Lebo: utaridi

  • Iran Yasisitiza Kuendeleza Diplomasia Licha ya Kutoiamini Marekani

    Iran Yasisitiza Kuendeleza Diplomasia Licha ya Kutoiamini Marekani

    Katika juhudi za kutafuta suluhu ya kidiplomasia, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, amefanya mazungumzo ya simu na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, yakilenga kutathmini hali ya usalama katika ukanda wa Mashariki ya Kati.

    Katika mazungumzo hayo ya Ijumaa, Waziri Araghchi amebainisha kuwa licha ya Iran kuwa na mashaka makubwa juu ya nia ya Marekani, nchi hiyo imechagua kushiriki kikamilifu katika mchakato wa mazungumzo unaopatanishwa na Pakistan.

    Araghchi ameitaja historia ya ahadi zilizovunjwa, usaliti wa kidiplomasia, na vitendo vya kijeshi vya Marekani kama vikwazo vikubwa vinavyochelewesha mafanikio ya mazungumzo hayo. Hata hivyo, amesisitiza kuwa Iran inaingia kwenye meza ya mazungumzo kwa uzito na uwajibikaji, ikilenga kufikia matokeo ya haki na ya kuridhisha kwa pande zote.

    Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, amelaani vikali matumizi ya nguvu dhidi ya mamlaka ya mataifa. Guterres amesisitiza umuhimu wa kuheshimu Mkataba wa Umoja wa Mataifa na kueleza kuwa njia pekee ya kupata amani na utulivu wa kudumu katika eneo la Ghuba na Bahari ya Oman ni kupitia mazungumzo ya kidiplomasia.

    Mazungumzo haya yanakuja wakati hali ya usalama katika ukanda huo ikiwa bado tete kufuatia mfululizo wa matukio ya kijeshi yaliyotokea tangu mwishoni mwa mwezi Februari mwaka huu, ikiwemo mashambulizi ya kijeshi yaliyosababishwa na uvamizi wa pamoja wa Marekani na Israel dhidi ya Iran.

    Ingawa usitishaji vita uliotangazwa mnamo Aprili 7, 2026, unaendelea kufuatiliwa kwa karibu, Pakistan na mataifa mengine ya kanda hiyo yanaendelea na jitihada za upatanishi ili kuhakikisha mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya Tehran na Washington yanazaa matunda.

  • Iran na Pakistan Zaungana Kuimarisha Usalama wa Chakula Kanda ya Ghuba.

    Iran na Pakistan Zaungana Kuimarisha Usalama wa Chakula Kanda ya Ghuba.

    Iran imetangaza nia yake ya kushirikiana kwa karibu na nchi jirani ya Pakistan ili kuhakikisha usalama endelevu wa chakula katika ukanda wa Ghuba ya Uajemi.

    Katika mazungumzo yaliyofanyika mjini Tehran kati ya Waziri wa Kilimo na Jihad wa Iran, Gholamreza Nouri Ghezeljeh, na Waziri wa Mambo ya Ndani wa Pakistan, Syed Mohsin Naqvi, pande zote mbili zimesisitiza kuwepo kwa uwezo mkubwa wa kibiashara na uzalishaji wa mazao ya kilimo na mifugo baina ya nchi hizo mbili.

    Waziri Ghezeljeh amesema kuwa uhusiano wa kihistoria na kitamaduni kati ya Tehran na Islamabad ni msingi imara wa ushirikiano wa kimkakati. Ameongeza kuwa nchi hizo zimeanza kuweka misingi madhubuti ya kuhakikisha upatikanaji wa bidhaa za msingi, hatua inayotajwa kuwa ni mhimili mkuu wa usalama wa chakula kwa mataifa hayo na kanda nzima.

    Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Pakistan, Syed Mohsin Naqvi, amekaribisha fursa hizo za ushirikiano. Hata hivyo, Naqvi amesisitiza kuwa amani na usalama ni vigezo muhimu vya lazima ili kuruhusu biashara na usalama wa chakula kustawi katika eneo hilo.

    Katika mkutano huo, mawaziri hao wamekubaliana kuharakisha utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa wakati wa ziara ya Rais Masoud Pezeshkian nchini Pakistan mwaka jana, hasa katika sekta ya kilimo na uboreshaji wa usafirishaji wa bidhaa muhimu za msingi.

    Ushirikiano huu unatazamwa kama hatua muhimu ya kuimarisha uchumi na utulivu katika kanda ya Mashariki ya Kati na Asia ya Kusini.

  • Athari Fiche za Vita: Uhitaji wa Huduma za Afya ya Akili yaongezeka kwa 240 % Israel

    Athari Fiche za Vita: Uhitaji wa Huduma za Afya ya Akili yaongezeka kwa 240 % Israel

    Jerusalem —

    Kwa mujibuwa gazeti la Jerusalem Post, Uhitaji wa huduma za afya ya akili nchini Israel umeongezeka kwa takriban asilimia 240 katika kipindi cha miaka miwili iliyopita. Hali hii inachochewa na vita vinavyoendelea na athari zake mbaya za muda mrefu kisaikolojia kwa wananchi, kwa mujibu wa shirika la huduma za afya la Clalit (Clalit Health Services).

    Shirika hilo, ambalo ni mtoa huduma mkubwa zaidi wa afya nchini humo linalohudumia zaidi ya nusu ya idadi ya watu wote, lilitangaza ongezeko hilo la kutisha siku ya Jumatatu wakati wa ziara ya Kamati ya Afya ya Bunge (Knesset) katika Hospitali ya Clalit-Beilinson. Ili kukabiliana na wimbi hilo kubwa la wagonjwa, Clalit imeajiri wataalamu wapya 290 wa afya ya akili na kupanua wigo wa kliniki 40 za afya ya akili nchi nzima.

