Lebo: habari

  • Iran Yasema Iko Tayari Kukabiliana na Uchokozi Wowote Mpya.

    Iran Yasema Iko Tayari Kukabiliana na Uchokozi Wowote Mpya.

    Wizara ya Ulinzi ya Iran imesema jeshi la nchi hiyo liko tayari kikamilifu kukabiliana na shambulio lolote jipya linaloweza kufanywa dhidi ya Iran na Marekani au Israel.

    Akizungumza kando ya hafla ya kumbukumbu iliyofanyika katika mji wa Rey, msemaji wa Wizara ya Ulinzi, Brigedia Jenerali Reza Talaei‑Nik, alisema majeshi ya Iran yako tayari kujibu vikali jaribio lolote la uchokozi.

    Hafla hiyo iliandaliwa kuwaenzi aliyekuwa Waziri wa Ulinzi, Meja Jenerali Aziz Nasirzadeh, pamoja na wenzake waliouawa katika shambulio la kigaidi linalodaiwa kufanywa na Marekani na Israel wakati wa vita vya hivi karibuni vilivyolazimishwa dhidi ya Iran.

    Kwa mujibu wa Talaei‑Nik, vita hivyo dhidi ya Iran vilifichua kile alichokitaja kuwa udhaifu wa Marekani, akisema mataifa mengi duniani sasa yanatambua kupungua kwa ushawishi wa upande mmoja wa Marekani katika siasa za kimataifa.

    Pia alizungumzia matokeo ya vita hivyo, akisema viongozi wa Marekani na Israel wanakosolewa na watu wengi duniani kutokana na matendo yao wakati wa mzozo huo na katika maeneo mengine.

    Talaei‑Nik aliongeza kuwa upinzani na ulinzi wa Iran wakati wa vita hivyo umechangia kuimarisha wazo la mfumo wa kimataifa wa ushirikiano wa pande nyingi badala ya utegemezi wa upande mmoja.

    Katika hotuba yake, alimkumbuka Meja Jenerali Nasirzadeh akisema kuwa katika kipindi cha miezi 18 aliyohudumu katika Wizara ya Ulinzi alitoa mchango mkubwa, hususan katika maendeleo na uzalishaji wa vifaa vya kijeshi.

    Msemaji huyo alisema wenzake na wafanyakazi wa wizara hiyo wamejipanga kuendeleza kazi na maono ya makamanda waliouawa, kwa dhamira na kujitolea sawa na walivyokuwa nao.

  • Mwanaharakati Fransis Awino amefungua kesi ili kupinga ongezeko la bei ya mafuta

    Mwanaharakati Fransis Awino amefungua kesi ili kupinga ongezeko la bei ya mafuta

    Mwanaharakati Francis Awino amefungua kesi katika Mahakama Kuu ya Nairobi kupinga ongezeko la hivi karibuni la bei ya mafuta lililotangazwa na Mamlaka ya Kudhibiti Nishati na Petroli (EPRA) tarehe 14 Mei 2026.Kesi hiyo, iliyowasilishwa chini ya Kitengo cha Katiba na Haki za Kibinadamu, inalenga kuhoji uhalali wa uamuzi huo, huku Awino akidai kuwa hatua hiyo imeweka mzigo mkubwa kwa wananchi na kukiuka haki za kikatiba kutokana na ukosefu wa uwazi pamoja na ushirikishwaji wa umma.Kwa mujibu wa nyaraka za mahakama, EPRA ilitangaza ongezeko la Sh16.65 kwa kila lita ya petroli na Sh46.29 kwa kila lita ya dizeli, hatua ambayo imeibua malalamiko kutoka kwa wadau mbalimbali wa uchumi.Awino anasisitiza kuwa ongezeko hilo limeathiri kwa kiasi kikubwa sekta mbalimbali, ikiwemo usafirishaji, kilimo, biashara ndogo ndogo, pamoja na kaya zinazotegemea bidhaa zinazotokana na mafuta.Aidha, mwanaharakati huyo ameibua wasiwasi kuhusu matumizi ya zaidi ya Sh5 bilioni kutoka mfuko wa Petroleum Development Levy Fund, akitaka serikali kutoa maelezo ya kina kuhusu namna fedha hizo zilivyotumika katika kupunguza bei ya dizeli na mafuta ya taa.Katika hoja nyingine, Awino amepinga uamuzi wa serikali kuruhusu kwa muda matumizi ya mafuta yenye kiwango cha juu cha salfa, akionya kuwa hatua hiyo inaweza kuhatarisha afya ya wananchi pamoja na mazingira.Pia amehoji utekelezaji wa tangazo la serikali la kupunguza ushuru wa VAT kwa bidhaa za petroli hadi asilimia nane mwezi Aprili mwaka huu, akidai kuwa wananchi hawajaona manufaa yoyote kutokana na hatua hiyo.Kupitia ombi la dharura lililowasilishwa katika Mahakama Kuu ya Milimani, Awino anaitaka mahakama kuingilia kati na kusitisha mara moja utekelezaji wa ongezeko hilo, akionya kuwa hali ya sasa inaweza kusababisha maandamano na taharuki nchini.Kesi hiyo inawasilishwa wakati ambapo maandamano yanatarajiwa kufanyika kesho kupinga kupanda kwa bei ya mafuta nchini Kenya.

