Lebo: Rwanda

  • Marekani yaiwekea vikwazo Rwanda kwa tuhuma za magendo ya Dhahabu

    Marekani yaiwekea vikwazo Rwanda kwa tuhuma za magendo ya Dhahabu

    KIGALI/WASHINGTON – Serikali ya Marekani imetangaza hatua kali za kiuchumi dhidi ya watu wawili na makampuni manne ya madini nchini Rwanda, ikituhumiwa kuhusika katika mnyororo wa biashara haramu ya madini inayochochea machafuko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

    Vikwazo hivyo vimekuja baada ya uchunguzi wa kina wa Washington kubaini kuwa wahusika hao wamekuwa wakisaidia biashara ya magendo ya dhahabu, ambayo mapato yake yanatumiwa kufadhili shughuli za kundi la waasi wa M23. Kundi hilo limekuwa likilaumiwa kwa kusababisha mivutano ya kiusalama na maafa ya kibinadamu katika ukanda wa Maziwa Makuu.

    Katika taarifa yake, Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imekitaja kiwanda cha kusafisha dhahabu cha Gasabo kilichopo jijini Kigali, kuwa kiungo muhimu na kituo kikuu cha kupitisha dhahabu inayotoka DRC kinyume cha sheria. Inaripotiwa kuwa mapema mwaka huu wa 2026, takriban kilo 60 za dhahabu zilipitishwa kupitia kiwanda hicho kwenda masoko ya nje.

    Mbali na makampuni hayo, vikwazo hivyo vimejumuisha viongozi waandamizi wa kampuni hizo, hatua inayolenga kuzuia mali zao na kuwazuia kufanya miamala yoyote ya kifedha inayohusisha taasisi za Marekani.

    Hatua hii ya Washington inatazamwa kama shinikizo jipya kwa serikali ya Kigali, ikitaka hatua madhubuti kuchukuliwa kukata mnyororo wa kifedha unaolisha makundi ya waasi mashariki mwa Kongo. Hadi sasa, viongozi wa kampuni zilizotajwa na serikali ya Rwanda hawajatoa tamko rasmi kufuatia hatua hiyo ya Marekani.

  • Felicien Kabuga Mtuhumiwa wa Mauwaji ya Kimbari nchini Rwanda aaga dunia

    Felicien Kabuga Mtuhumiwa wa Mauwaji ya Kimbari nchini Rwanda aaga dunia

    Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita (ICC) yenye makao yake The Hague imetangaza kuwa mshukiwa wa mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 nchini Rwanda, Félicien Kabuga, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 90.

    Taarifa zinaeleza kuwa Kabuga alifariki Jumamosi alipokuwa akipatiwa matibabu hospitalini, huku Jaji Graciela Gatti Santana ameamuru uchunguzi wa haraka kufanyika ili kubaini chanzo cha kifo hicho.Kabuga alikuwa miongoni mwa watu waliotafutwa zaidi duniani kwa tuhuma za kuhusika katika kupanga na kuchochea mauaji ya takribani watu laki nane waliouawa kati ya Aprili na Juni 1994 nchini Rwanda.

    Alikamatwa nchini Ufaransa mwaka 2020 kabla ya kuhamishiwa The Hague, ambako alikabiliwa na mashtaka ya mauaji ya kimbari, njama za kutekeleza mauaji hayo pamoja na uhalifu dhidi ya ubinadamu.