Lebo: Israel

  • Iran Yaweka Masharti 5 Kabla ya Kuendelea Mazungumzo na Marekani.

    Iran Yaweka Masharti 5 Kabla ya Kuendelea Mazungumzo na Marekani.

    Chanzo kimoja chenye taarifa kimesema kuwa Iran haitashiriki duru ya pili ya mazungumzo na Marekani hadi pale masharti matano ya kujenga imani yatakapotekelezwa.

    Kwa mujibu wa chanzo hicho, masharti hayo yanahusisha kusitishwa kwa vita katika maeneo yote hususan Lebanon, kuondolewa kwa vikwazo dhidi ya Iran, kuachiliwa kwa fedha za Iran zilizozuiwa nje ya nchi, kulipwa fidia kwa madhara yaliyotokana na vita pamoja na kutambuliwa kwa mamlaka ya Iran katika Mlango wa Hormuz.

    Chanzo hicho pia kilieleza kuwa Iran imeifikishia Pakistan, inayoshiriki kama mpatanishi, wasiwasi wake kuhusu kuendelea kwa mzingiro wa baharini katika Bahari ya Arabia na Ghuba ya Oman hata baada ya kusitishwa kwa mapigano. Tehran inaona hali hiyo kuwa ishara ya kutokuaminika kwa mazungumzo na Marekani.

    Iran imefafanua kuwa masharti hayo yana lengo la kujenga kiwango cha chini cha uaminifu kabla ya kurejea mezani kwa mazungumzo mapya. Viongozi wa Tehran wanaamini kuwa bila hatua za vitendo katika masuala hayo, mazungumzo mapya hayawezi kuanza.

    Taarifa hizo zinaeleza kuwa masharti hayo yalitolewa kama jibu kwa pendekezo la vipengele 14 kutoka Marekani, ambalo vyanzo vya Iran vinadai lilikuwa la upande mmoja na lililolenga zaidi maslahi ya Washington.

    Kwa mujibu wa vyanzo hivyo, Marekani ilikuwa ikijaribu kupitia mazungumzo kufanikisha baadhi ya malengo ambayo haikuweza kuyapata kupitia vita.

  • Marekani Yaonyesha Nguvu kwa Kufichua Manowari ya Nyuklia Karibu na Iran.

    Marekani Yaonyesha Nguvu kwa Kufichua Manowari ya Nyuklia Karibu na Iran.

    Marekani Yatangaza Kuwasili kwa Manowari ya Nyuklia Gibraltar.

    Jeshi la Wanamaji la Marekani limethibitisha hadharani kuwasili kwa manowari ya makombora ya balistiki ya daraja la Ohio katika eneo la Gibraltar, katika hatua nadra inayochukuliwa kama ishara ya kuonyesha nguvu.

    Kwa mujibu wa taarifa hiyo, uamuzi wa kutangaza hadharani harakati za manowari hiyo umevutia hisia za wachambuzi wa masuala ya usalama, kwani kwa kawaida vyombo hivyo hutumwa kwa usiri mkubwa kutokana na nafasi yake ya kimkakati katika mfumo wa silaha za nyuklia.

    Tangazo hilo linakuja wakati mvutano ukiendelea kuhusiana na mazungumzo ya kimataifa, usalama wa Mlango wa Hormuz, pamoja na kuongezeka kwa taharuki kati ya Marekani, Israel na Iran.

    Wataalamu wanasema hatua hiyo inaweza kutafsiriwa kama ujumbe wa kisiasa na kijeshi unaolenga kuashiria msimamo wa Marekani katika eneo hilo.

  • Ofisi ya Netanyahu yaishambulia Ulaya, yadai Israel inafanya “kazi chafu” kwa niaba yao.

    Ofisi ya Netanyahu yaishambulia Ulaya, yadai Israel inafanya “kazi chafu” kwa niaba yao.

    Ofisi ya Benjamin Netanyahu imetoa shutuma kali dhidi ya mataifa ya Ulaya kufuatia mfululizo wa ukosoaji kuhusu upanuzi wa makazi ya walowezi wa Israel katika eneo la Ukingo wa Magharibi linalokaliwa kwa mabavu.

    Katika taarifa rasmi iliyotolewa leo, ofisi ya kiongozi huyo wa Israel—ambaye amekuwa akitajwa na wakosoaji na mashirika ya kimataifa kama mhalifu wa vita—imesema kuwa nchi za Ulaya zinafanya unafiki.

    Taarifa hiyo imedai kuwa Israel na Marekani “zinaifanyia Ulaya kazi chafu” kwa kukabiliana kijeshi na Iran pamoja na makundi ya upinzani katika ukanda wa Mashariki ya Kati.

    Israel imewashutumu wanasiasa wa Ulaya kwa kile ilichokiita “kuinamia shinikizo za ndani za kisiasa,” ikilaani vikali hatua zozote zinazolenga kuwawekea vikwazo walowezi wa Israel. Katika kile kinachoonekana kama msisitizo wa kiitikadi, taarifa hiyo imetumia majina ya kibiblia ya “Yudea na Samaria” kurejelea eneo la Ukingo wa Magharibi.

    Licha ya upinzani mkubwa kutoka kwa jamii ya kimataifa, ofisi ya Netanyahu imesisitiza kuwa itaendelea kulinda na kuendeleza shughuli za walowezi katika eneo hilo, ikilitaja kama “ardhi ya mababu.”

    Aidha, Israel imetupilia mbali uwezekano wa kufuata vikwazo vyovyote vilivyowekwa na Ulaya dhidi ya walowezi wake, hatua inayozidi kuongeza mvutano wa kidiplomasia kati ya Israel na washirika wake wa zamani barani Ulaya.

