Lebo: habari

  • Utawala wa Trump Wapanga Mikakati Mipya ya Kurejesha Usafiri wa Meli katika Lango la Hormuz

    Utawala wa Trump Wapanga Mikakati Mipya ya Kurejesha Usafiri wa Meli katika Lango la Hormuz

    WASHINGTON D.C. – Utawala wa Rais Donald Trump umeanza mchakato wa kutafuta njia mbadala za kurejesha kikamilifu usafirishaji wa meli za mafuta kupitia Lango la Hormuz, hatua inayolenga kuimarisha biashara ya kimataifa katika njia hiyo muhimu ya maji.

    Kwa mujibu wa ripoti kutoka shirika la POLITICO, Rais Trump pamoja na Mkuu wa Wafanyakazi wa Ikulu, Susie Wiles, wametoa maelekezo kwa maafisa husika kubuni mikakati itakayowahamasisha wamiliki wa meli na makampuni ya bima kurejea kufanya kazi katika eneo hilo, licha ya kuendelea kwa mazungumzo ya kidiplomasia kati ya Marekani na Iran.

    Miongoni mwa mapendekezo yaliyo mezani ni kuanzishwa kwa mfumo wa “VIP,” ambapo wamiliki wa meli watalipia ada maalum ili kupata kipaumbele cha kupita katika njia hiyo, huku wakipewa ulinzi wa karibu na vikosi vya wanamaji vya Marekani.

    Aidha, utawala huo unatafakari kutumia Sheria ya Uzalishaji wa Ulinzi (Defense Production Act) ili kuwalazimisha watoa huduma za bima nchini Marekani kutoa bima kwa meli zinazopita katika eneo hilo, hatua inayolenga kupunguza hofu ya kiusalama kwa wafanyabiashara.

    Mkakati huu pia unalenga kushinikiza mataifa ya Ulaya kuongeza ushiriki wake katika operesheni za kulinda usalama wa baharini katika kanda hiyo, ili kuhakikisha utulivu wa muda mrefu wa usafirishaji wa nishati duniani.

  • Hillary Clinton: Netanyahu Anatumia Vita Kujinusuru Kisiasa

    Hillary Clinton: Netanyahu Anatumia Vita Kujinusuru Kisiasa

    Mwanasiasa mkongwe wa Marekani, Hillary Clinton, amedai kuwa Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, anaamini kuwa vita vinaweza kumsaidia kisiasa wakati huu ambapo anakabiliwa na shinikizo kubwa kutoka pande mbalimbali za upinzani.

    Akizungumza kuhusu hali ya kisiasa nchini Israel, Clinton alisema Netanyahu anajaribu kudhibiti upinzani unaoongezeka kwa kuchochea migogoro, akiamini kuwa hali ya taharuki ya vita inaweza kuwafanya wananchi kuungana nyuma ya uongozi wake.

    Kwa mujibu wa Clinton, mkakati huo unalenga kuhamisha mjadala wa kisiasa kutoka kwenye changamoto za ndani kwenda kwenye masuala ya usalama wa taifa, jambo ambalo mara nyingi huongeza uungwaji mkono kwa viongozi walioko madarakani.

    Hata hivyo, Clinton anaamini kuwa makubaliano ya kusitisha vita kati ya Marekani na Iran yanaweza kuwa hatua muhimu itakayobadilisha mwelekeo wa siasa za Israel. Amesema suala hilo linaweza kuwa “tone la mwisho” litakalosababisha kuongezeka kwa shinikizo dhidi ya Netanyahu na hatimaye kufungua nafasi ya kuondoka kwake madarakani katika uchaguzi ujao.

  • “Hatupokei wachochezi” Austria yampiga marufuku waziri wa Israel, Itamar Ben-Gvir

    “Hatupokei wachochezi” Austria yampiga marufuku waziri wa Israel, Itamar Ben-Gvir

    VIENNA, AUSTRIA – Shinikizo dhidi ya viongozi wenye msimamo mkali nchini Israel limezidi kupamba moto barani Ulaya baada ya nchi ya Austria kutangaza kuunga mkono pendekezo la kupigwa marufuku kwa Waziri wa Usalama wa Taifa wa nchi hiyo, Itamar Ben-Gvir, kuingia barani humo.

