Lebo: Tanzania

  • Edhah Abdallah Avuna Faida Kubwa Baada ya Uwekezaji wa Mabilioni Sekta ya Saruji Kenya

    Edhah Abdallah Avuna Faida Kubwa Baada ya Uwekezaji wa Mabilioni Sekta ya Saruji Kenya

    Mfanyabiashara wa Tanzania, Edhah Abdallah, ameanza kupata faida kubwa kutokana na uwekezaji wake katika sekta ya saruji nchini Kenya kupitia Bamburi Cement na East African Portland Cement Company (EAPC).

    EAPC ilirekodi ongezeko kubwa la faida hadi Shilingi za Kenya bilioni 5.53 mwaka ulioishia Juni 2025, kutoka bilioni 1.16 mwaka uliotangulia, huku mapato yakiongezeka hadi bilioni 7.08. Bamburi Cement nayo ilitoka kwenye hasara ya Shilingi za Kenya milioni 905 hadi faida ya bilioni 3.08 mwaka ulioishia Desemba 2025.

    Mafanikio hayo yamechangiwa na kuongezeka kwa uzalishaji, mauzo, bei nzuri za bidhaa, kupungua kwa gharama za uendeshaji na kuimarika kwa mahitaji ya soko. Edhah alinunua Bamburi kwa Shilingi za Kenya bilioni 23.6 na pia anamiliki asilimia 68.7 ya EAPC kupitia Kalahari Cement.

    Kwa ujumla, uwekezaji wake unaonekana kuongezeka thamani kutokana na ukuaji wa faida na mali za kampuni hizo.

  • Askofu Bagonza: Hakuna dhehebu lenye uwezo wa kutuchagulia rais, Akanusha njama za 2030

    Askofu Bagonza: Hakuna dhehebu lenye uwezo wa kutuchagulia rais, Akanusha njama za 2030

    Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Karagwe Dkt. Benson Bagonza amesema Kanisa hilo halijawahi kukaa kikao chochote cha kupanga Rais ajae wala hakuna Dhehebu lenye uwezo wa kuchagua nani awe Rais.

    Askofu Dkt. Bagonza ametoa kauli hiyo wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Dayosisi maarufu ‘KAD DAY’ ambapo Mgeni rasmi alikuwa ni Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Uhusiano, Deus Sangu.

    “Kitengo chako cha mahusiano kinayahusisha Makanisa, Misikiti na makundi yote ya kiimani, sisi sote wa Makanisa tupo chini yako kwa ajili ya uratibishaji wa mahusiano na makundi haya ya imani ni muhimu kwa sababu ndani yake kuna Vyama vyote, Makabila yote, Rangi zote, Maskini na Matajiri.”

    “Sisi kama KKKT hatujawahi kukaa kikao chochote kupanga Rais ajaye, hatujawahi na hatuna mpango huo kwani tunaamini hakuna Dhehebu lolote Nchini lenye uwezo wa kutuchagulia Rais, nayasema haya ili kukemea njama ya kuchafua Kanisa letu kwamba tunapanga kuweka Rais mwaka 2030” Askofu Dkt.Bagonza.

  • Julius Malema Ahoji Kwanini Mnangagwa (rais wa Zimbabwe) Alinusurika Corona Ila Sio Magufuli

    Julius Malema Ahoji Kwanini Mnangagwa (rais wa Zimbabwe) Alinusurika Corona Ila Sio Magufuli

    JOHANNESBURG, 17 Mei 2026 — Kiongozi wa chama cha Economic Freedom Fighters (EFF), Julius Malema, amezua mjadala kufuatia kauli yake ya kuhoji namna janga la COVID‑19 lilivyodai maisha ya aliyekuwa Rais wa Tanzania, hayati John Magufuli, huku Rais wa Zimbabwe, Emmerson Mnangagwa, akiendelea kuishi.

    Akizungumza katika hafla ya kisiasa, Malema alimwelezea Magufuli kama “rais aliyekuwa mstari wa mbele katika utekelezaji wa majukumu yake,” na kudai kuwa aliondolewa na virusi vya corona.

    Katika maelezo yake, alihoji kwa nini janga hilo “halikumgusa” Mnangagwa, ambaye alimkosoa vikali kwa kumtaja kama kiongozi asiye na uwezo.

    Kauli hiyo imeibua mjadala katika mitandao ya kijamii na miongoni mwa wachambuzi wa siasa, huku baadhi wakiona ni maoni ya kisiasa yenye lengo la kukosoa uongozi wa Zimbabwe, na wengine wakisisitiza umuhimu wa kuheshimu kumbukumbu za viongozi waliotangulia mbele ya haki.