  • Times of Israel yateta unyama wa mazayuni: “tumechupa mipaka yote ya ubinadamu”

    Times of Israel yateta unyama wa mazayuni: “tumechupa mipaka yote ya ubinadamu”

    Gazeti la Times of Israel limetoa tahariri likikosoa vikali tukio la kufukuliwa kwa kaburi la Mpalestina linalodaiwa kufanywa na walowezi wakiwa chini ya uangalizi wa jeshi la Israel.

    Gazeti hilo limeeleza kuwa kitendo hicho kimeibua maswali mazito ya kimaadili ndani ya jamii ya Israel.Kwa mujibu wa tahariri hiyo, tukio hilo lilitokea huku wanajeshi wakiwa karibu na eneo la tukio.

    Badala ya kuchukua hatua za kuzuia au kukomesha kitendo hicho, wanajeshi hao waliripotiwa kushuhudia bila kuingilia kati.

    Times of Israel imeeleza kuwa vitendo vya aina hiyo haviakisi nguvu, bali vinaashiria changamoto za kimaadili na vinakinzana na misingi ya Kiyahudi ambayo Israel hudai kuilinda.

    Gazeti hilo pia limeonya kuwa kuvumilia au kupuuza matukio kama hayo kunaweza kudhoofisha madai ya “tofauti ya kimaadili” ambayo Israel imekuwa ikiyasisitiza kwa muda mrefu.Katika tahariri hiyo, gazeti limehimiza kurejea katika misingi ya haki na huruma, likisema kuwa tabia zinazochukuliwa kuwa za “sumu” zinaweza kuathiri mshikamano na maadili ya jamii kwa ujumla.

  • Trump Azungumza na Netanyahu Kuhusu Majibu ya Iran, Akataa Pendekezo la Tehran

    Trump Azungumza na Netanyahu Kuhusu Majibu ya Iran, Akataa Pendekezo la Tehran

    Rais wa Marekani Donald Trump amesema amezungumza na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kuhusu majibu ya hivi karibuni ya Iran katika mazungumzo yanayoendelea kuhusu mgogoro huo.

    Trump alielezea mazungumzo yao kama “simu nzuri sana” na kusema kuwa Marekani ina uhusiano mzuri na Israel.Akizungumza kuhusu majibu ya Tehran, Trump alisema amekataa pendekezo jipya la Iran lililolenga kumaliza vita. Katika mahojiano na Axios, alisema haridhishwi na barua iliyotumwa na Iran, akisema kuwa haifai na kwamba hapendi majibu yao.

    Trump pia alitoa kauli kali dhidi ya Iran, akidai kuwa kwa muda wa miaka 47 nchi hiyo imekuwa ikitumia mbinu za udanganyifu dhidi ya mataifa mengi.

    Kauli hizo zinakuja baada ya Washington kusubiri kwa siku 10 kupokea majibu ya Tehran, huku mvutano ukiendelea na kukiwa na hofu ya kuongezeka tena kwa mgogoro. Hata hivyo, Trump hakutoa ufafanuzi iwapo mazungumzo yataendelea au kama uwezekano wa hatua za kijeshi bado unazingatiwa.

  • ‘Usaliti’ au Uhuru? tetesi UAE kujindoa katika umoja wa nchi za kiarabu ili kuikumbatia Israel

    ‘Usaliti’ au Uhuru? tetesi UAE kujindoa katika umoja wa nchi za kiarabu ili kuikumbatia Israel

    Baadhi ya vyanzo vya habari vinaripoti uwezekano wa Falme za Kiarabu (UAE) kujiondoa katika Umoja wa Nchi za Kiarabu, wiki moja baada ya kutangazwa kwa habari za kujiondoa kwa nchi hiyo kutoka kundi la nchi zinazouza nje mafuta (OPEC).

    Ingawa taarifa hiyo bado haijathibitishwa rasmi na mamlaka za UAE au Umoja wa Nchi za Kiarabu, wachambuzi wanasema hatua hiyo ingeashiria mabadiliko makubwa ya kimkakati katika sera ya nje ya Abu Dhabi. Mabadiliko hayo yanaweza kuathiri mustakabali wa moja ya taasisi kongwe zaidi katika ulimwengu wa Kiarabu.

    Umoja wa Nchi za Kiarabu, ambao ni miongoni mwa taasisi za zamani zaidi za ushirikiano wa kikanda katika Asia ya Magharibi, unaweza kukumbwa na athari kubwa endapo UAE itaamua kujiondoa rasmi.

    Nchi hiyo ni miongoni mwa wanachama wa mwanzo na pia ni moja ya mataifa yenye nguvu kiuchumi ndani ya umoja huo.Kwa mujibu wa wachambuzi wa masuala ya kisiasa, kuondoka kwa UAE kunaweza kuchukuliwa kama pigo kubwa kwa Umoja wa Nchi za Kiarabu, na huenda kukazua maswali kuhusu mustakabali wa taasisi hiyo yenye takribani miaka 80.Kwa upande wa UAE, hatua kama hiyo inaweza kusababisha ukosoaji na tuhuma za “usaliti” kutoka kwa baadhi ya nchi za Kiarabu katika muda mfupi.

    Hata hivyo, baadhi ya wachambuzi wanaamini kwamba katika muda mrefu inaweza kuipa Abu Dhabi uhuru mkubwa zaidi wa kimkakati katika sera zake za nje na kupunguza utegemezi wake kwa mfumo wa pan‑Arabism.