    Takwimu hizi zinaangazia kile ambacho wataalamu wanakielezea kama “athari fiche za vita” — kiwewe cha kitaifa ambacho madhara yake yanavuka mbali zaidi ya majeraha ya kimwili. Tangu kuzuka kwa mzozo wa sasa, jamii ya Israel imekuwa ikikabiliwa na mawimbi ya mara kwa mara ya msongo wa mawazo kutokana na mashambulizi ya roketi, ukimbizi wa ndani, kupoteza maisha, na tishio la kiusalama la kudumu, mambo ambayo yamechangia ongezeko kubwa la matatizo ya wasiwasi (anxiety), sonona (depression), ugonjwa wa kiwewe baada ya tukio (PTSD), na mahitaji mengine ya kiakili.

  • Iran yadaiwa kuharibu ndege zisizo na rubani za Marekani zenye thamani ya mabilioni

    Iran yadaiwa kuharibu ndege zisizo na rubani za Marekani zenye thamani ya mabilioni

    TEHRAN – Ripoti mpya ya shirika la habari la Bloomberg imebainisha kuwa, tangu kuanza kwa mzozo wa sasa, Iran imefanikiwa kutungua zaidi ya ndege zisizo na rubani (drones) za Marekani aina ya MQ-9 Reaper, idadi ambayo ni zaidi ya 24.Hatua hiyo imesababisha pigo kubwa kwa jeshi la Marekani, huku ikikadiriwa kusababisha hasara ya kifedha inayokaribia dola bilioni 1. Takwimu hizo zinaonesha kuwa uharibifu huo umepunguza kwa takriban 20% uwezo wa jeshi la Marekani (Pentagon) katika kundi la ndege hizo walizokuwa nazo kabla ya kuanza kwa mzozo huu.Uchambuzi wa wataalamu wa kijeshi unaonesha kuwa kupotea kwa ndege hizi za kisasa za upelelezi na mashambulizi ni changamoto kubwa kwa mkakati wa anga wa Marekani katika ukanda huu.

  • Mvutano Bado Mkali: Iran Yasema Hakuna Dalili za Makubaliano ya Haraka na Marekani

    Mvutano Bado Mkali: Iran Yasema Hakuna Dalili za Makubaliano ya Haraka na Marekani

    TEHRAN, IRAN – Serikali ya Iran imeweka wazi kuwa hakuna dalili zozote za kufikia makubaliano ya haraka na Marekani, ikisisitiza kuwa tofauti kati ya mataifa hayo mawili ni kubwa, nyingi, na zenye mizizi mirefu ambayo haisuluhishiki kwa urahisi.

    Akitoa ufafanuzi huo, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Bw. Ismael Baqaei, amesema kuwa ni vigumu kutarajia suluhu ya haraka kupitia vikao vichache. “Hatuwezi kusema tumefikia hatua ambayo makubaliano yapo karibu. Hapana, hali haiko hivyo. Tofauti kati ya Iran na Marekani ni kubwa sana na hazisuluhishiki kwa urahisi.

    Hatuwezi kusema kwa uhakika kwamba baada ya ziara chache au mazungumzo ya wiki au miezi kadhaa, tutafikia muafaka,” alisema Bw. Baqaei.

    Akigusia suala la mpango wa nyuklia wa taifa hilo, Msemaji huyo alisisitiza kuwa Iran ni mwanachama halali wa Mkataba wa Kuzuia Usambazaji wa Silaha za Nyuklia (NPT) na hivyo ina haki ya msingi ya kurutubisha uraniamu. Aliongeza kuwa msimamo wa taifa hilo kuhusu akiba yake ya uraniamu iliyorutubishwa uko wazi na unajulikana.

    Hata hivyo, Bw. Baqaei alifafanua kuwa mazungumzo yanayoendelea kwa sasa hayaingii kwa undani kwenye masuala ya kiufundi ya nyuklia, kwani kufanya hivyo kunaweza kukwamisha juhudi za kupata suluhu.”Maelezo ya kina kuhusiana na suala la nyuklia hayajadiliwi katika hatua hii, na kwa hakika hatutafikia suluhu yoyote ikiwa tutajaribu kuchimba kwa kina kuhusu akiba yetu ya uraniamu iliyorutubishwa,” alihitimisha.

  • Umoja wa Ulaya Wapanua Wigo wa Vikwazo Dhidi ya Iran

    Umoja wa Ulaya Wapanua Wigo wa Vikwazo Dhidi ya Iran

    BRUSSELS/TEHRAN – Umoja wa Ulaya (EU) leo umetangaza uamuzi wa kupanua mfumo wake wa vikwazo dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

    Hatua hii imetajwa na upande wa Iran kama kitendo dhidi ya taifa hilo, ambacho kinapuuza haki yake ya kisheria ya kusimamia usalama wa usafiri wa majini katika Mlango wa Bahari wa Hormuz, ambao sehemu yake ipo ndani ya mamlaka ya maji ya Iran.

    Kwa mujibu wa taarifa hiyo, vikwazo hivi vipya vitawalenga watu binafsi na taasisi mbalimbali.

    WUmoja wa Ulaya unadai kuwa walengwa wa vikwazo hivi ni wale wanaohusika na vitendo vinavyolenga kutishia uhuru na usalama wa usafiri wa baharini katika ukanda wa Asia Magharibi, hususan katika eneo la kimkakati la Mlango wa Bahari wa Hormuz.