    Kwa mujibu wa ripoti iliyochapishwa na gazeti la Kronen Zeitung, idadi ya wanasiasa mashuhuri ndani ya Umoja wa Ulaya (EU) wanaotaka kuwekewa vikwazo kwa wajumbe wa baraza la mawaziri la utawala wa Israel imeendelea kuongezeka. Hatua hiyo inakuja kutokana na mfululizo wa ghasia na ukandamizaji unaofanywa dhidi ya Wapalestina katika eneo la Ukingo wa Magharibi (West Bank).

    Katika msimamo mkali zaidi, mwanasiasa mashuhuri wa Austria, Beate Meinl-Reisinger, amejitokeza waziwazi kupinga vitendo vya Waziri Ben-Gvir, ambaye anajulikana kwa sera zake kali za mrengo wa kulia.

    Akizungumza siku ya Jumatatu pambezoni mwa mkutano wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Umoja wa Ulaya uliofanyika mjini Luxembourg, Meinl-Reisinger alibainisha kuwa mienendo ya waziri huyo haikubaliki. Alisisitiza kuwa msimamo huo unatokana na dharau na tabia za kikatili ambazo Ben-Gvir amekuwa akizionesha, hususan dhidi ya wahudumu na washiriki wa misafara ya kutoa misaada ya kibinadamu kuelekea Ukanda wa Gaza.

    “Mtu huyu hakaribishwi hapa kwetu,” alikaririwa Meinl-Reisinger, akionyesha msisitizo wa Austria katika kuungana na mataifa mengine wanachama wa EU yanayotaka kuwajibishwa kwa viongozi wanaochochea uvunjifu wa haki za binadamu.

    Hatua hii ya Austria inatajwa kuwa pigo kadiplomasia kwa serikali ya Israel, ikizingatiwa kuwa mataifa mengi ya Ulaya sasa yanaanza kuchukua hatua madhubuti za kivitendo badala ya kutoa matamko ya kulaani pekee.

  • “Bila mimi, Israel haitakuwepo” – rais Trump apiga mkwara mzito, akosoa mashambulizi ya Beirut

    “Bila mimi, Israel haitakuwepo” – rais Trump apiga mkwara mzito, akosoa mashambulizi ya Beirut

    WASHINGTON, MAREKANI

    Rais wa Marekani, Donald Trump, amedai kuwepo kwa taifa la Israel kunategemea mchango wake binafsi, huku akionyesha kutoridhishwa na namna nchi hiyo inavyoendesha operesheni zake za kijeshi nchini Lebanon.

    Katika mfululizo wa matamshi yake ya hivi karibuni, Rais Trump amesisitiza kuwa bila jitihada na ulinzi wake, taifa la Israel lisingekuwa na uwezo wa kuendelea kuwepo duniani. “Bila mimi, hakutakuwa na Israel,” alikaririwa kiongozi huyo.

    Aidha, Rais Trump amefichua kuwa amewasilisha ujumbe kwa serikali ya Israel akieleza kuwa haungi mkono mashambulizi yanayofanywa na jeshi la nchi hiyo katika mji wa Beirut, Lebanon. Trump amebainisha kuwa amechukizwa na namna Israel inavyoshughulikia mgogoro wa Lebanon, akisema kuwa hali hiyo hairidhishi.

    Katika kile kinachoonekana kama shinikizo la wazi kwa uongozi wa Israel, Rais Trump amemtaka Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu kuongeza umakini na kuwa na uwajibikaji mkubwa zaidi kuhusiana na hatua zinazochukuliwa dhidi ya Lebanon.

    “Sijafurahishwa na jinsi Israel inavyoshughulika na Lebanon. Netanyahu lazima sasa awe na uwajibikaji zaidi,” aliongeza Rais Trump.

    Kauli hizi za Rais Trump zinakuja wakati ambapo hali ya usalama Mashariki ya Kati ikiendelea kuwa tete, huku kiongozi huyo akisisitiza msimamo wake juu ya hatma ya kanda hiyo na ushirika kati ya Marekani na Israel.

