Lebo: Saudi

  • Saudi Arabia yaanza kupunguza uwekezaji mkubwa katika michezo, kunani?

    Saudi Arabia yaanza kupunguza uwekezaji mkubwa katika michezo, kunani?

    Saudi Arabia imeanza kujiondoa katika baadhi ya miradi yake mikubwa ya uwekezaji, hasa katika sekta ya michezo, kwa mujibu wa ripoti ya gazeti la The New York Times.

    WKatika kipindi cha takribani muongo mmoja uliopita, nchi hiyo chini ya uongozi wa Mwanamfalme Mohammed bin Salman iliwekeza fedha nyingi katika michezo na burudani ikiwa ni sehemu ya juhudi za kupunguza utegemezi wa uchumi wake kwa mafuta na kuboresha taswira yake kimataifa.

    Hata hivyo, kupungua kwa mapato ya mafuta, kuongezeka kwa gharama za matumizi, pamoja na shinikizo la mizozo ya kikanda, kumesababisha baadhi ya miradi hiyo kupunguzwa au kusimamishwa.

    Miongoni mwa miradi inayotajwa ni mradi wa mashindano ya gofu wa LIV, ambao ulianzishwa kwa uwekezaji wa mabilioni ya dola na ulihusisha ushiriki wa wachezaji mashuhuri. Saudi Arabia imeripotiwa kutangaza kuwa haitauendelea kuufadhili mradi huo baada ya mwisho wa mwaka huu.

    Hatua hiyo inaashiria mabadiliko ya mkakati wa kiuchumi wa Saudi Arabia, ambapo sasa inaelekeza zaidi nguvu katika uwekezaji wa ndani na kuongeza ufanisi wa matumizi—jambo linaloweza pia kuwa na athari katika sekta ya michezo duniani.

  • Saudi Arabia yafunga anga na kambi zake za kijeshi kwa Marekani

    Saudi Arabia yafunga anga na kambi zake za kijeshi kwa Marekani

    Vyanzo vyenye taarifa katika eneo la Ghuba ya Uajemi vimeripoti kuwa Saudi Arabia imefunga anga yake pamoja na baadhi ya kambi zake za kijeshi kwa matumizi ya Marekani.

    Hatua hiyo inadaiwa kuchukuliwa baada ya Riyadh kukosa dhamana za usalama kutoka Washington dhidi ya uwezekano wa mashambulizi ya makombora kutoka Iran.

    Kwa mujibu wa ripoti iliyochapishwa na mtandao wa habari wa Israel, i24News, Saudi Arabia imesema vikwazo hivyo vitaendelea hadi Marekani itakapotoa dhamana za wazi za ulinzi dhidi ya mashambulizi yanayoweza kutokea.

    Vyanzo hivyo vimeeleza kuwa viongozi wa Saudi Arabia wanaamini Iran itaendelea kuwa na ushawishi hata kama itafikia makubaliano na Marekani, jambo linaloifanya Riyadh kutaka kuepuka kuhusika moja kwa moja katika mvutano wowote na Tehran.

    Ripoti hiyo pia inaeleza kuwa Saudi Arabia itaendelea kupunguza matumizi ya anga yake na kambi zake na Marekani kwa shughuli zinazohusiana na kile kilichoitwa “Mradi wa Uhuru”, hadi Washington itakapoweka wazi mipango yake ya kijeshi na kutoa ulinzi unaofaa dhidi ya mashambulizi ya Iran.

    Hata hivyo, vyanzo katika eneo la Ghuba vimesisitiza kuwa hatua hiyo haimaanishi Saudi Arabia inapinga ushirikiano wake na Marekani, bali inalenga kupunguza hatari ya kushambuliwa na makombora ya Iran.