    Hadi sasa, hakujawa na majibu rasmi kutoka serikalini Zimbabwe kuhusu kauli hizo.

  • Heche: Lissu Aumwa Tumbo kwa Maumivu Makali Gerezani

    Heche: Lissu Aumwa Tumbo kwa Maumivu Makali Gerezani

    Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), John Heche, amesema amepokea taarifa kutoka kwa mdogo wa Mwenyekiti wa chama hicho, Tundu Lissu, kuwa Lissu anaumwa tumbo na anapata maumivu makali tangu jana.

    Heche alitoa kauli hiyo Mei 17, 2026 wakati akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika katika Viwanja vya Shule ya Msingi Nyankumbu, Kata ya Nyankumbu, Wilaya na Mkoa wa Geita.

    Amesema mdogo wa Lissu aitwaye Vicent alimpa taarifa kwa njia ya simu kuwa Lissu alianza kuumwa tumbo tangu jana jioni na anaendelea kupata maumivu makali, hali inayozua wasiwasi kwa viongozi na wanachama wa chama hicho.

    Heche ameongeza kuwa chama hicho kimesisitiza mara kadhaa kuwa endapo kiongozi wao atapata madhara akiwa gerezani, hali hiyo haitavumilika.

    “Tukiwa njiani kuja hapa nimepigiwa simu na mdogo wake Lissu aitwaye Vicent akiniambia kuwa tangu jana jioni Mwenyekiti wetu anaumwa sana tumbo. Tumbo linamkata na ana maumivu makali sana. Tumesema tena na tena, Lissu akipata shida haitaeleweka nchi hii,” amesema Heche.

  • Taharuki Bungeni Baada ya Kengele ya Dharura Kulia Ghafla

    Taharuki Bungeni Baada ya Kengele ya Dharura Kulia Ghafla

    Dodoma: Baadhi ya wabunge wamelazimika kutoka kwa tahadhari ndani ya ukumbi wa Bunge baada ya kengele ya dharura kulia ghafla, ikiashiria uwepo wa hatari au hitilafu ya kiusalama ndani ya jengo hilo.

    Tukio hilo limetokea wakati wabunge walipokuwa wakiendelea kuchangia Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Uchukuzi kwa mwaka wa fedha 2026/27, hali iliyosababisha shughuli za Bunge kusimama kwa takribani sekunde 30 kabla ya kuendelea tena.

    Kwa mujibu wa taratibu za usalama, kengele za dharura katika maeneo ya mikusanyiko kama Bunge hutumika kutoa tahadhari endapo mifumo ya usalama itabaini hali inayoweza kuhatarisha usalama wa watu waliopo ndani ya jengo.

    Kengele hizo zinaweza kuwashwa kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo moshi, moto, hitilafu ya umeme, tahadhari za kiusalama au changamoto za kiufundi katika mifumo ya usalama ya jengo.

  • Serikali ya Kenya Yashukuru Mapokezi ya Tanzania, Yaahidi Kuimarisha Ushirikiano wa Kikanda

    Serikali ya Kenya Yashukuru Mapokezi ya Tanzania, Yaahidi Kuimarisha Ushirikiano wa Kikanda

    Serikali ya Kenya imetoa shukrani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, pamoja na wananchi wa Tanzania kwa mapokezi ya kipekee na ukarimu waliouonyesha wakati wa Ziara ya Kihistoria ya Kitaifa iliyofanyika nchini humo.

    Kupitia taarifa rasmi, Serikali ya Kenya imesisitiza dhamira yake ya kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa makubaliano mbalimbali yaliyosainiwa wakati wa ziara hiyo, ambayo yanalenga kuimarisha maendeleo ya pamoja na kukuza ustawi wa mataifa hayo mawili.

    Serikali hiyo pia imeeleza kuwa itaendelea kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na ushirikiano wa pande mbili kati ya Kenya na Tanzania, sambamba na kuendeleza ushirikiano ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kwa lengo la kuongeza muunganiko wa kikanda na ustawi wa pamoja.

    Ziara hiyo ya Kitaifa ya siku mbili ilihitimishwa kwa hafla ya kuagana rasmi na Rais Samia Suluhu Hassan katika Ikulu ya Dodoma, baada ya majadiliano yenye mafanikio kati ya viongozi wa nchi hizo mbili.