  • Uingereza kufadhili Nishati ya Nyuklia Ukraine: Mkakati wa Pauni Milioni 210 Wafikiwa G7

    Uingereza kufadhili Nishati ya Nyuklia Ukraine: Mkakati wa Pauni Milioni 210 Wafikiwa G7

    Waziri Mkuu wa Uingereza, Keir Starmer, ametoa ahadi nzito katika mkutano wa kilele wa G7 kwa kuweka bayana mkakati mpya wa kuimarisha usalama wa nishati nchini Ukraine.

    Katika hatua inayolenga kudumisha utulivu wa umeme na viwanda nchini humo, Uingereza imekubaliana kuipatia Ukraine urani iliyoboreshwa (enriched uranium) kwa ajili ya matumizi katika mitambo ya nyuklia hadi mwaka 2028. Mpango huu, unaoungwa mkono na ufadhili wa pauni milioni 210 kutoka kwa serikali ya Uingereza, unalenga kuipa Ukraine uhakika wa nishati katika kipindi hiki kigumu.

    Hatua hii inatazamwa kama nguzo muhimu ya ushirikiano wa kimataifa, ikiiwezesha Ukraine kujimudu kiuchumi na kupunguza utegemezi wa rasilimali za nje wakati huu wa changamoto za kiusalama.

  • Lukashenko aiwashia moto Israel: “Hakuna tukio la kihistoria linalohalalisha mauaji ya watoto Gaza”

    Lukashenko aiwashia moto Israel: “Hakuna tukio la kihistoria linalohalalisha mauaji ya watoto Gaza”

    MINSK, BELARUS

    Rais wa Belarus, Alexander Lukashenko, ametoa tamko zito na la kulaani vikali hatua za kijeshi zinazochukuliwa na Israel katika Ukanda wa Gaza, akihoji uhalali wa mashambulizi hayo dhidi ya raia wasio na hatia.

    Katika kile kinachoonekana kama ukosoaji mkali zaidi kutoka kwake tangu kuanza kwa mzozo huo, Rais Lukashenko ameitaka serikali ya Israel kurejea katika hali ya kawaida na kutafakari upya mustakabali wake.

    Hoja Kuhusu Mauaji na Historia
    Akizungumzia kadhia hiyo, Lukashenko amepuuzia hoja ya kutumia historia ya ‘Holocaust’ (maangamizi makuu ya Wayahudi) kama ngao ya kutekeleza mauaji ya sasa.

    “Ni tukio gani la Holocaust ambalo Waisrael wanalizungumzia, linaloweza kuhalalisha mauaji ya watu wengi kiasi hiki, hasa wanawake na watoto?” alihoji Lukashenko kwa mshangao.

    Aliongeza kuwa idadi kubwa ya watoto wamepoteza maisha Gaza na kwamba jeshi la Israel limefuta kila kitu katika uso wa dunia ndani ya eneo hilo.

    Upumbavu Mtupu
    Rais huyo pia amekemea vikali kile alichokiita kuwa ni mipango ya “ajabu” inayodaiwa kupangwa na baadhi ya watu nchini Israel. Lukashenko ameshutumu taarifa za kuwepo kwa nia ya kujenga maeneo ya mapumziko na starehe (resorts) juu ya maeneo yaliyoharibiwa ambayo bado yana miili ya watu.

    “Sasa wanazungumzia kujenga aina fulani ya maeneo ya starehe juu ya mifupa ya wafu. Huo ni upumbavu mtupu,” alisema Rais Lukashenko.

    Onyo kwa Israel
    Katika hitimisho la kauli yake, kiongozi huyo wa Belarus ametoa onyo akisema kuwa ni wakati muafaka kwa Israel kuzinduka na kutathmini kwa kina namna mataifa mengine yanavyoichukulia na jinsi itakavyoweza kuendelea kuwepo hapo baadaye.

    “Israel inahitaji kurejea katika fahamu zake na kutafakari juu ya kuwepo kwake hapo baadaye,” alisisitiza kiongozi huyo.

    Kauli hii ya Lukashenko inakuja wakati shinikizo la kimataifa likizidi kuongezeka dhidi ya Israel kutokana na hali mbaya ya kibinadamu inayoshuhudiwa katika Ukanda wa Gaza.