminiana ni la asili, limejaa tele, na limeoteshwa nchini mwao kutokana na vitendo vya Marekani. Katika kile kinachoonekana kama shambulio la maneno dhidi ya ubora wa bidhaa na diplomasia ya Marekani, Ghalibaf aliongeza kuwa Marekani haina kingine cha kusafirisha nje isipokuwa soya za GMO (zilizobadilishwa vinasaba), ahadi zilizovunjika, na maneno ya kejeli.

    Kauli hii ya Ghalibaf imekuja wakati kukiwa na mivutano ya kidiplomasia kuhusu namna Iran itakavyotumia mabilioni ya dola ya mali zake ambazo zilikuwa zimezuiliwa nje ya nchi kutokana na vikwazo, na sasa zimeanza kuachiwa.

    Wakati Washington ikidai kuwa fedha hizo zinaweza kutumika kwa mahitaji ya kibinadamu ikiwemo chakula na kilimo, Tehran imesisitiza kuwa ina mamlaka kamili ya kuamua jinsi ya kutumia rasilimali zake bila kuingiliwa na nchi za Magharibi.

  • DAKIKA 80 ZA PATASHIKA: Jinsi Ghalibaf Alivyozima Mazungumzo na Marekani.

    DAKIKA 80 ZA PATASHIKA: Jinsi Ghalibaf Alivyozima Mazungumzo na Marekani.

    TEHRAN, IRAN – Spika wa Bunge la Iran, Mohammad Bagher Ghalibaf, amefichua mzozo mzito wa kidiplomasia uliopelekea upande wa Iran kusitisha ghafla mazungumzo na Marekani, kufuatia lugha ya vitisho kutoka kwa Rais wa nchi hiyo, Donald Trump.

    Akielezea mkasa huo uliotokea katikati ya vikao vya majadiliano, Ghalibaf amesema kuwa alipata taarifa za kushtua kwamba Trump ametoa matamshi ya kibeberu yakilenga kumtishia Rais wa Iran, timu ya majadiliano, pamoja na vitisho vya kushambulia ardhi ya nchi hiyo.

    Akizungumza kwa msimamo thabiti mbele ya mjumbe wa Marekani, naibu Rais, JD Vance, Spika Ghalibaf alimtaka mwanasiasa huyo kuelewa kuwa Iran haitayumbishwa.

    “Tuko hapa katika mazungumzo, na kwa mujibu wa makubaliano yaliyotiwa saini, kipengele cha kwanza kinakataza vitisho au shinikizo la aina yoyote. Hata hivyo, leo Rais wenu ametoa vitisho. Eleweni kuwa sisi hatujadiliani kamwe chini ya kivuli cha vitisho au shinikizo,” Ghalibaf alimweleza Vance kabla ya kuchukua uamuzi mgumu wa kusitisha mazungumzo hayo.

    Inaarifwa kuwa mara baada ya kutoa kauli hiyo, ujumbe wa Iran uliondoka ukumbini na kukataa kurejea mezani, licha ya upande wa Marekani kujaribu kutafuta namna ya kuonana tena kupitia nchi wasuluhishi.

    Licha ya jitihada za kidiplomasia zilizofanywa na wasuluhishi kutoka Qatar na Pakistan, Iran ilishikilia msimamo wake wa kutozungumza moja kwa moja na Marekani. Badala yake, Iran ilikubali kuwasiliana na wasuluhishi hao pekee ili kufikisha ujumbe wao.

    Mvutano huo wa kidiplomasia uliodumu kwa dakika 80, uliazimia kutoa msimamo wa mwisho ambao baadaye uliwasilishwa kupitia taarifa rasmi iliyotolewa na upande wa Qatar na Pakistan.

    Tukio hili linaashiria msimamo mkali wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kulinda heshima ya taifa hilo dhidi ya kile inachokiita kuwa ni sera za mabavu za mataifa ya Magharibi.