  • James Orengo: Niko tayari kukabiliana na Ruto katika uchaguzi wa mwaka 2027

    James Orengo: Niko tayari kukabiliana na Ruto katika uchaguzi wa mwaka 2027

    Gavana wa Siaya, James Orengo, ametangaza nia ya kugombea urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2027, hatua inayotafsiriwa na wachambuzi kama mwanzo wa mapambano makali dhidi ya Rais William Ruto.Tangazo hilo linafuatia mashauriano ya kisiasa yaliyodumu kwa wiki kadhaa katika maeneo mbalimbali, ikiwemo Nairobi, Magharibi mwa Kenya na Nyanza, ambako wafuasi wake wamekuwa wakimsukuma kuingia katika siasa za kitaifa. Kilichoanza kama mikutano ya kawaida ya ODM sasa kimebadilika na kuwa kampeni ya wazi ya kumtambulisha kama kiongozi wa upinzani.Orengo anashirikiana kwa karibu na kundi la “Linda Mwananchi” pamoja na viongozi kama Edwin Sifuna na Babu Owino, akisisitiza kuwa ODM ina hazina ya viongozi wanaoweza kuwania urais. Hata hivyo, wachambuzi wanaona hatua yake pia inalenga kujiimarisha kama kiongozi wa kisiasa wa jamii ya Waluo na kujiweka tayari kwa miungano ya kisiasa ya baadaye.Akiwahutubia wananchi katika maeneo ya Muhoroni na Nyakach, Orengo alisisitiza umuhimu wa jamii ya Waluo kuwa na mgombea urais ili kuongeza nguvu ya mazungumzo ya kisiasa kitaifa. Alijitaja kama mrithi wa kisiasa wa Jaramogi Oginga Odinga na akasema yuko tayari kumpa changamoto Rais Ruto.Aidha, alikosoa serikali kwa kupanda kwa gharama ya maisha na matatizo ya kiuchumi, akitaja kufungwa kwa viwanda vya sukari, hali mbaya ya miundombinu na migogoro ya mara kwa mara katika eneo la Sondu. Pia alizungumzia kusuasua kwa mradi wa bwawa la Koru-Soin, hali inayosababisha mafuriko ya kila mwaka Nyakach.Orengo alisisitiza kuwa iwapo atachaguliwa, atarejesha viwanda vya sukari chini ya umiliki wa umma. Pia aliwataka viongozi wanaotaka kuchaguliwa tena kuungana naye au wakabiliwe na hatari ya kushindwa uchaguzi wa 2027.Hata hivyo, bado hajaweka wazi iwapo atagombea kupitia ODM au chama kingine, licha ya kusisitiza kuwa yeye ni kiongozi ndani ya chama hicho. Tangazo lake linajiri wakati mjadala kuhusu uongozi na mgombea wa urais ndani ya ODM ukiendelea.Iwapo atawasilisha rasmi azma yake, hii itakuwa mara ya pili kwa Orengo kuwania urais tangu jaribio lake la mwaka 2002 kupitia chama cha SDP.

