Lebo: Marekani

  • Ken Paxton Apata Ushindi wa Kishindo Dhidi ya Seneta John Cornyn katika Mchuano wa Texas.

    Ken Paxton Apata Ushindi wa Kishindo Dhidi ya Seneta John Cornyn katika Mchuano wa Texas.

    (TEXAS, MAREKANI) – Katika pigo jingine kubwa kwa mrengo wa chama cha Republican, Ken Paxton, anayeungwa mkono kwa dhati na Rais Donald Trump, amemshinda Seneta wa muda mrefu wa Marekani, John Cornyn, katika uchaguzi wa mchujo (primary runoff) jimboni Texas.

    Ushindi huo wa Paxton unamfanya Cornyn kuwa Seneta wa pili wa Republican kupoteza uteuzi wa chama chake ndani ya kipindi cha chini ya wiki mbili, baada ya Trump kuelekeza ushawishi wake dhidi ya maseneta hao. Matokeo haya yanatarajiwa kumlazimisha Seneta Cornyn, mwenye umri wa miaka 74, kustaafu siasa ifikapo mwaka ujao, huku yakilazimisha safu ya uongozi wa chama cha Republican kumuunga mkono Paxton licha ya kuwepo kwa upinzani wa muda mrefu dhidi yake ndani ya chama.

    Paxton, mwenye umri wa miaka 63, aliingia katika kinyang’anyiro hiki huku akikabiliwa na mfululizo wa kashfa za kisheria na kisiasa. Hata hivyo, hali ilibadilika ghafla na kumpa kasi ya kipekee baada ya kupokea baraka na uungaji mkono rasmi kutoka kwa Donald Trump wiki iliyopita, hatua iliyofuta mashaka ya wapiga kura na kumpa ushindi huu muhimu.

    Huu ni mwendelezo wa wimbi la ushawishi wa Trump ndani ya chama cha Republican, ambapo wagombea wanaopingwa naye wameendelea kupoteza viti vyao mbele ya wale wanaobeba ajenda yake.

  • Armenia nchi ya kwanza kununua Mtambo wa Ulinzi wa Iran “Majed” uliyopiga ndege za Marekani

    Armenia nchi ya kwanza kununua Mtambo wa Ulinzi wa Iran “Majed” uliyopiga ndege za Marekani

    TEHRAN/YEREVAN — Katika hatua inayoashiria mabadiliko makubwa ya kiusalama, taifa la Armenia inaripotiwa kusaini mkataba wa siri wa ununuzi wa silaha wenye thamani ya dola za Marekani milioni 500 na Iran. Kwa mujibu wa ripoti kutoka shirika la habari la Iran International, inayomilikiwa na Saudi Arabia mkataba huo unahusisha ununuzi wa mtambo wa kisasa wa ulinzi wa anga wa Majed, ulioundwa na kutengenezwa nchini Iran.

    Makubaliano haya yanatajwa kubeba uzito mkubwa, kwani yanagharimu takriban theluthi moja ya bajeti yote ya ulinzi ya Armenia kwa mwaka 2024, ambayo inasimama kwenye dola bilioni 1.4. Kwa upande mwingine, hatua hii inatoa fursa kwa Iran kurejesha na kuimarisha ushawishi wake wa kijeshi katika ukanda wa Caucasus Kusini.

    Wachambuzi wa masuala ya kiusalama wanaeleza kuwa uamuzi huu wa Armenia unachochewa na hofu inayoongezeka ya kiusalama kufuatia mivutano inayoendelea na jirani yake, Azerbaijan. Aidha, hatua hii inachukuliwa kama mbadala baada ya Armenia kuhisi kupungua kwa uungwaji mkono wa kijeshi kutoka kwa mshirika wake wa kihistoria, Urusi.

  • Iran: Hakuna Mazungumzo Mapya na Marekani Hadi Fedha Zilizozuiwa Zirejeshwe

    Iran: Hakuna Mazungumzo Mapya na Marekani Hadi Fedha Zilizozuiwa Zirejeshwe

    Shirika la Habari la Fars, likinukuu chanzo cha uhakika, limeripoti kuwa hakutakuwa na mazungumzo yoyote kati ya Iran na Marekani bila kufanyika kwa uhamishaji wa fedha za Iran zilizozuiwa. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, mzozo mkubwa wa hivi punde kati ya mataifa haya mawili kuelekea kuanza kwa mazungumzo, unahusu utaratibu wa kuiwezesha Iran kufikia mali zake hizo.

    Kwa mujibu wa chanzo hicho, suala la fedha za Iran zinazoshikiliwa linashughulikiwa kupitia juhudi za upatanishi zinazoongozwa na nchi ya Qatar. Imeelezwa pia kuwa hapo awali, Marekani ilikiuka ahadi zake kuhusiana na urejeshwaji wa mali hizo za Iran.

    Chanzo hicho kimeiambia Fars kuwa Iran imeshikilia msimamo wake thabiti, ikisisitiza kwamba maadamu fedha hizo zilizokubaliwa hazijahamishwa, hakuna makubaliano yoyote yanayoweza kufikiwa baina yao.

