Lebo: Iran

  • Vance: Mazungumzo ya Marekani na Iran Yapiga Hatua.

    Vance: Mazungumzo ya Marekani na Iran Yapiga Hatua.

    Makamu wa Rais wa Marekani, JD Vance, amesema mazungumzo kati ya Marekani na Iran yamepiga hatua kubwa, huku pande hizo mbili zikiendelea kujadiliana kuhusu baadhi ya vipengele vya lugha ya makubaliano na vifungu vya rasimu ya mkataba unaotarajiwa kufikiwa.

    Vance amesema bado ni vigumu kusema kwa uhakika ni lini au iwapo Rais Donald Trump atasaini hati ya makubaliano (MoU), akieleza kuwa bado kuna mjadala unaoendelea kuhusu baadhi ya vipengele vya maandishi ya makubaliano hayo. Hata hivyo, amesisitiza kuwa maendeleo yaliyofikiwa hadi sasa yanaashiria kuwa pande hizo zinakaribia kufikia hatua ya kuketi pamoja na kutatua masuala yaliyosalia.

    Kwa mujibu wa Vance, Iran inaonesha nia ya kufikia makubaliano na pia kutaka kufunguliwa kwa Mlango-Bahari wa Hormuz, jambo ambalo Marekani nayo inaliona kuwa la muhimu. Ameeleza kuwa mazungumzo kati ya pande hizo mbili yanaendelea kuhusu suala hilo, huku Washington ikiamini kuwa Tehran imekuwa ikijadiliana kwa nia njema, angalau kwa hatua ya sasa.

    Katika hatua nyingine, Vance amesema Iran imekubali kutotengeneza wala kutomiliki mpango wa nyuklia, na kwamba suala hilo litafuatiliwa na kuthibitishwa kadri muda unavyokwenda. Ameongeza kuwa hali ya sasa inaipa Marekani na washirika wake nafasi ya kuudhoofisha kwa kiasi kikubwa na kwa muda mrefu mpango wa nyuklia wa Iran.

    Licha ya ishara hizo za matumaini, Vance amesema bado kunahitajika maendeleo ya ziada ili kufikia mwafaka wa mwisho, lakini akaonyesha matumaini kuwa mazungumzo yataendelea kuzaa matunda katika siku zijazo.

  • Jeshi la Wanamaji la IRGC lasema meli 23 zimepita Mlango wa Hormuz ndani ya saa 24.

    Jeshi la Wanamaji la IRGC lasema meli 23 zimepita Mlango wa Hormuz ndani ya saa 24.

    Tehran – Jeshi la Wanamaji la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu wa Iran (IRGC) limetangaza kuwa jumla ya meli 23 za kibiashara, zikiwemo meli za mafuta na zile za kubeba makontena, zimepita salama katika Mlango wa Hormuz ndani ya kipindi cha saa 24 zilizopita.

    Kwa mujibu wa taarifa hiyo, meli zote zilivuka njia hiyo ya kimkakati baada ya kufanyika uratibu rasmi na mamlaka za wanamaji za IRGC.

    Katika taarifa iliyotolewa usiku wa Jumatano, IRGC ilisema inaendelea kusimamia kwa karibu njia hiyo ya baharini, ikieleza kuwa ina udhibiti wa kudumu, thabiti na wenye nguvu katika eneo hilo.

    Taarifa hiyo pia iliieleza Ghuba ya Uajemi kuwa ni eneo la bahari linalohusu mataifa ya kanda pekee. Aidha, IRGC ilidai kuwa hali ya sintofahamu ya kiusalama inayoshuhudiwa sasa katika eneo hilo inachangiwa na uwepo pamoja na shughuli za kijeshi za Marekani.

    Kwa mujibu wa taarifa hiyo, majeshi ya Marekani ndiyo chanzo kikuu cha kuyumbisha utulivu wa eneo hilo.

  • Iran Yashambulia Meli ya Mafuta ya Marekani Iliyozimwa Rada Hormuz.

    Iran Yashambulia Meli ya Mafuta ya Marekani Iliyozimwa Rada Hormuz.

    BANDAR ABBAS, IRAN — Chanzo cha kuaminika cha kijeshi kimeiambia Wakala wa Habari wa Tasnim kuwa, usiku wa kuamkia Alhamisi, meli moja ya mafuta ya Marekani ilijaribu kupita kwa siri katika Mlango wa Hormuz baada ya kuzima mifumo yake ya rada.

    Hata hivyo, kufuatia hatua ya haraka na madhubuti ya Kikosi cha Wanamaji cha Walinda Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (IRGC), ikiwemo kufyatua risasi za tahadhari kuelekea meli hiyo, chombo hicho kililazimika kusitisha safari yake na kurejea kilikotoka.

    Kwa mujibu wa taarifa hiyo, katika kujibu tukio hilo, jeshi la Marekani lilifyatua mashambulizi kuelekea eneo la ardhi tupu lililoko karibu na Bandar Abbas. Sauti za milipuko zilizosikika katika maeneo ya karibu zinaripotiwa kuhusishwa na tukio hilo.

    Taarifa za awali zinaeleza kuwa mashambulizi hayo hayakusababisha vifo, majeruhi wala uharibifu wa mali.

  • Ripoti: Akiba ya Makombora ya Marekani Yaporomoka, Urejeshaji Kuchukua Hadi Miaka Mitano.