  • Droni ya Marekani “MQ-9 Reaper” yadunguliwa mkoani Marib, Yemen

    Droni ya Marekani “MQ-9 Reaper” yadunguliwa mkoani Marib, Yemen

    Yemen wadai kuitungua droni ya Marekani aina ya MQ-9 Reaper katika eneo la Safer, mkoani Marib.Mpaka sasa, hakuna tamko rasmi lililotolewa na msemaji wa jeshi la Yemen, Yahya Saree, kuhusu tukio hilo. Kwa upande mwingine, jeshi la Marekani bado halijathibitisha wala kukanusha madai ya kupotea kwa droni hiyo.

  • Marekani na Israeli Zipo Tayari kwa Uwezekano wa Mashambulizi Dhidi ya Iran.

    Marekani na Israeli Zipo Tayari kwa Uwezekano wa Mashambulizi Dhidi ya Iran.

    Kulingana na duru za kijeshi kutoka nchini Israeli zilizokaririwa na shirika la habari la Kan News, majeshi ya Marekani na Israeli yamewekwa katika hali ya tahadhari ya juu, yakijiandaa kwa uwezekano wa kuanzisha tena mashambulizi dhidi ya Iran.

    Imeelezwa kuwa operesheni yoyote mpya ya kijeshi itakayofanyika itakuwa ni ya ushirikiano wa pamoja kati ya mataifa hayo mawili.Kwa mujibu wa ripoti hiyo, mikakati ya sasa ya Israeli inalenga hasa kushambulia na kudhoofisha miundombinu mikuu ya nishati ya taifa la Iran.

    Serikali ya Israeli inaamini kuwa hatua hii itaishinikiza Tehran kulegeza msimamo wake katika meza ya mazungumzo. Hata hivyo, wachambuzi wa masuala ya kiusalama wanaonyesha wasiwasi wao, wakitilia shaka ikiwa shinikizo hilo la kijeshi litaifanya Iran kusalimu amri na kukubaliana na matakwa hayo.

    Katika hatua inayoashiria uzito wa hali hiyo, imeripotiwa kuwa Donald Trump na Waziri Mkuu wa Israeli, Benjamin Netanyahu, wamefanya mazungumzo ya simu ya zaidi ya dakika 30 hii leo. Katika mazungumzo hayo, suala la uwezekano wa kurejea katika mapigano lilijadiliwa kwa kina. Maafisa wa ngazi za juu wa Israeli wameweka wazi na kusisitiza kuwa, hatima na uamuzi wa mwisho wa kuanzisha tena mapigano hayo upo mikononi mwa Donald Trump.

  • Felicien Kabuga Mtuhumiwa wa Mauwaji ya Kimbari nchini Rwanda aaga dunia

    Felicien Kabuga Mtuhumiwa wa Mauwaji ya Kimbari nchini Rwanda aaga dunia

    Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita (ICC) yenye makao yake The Hague imetangaza kuwa mshukiwa wa mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 nchini Rwanda, Félicien Kabuga, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 90.

    Taarifa zinaeleza kuwa Kabuga alifariki Jumamosi alipokuwa akipatiwa matibabu hospitalini, huku Jaji Graciela Gatti Santana ameamuru uchunguzi wa haraka kufanyika ili kubaini chanzo cha kifo hicho.Kabuga alikuwa miongoni mwa watu waliotafutwa zaidi duniani kwa tuhuma za kuhusika katika kupanga na kuchochea mauaji ya takribani watu laki nane waliouawa kati ya Aprili na Juni 1994 nchini Rwanda.

    Alikamatwa nchini Ufaransa mwaka 2020 kabla ya kuhamishiwa The Hague, ambako alikabiliwa na mashtaka ya mauaji ya kimbari, njama za kutekeleza mauaji hayo pamoja na uhalifu dhidi ya ubinadamu.