    Hata hivyo, mashauriano yanayoendelea nchini Qatar yameripotiwa kupiga hatua nzuri kuelekea kutatua kikwazo hicho.

    Licha ya hatua hiyo, chanzo hicho kimebainisha kuwa jopo la wapatanishi la Iran halichukulii maelewano hayo ya awali kama uamuzi wa mwisho, hasa kutokana na rekodi ya Marekani ya kukiuka makubaliano huko nyuma. Kimeongeza kuwa Iran imethibitisha kuwa iko tayari kwa hatua na chaguzi zote zinazoweza kujitokeza.

  • Marekani Yakanusha Madai ya Kuanza Tena Kusindikiza Meli Lango la Hormuz

    Marekani Yakanusha Madai ya Kuanza Tena Kusindikiza Meli Lango la Hormuz

    Ripoti zinazokinzana zimeibuka kufuatia madai ya gazeti la Wall Street Journal (WSJ) kwamba Marekani imeanza tena operesheni ya kutoa msaada na ulinzi kwa meli zinazopita katika Ghuba ya Uajemi.

    Awali, gazeti hilo liliripoti madai kutoka kwa maafisa wa kijeshi wa Marekani yakieleza kuwa Jeshi la Majini la nchi hiyo linaendeleza tena utaratibu wa kusaidia meli zinazovuka Lango la Hormuz. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, meli moja kubwa ya mafuta ya Ugiriki iliyokuwa imesheheni mapipa milioni mbili ya mafuta ghafi, ilidaiwa kusindikizwa na Jeshi la Majini la Marekani ilipokuwa ikipita kwenye pwani ya Oman.

    Hata hivyo, Kamandi Kuu ya Jeshi la Marekani (CENTCOM) imejitokeza na kutoa taarifa rasmi kukanusha vikali madai hayo. CENTCOM imefafanua wazi kuwa operesheni hiyo ya ulinzi bado haijaanza tena.

    Katika taarifa yake, kamandi hiyo imesisitiza kuwa, kwa sasa, vikosi vya Marekani havisindikizi wala kuongoza meli yoyote ya kibiashara katika eneo hilo lenye umuhimu mkubwa wa kimkakati la Lango la Hormuz.

  • Jarida la The New Yorker: Makubaliano Yoyote na Iran, Yatakuwa Fedheha kwa Trump.

    Jarida la The New Yorker: Makubaliano Yoyote na Iran, Yatakuwa Fedheha kwa Trump.

    WASHINGTON – Jarida la Marekani la The New Yorker limeripoti kuwa makubaliano yoyote yatakayofikiwa na Donald Trump kwa ajili ya kumaliza mzozo na Iran yatakuwa ya fedheha kwake, kutokana na mazingira magumu aliyoyatengeneza yeye mwenyewe.

    Kwa mujibu wa uchambuzi wa chombo hicho cha habari, vita dhidi ya Iran vimegeuka na kuwa “kushindwa kimkakati” kwa upande wa Marekani, huku serikali ya Iran kwa sasa ikijikuta katika nafasi yenye nguvu zaidi kuliko ilivyokuwa hapo awali.

    Ripoti hiyo inaeleza kuwa katika hali ya sasa, Trump amelazimika kufanya maamuzi kati ya chaguo “baya” na “baya zaidi,” na inaonekana wazi kuwa ameelekea kwenye chaguo ambalo ni “baya sana.” Inadaiwa kuwa chini ya mfumo wa makubaliano hayo yaliyopendekezwa, Iran haitapata tu fedha taslimu, bali pia itanufaika na kuondolewa kwa vikwazo vya kiuchumi.

    Jarida hilo linahitimisha kwa mtazamo kuwa, vita vilivyoanzishwa kwa lengo la kuiangusha serikali ya Iran, katika uhalisia wake, vimeishia kuipa nguvu na kuiimarisha serikali hiyo zaidi.

  • Marekani Yathibitisha Kufanya Mashambulizi Kusini mwa Iran, Yakana Kukiuka Usitishaji wa Vita.

    Marekani Yathibitisha Kufanya Mashambulizi Kusini mwa Iran, Yakana Kukiuka Usitishaji wa Vita.

    Makubaliano ya kusitisha mapigano yameripotiwa kukiukwa na Marekani kufuatia uthibitisho kutoka kwa vikosi vyake kuhusu kutekeleza mashambulizi katika maeneo ya kusini mwa Iran.

    Kwa mujibu wa shirika la habari la Fox News, likinukuu taarifa kutoka Kamandi Kuu ya Marekani (CENTCOM), mashambulizi hayo yalilenga maalum vituo vya kurushia makombora pamoja na boti zilizokuwa zikijaribu kutega mabomu (mina) baharini.

    Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Msemaji wa Kamandi Kuu ya Marekani ameeleza kuwa vikosi vyao vilitekeleza mashambulizi hayo siku ya Jumatatu kusini mwa Iran. Hata hivyo, msemaji huyo ametetea hatua hiyo akidai kuwa ilichukuliwa kwa lengo la kujilinda dhidi ya vitisho vya kiusalama.