    Ripoti: Akiba ya Makombora ya Marekani Yaporomoka, Urejeshaji Kuchukua Hadi Miaka Mitano.

    WASHINGTON — Uchambuzi mpya umeeleza kuwa Marekani huenda ikahitaji kati ya miaka mitatu hadi mitano kujenga upya akiba zake muhimu za makombora, baada ya kutumika kwa kiwango kikubwa katika vita vya Iran, hali inayozua wasiwasi kuhusu utayari wa nchi hiyo endapo kutazuka mzozo mwingine unaowezekana na China.

    Kwa mujibu wa ripoti hiyo, akiba ya makombora ya masafa marefu aina ya Tomahawk, makombora ya kujihami ya Patriot, pamoja na mifumo ya THAAD, imepungua kwa kiasi kikubwa. Ripoti inaongeza kuwa licha ya kuongezwa kwa matumizi ya sekta ya ulinzi chini ya uongozi wa Trump, kurejesha akiba hizo kutahitaji muda mrefu kutokana na udogo wa uwezo wa uzalishaji.

    Makadirio ya muda wa kurejesha akiba hiyo yanaonyesha kuwa:

    • Makombora ya Tomahawk huenda yakarejeshwa kikamilifu ifikapo mwaka 2030
    • Vizuizi vya THAAD vinatarajiwa kurejea kiwango cha kawaida mwishoni mwa mwaka 2029
    • Makombora ya Patriot yanakadiriwa kurejeshwa katikati ya mwaka 2029

    Ripoti hiyo imeibua mjadala mpya kuhusu uwezo wa Marekani wa kuhimili vita vya muda mrefu huku ikijiandaa kwa changamoto nyingine za kijeshi katika maeneo tofauti ya dunia.

  • Armenia nchi ya kwanza kununua Mtambo wa Ulinzi wa Iran “Majed” uliyopiga ndege za Marekani

    Armenia nchi ya kwanza kununua Mtambo wa Ulinzi wa Iran “Majed” uliyopiga ndege za Marekani

    TEHRAN/YEREVAN — Katika hatua inayoashiria mabadiliko makubwa ya kiusalama, taifa la Armenia inaripotiwa kusaini mkataba wa siri wa ununuzi wa silaha wenye thamani ya dola za Marekani milioni 500 na Iran. Kwa mujibu wa ripoti kutoka shirika la habari la Iran International, inayomilikiwa na Saudi Arabia mkataba huo unahusisha ununuzi wa mtambo wa kisasa wa ulinzi wa anga wa Majed, ulioundwa na kutengenezwa nchini Iran.

    Makubaliano haya yanatajwa kubeba uzito mkubwa, kwani yanagharimu takriban theluthi moja ya bajeti yote ya ulinzi ya Armenia kwa mwaka 2024, ambayo inasimama kwenye dola bilioni 1.4. Kwa upande mwingine, hatua hii inatoa fursa kwa Iran kurejesha na kuimarisha ushawishi wake wa kijeshi katika ukanda wa Caucasus Kusini.

    Wachambuzi wa masuala ya kiusalama wanaeleza kuwa uamuzi huu wa Armenia unachochewa na hofu inayoongezeka ya kiusalama kufuatia mivutano inayoendelea na jirani yake, Azerbaijan. Aidha, hatua hii inachukuliwa kama mbadala baada ya Armenia kuhisi kupungua kwa uungwaji mkono wa kijeshi kutoka kwa mshirika wake wa kihistoria, Urusi.

  • Iran: Hakuna Mazungumzo Mapya na Marekani Hadi Fedha Zilizozuiwa Zirejeshwe

    Iran: Hakuna Mazungumzo Mapya na Marekani Hadi Fedha Zilizozuiwa Zirejeshwe

    Shirika la Habari la Fars, likinukuu chanzo cha uhakika, limeripoti kuwa hakutakuwa na mazungumzo yoyote kati ya Iran na Marekani bila kufanyika kwa uhamishaji wa fedha za Iran zilizozuiwa. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, mzozo mkubwa wa hivi punde kati ya mataifa haya mawili kuelekea kuanza kwa mazungumzo, unahusu utaratibu wa kuiwezesha Iran kufikia mali zake hizo.

    Kwa mujibu wa chanzo hicho, suala la fedha za Iran zinazoshikiliwa linashughulikiwa kupitia juhudi za upatanishi zinazoongozwa na nchi ya Qatar. Imeelezwa pia kuwa hapo awali, Marekani ilikiuka ahadi zake kuhusiana na urejeshwaji wa mali hizo za Iran.

    Chanzo hicho kimeiambia Fars kuwa Iran imeshikilia msimamo wake thabiti, ikisisitiza kwamba maadamu fedha hizo zilizokubaliwa hazijahamishwa, hakuna makubaliano yoyote yanayoweza kufikiwa baina yao.

    Hata hivyo, mashauriano yanayoendelea nchini Qatar yameripotiwa kupiga hatua nzuri kuelekea kutatua kikwazo hicho.

    Licha ya hatua hiyo, chanzo hicho kimebainisha kuwa jopo la wapatanishi la Iran halichukulii maelewano hayo ya awali kama uamuzi wa mwisho, hasa kutokana na rekodi ya Marekani ya kukiuka makubaliano huko nyuma. Kimeongeza kuwa Iran imethibitisha kuwa iko tayari kwa hatua na chaguzi zote zinazoweza kujitokeza.