Mwandishi: Hussein Suleiman

  • 90 waaga dunia na wengine kadhaa kujeruhiwa kwenye mgodi China

    90 waaga dunia na wengine kadhaa kujeruhiwa kwenye mgodi China

    TAKRIBAN watu 90 walifariki kufuatia mlipuko katika mgodi wa makaa ya mawe [coal kwa Kimombo] kaskazini mwa China, kulingana na vyombo vya habari vya serikali ya nchi hiyo.

    Mlipuko huo wa gesi ulitokea katika Mgodi wa Makaa ya Mawe wa Liushenyu unaomilikiwa na kampuni ya Tongzhou Group katika Mkoa wa Shanxi.

    Mamia ya waokoaji walitumwa katika eneo hilo huku watu 27 wakiripotiwa kulazwa hospitalini wakipokea matibabu, mmoja akiwa katika hali mahututi.

    Operesheni za uokoaji bado zinaendelea.Mlipuko huo ulitokea usiku Ijumaa katika mgodi huo uliokuwa na wafanyakazi 247 waliokuwa kazini wakati wa ajali hiyo.

    Mmoja wa wachimbaji waliojeruhiwa, Wang Yong, aliambia televisheni ya serikali kuwa hakusikia mlio wowote wakati mlipuko ulipotokea bali aliona moshi mzito ukitanda ghafla.

    “Nilinusa harufu kama ile ya milipuko. Nikaanza kuwapigia watu kelele wakimbie.

    Tulipokuwa tunakimbia niliona watu wakianguka kutokana na moshi huo. Baadaye nami nikapoteza fahamu,” alisema.

    Aliongeza kuwa alikaa chini kwa karibu saa moja kabla ya kuzinduka na kumwamsha mwenzake waliyetoroka pamoja kutoka mgodini.Baada ya mkasa huo, Rais wa China Xi Jinping aliagiza juhudi zote zifanywe kuwahudumia majeruhi na kutafuta manusura. Pia aliitaka serikali kuchunguza chanzo cha ajali hiyo na kuwachukulia hatua waliohusika.Vyombo vya habari vya serikali vilisema maafisa wanaosimamia mgodi huo wamezuiliwa huku uchunguzi ukiendelea. Hata hivyo, chanzo rasmi cha mlipuko huo bado hakijatangazwa.

    Ripoti zinaonyesha viwango vya gesi ya kaboni, ambayo ni sumu kali isiyo na harufu, vilipatikana kuwa juu ya kiwango kinachoruhusiwa.

    Wizara ya Usimamizi wa Dharura ya China ilituma wafanyakazi 345 kutoka vikosi sita vya uokoaji kusaidia shughuli hizo.

    Mnamo mwaka 2024, mgodi wa Liushenyu ulitajwa na Mamlaka ya Kitaifa ya Usalama wa Migodi ya China kuwa miongoni mwa migodi yenye “hatari kubwa za usalama”.

    Kampuni ya Tongzhou Group pia ilipewa adhabu mbili za kiutawala mwaka 2025 kutokana na masuala ya usalama.

  • Iran yadaiwa kuharibu ndege zisizo na rubani za Marekani zenye thamani ya mabilioni

    Iran yadaiwa kuharibu ndege zisizo na rubani za Marekani zenye thamani ya mabilioni

    TEHRAN – Ripoti mpya ya shirika la habari la Bloomberg imebainisha kuwa, tangu kuanza kwa mzozo wa sasa, Iran imefanikiwa kutungua zaidi ya ndege zisizo na rubani (drones) za Marekani aina ya MQ-9 Reaper, idadi ambayo ni zaidi ya 24.Hatua hiyo imesababisha pigo kubwa kwa jeshi la Marekani, huku ikikadiriwa kusababisha hasara ya kifedha inayokaribia dola bilioni 1. Takwimu hizo zinaonesha kuwa uharibifu huo umepunguza kwa takriban 20% uwezo wa jeshi la Marekani (Pentagon) katika kundi la ndege hizo walizokuwa nazo kabla ya kuanza kwa mzozo huu.Uchambuzi wa wataalamu wa kijeshi unaonesha kuwa kupotea kwa ndege hizi za kisasa za upelelezi na mashambulizi ni changamoto kubwa kwa mkakati wa anga wa Marekani katika ukanda huu.

  • Waziri Mkuu wa Uhispania: Nitashinikiza ili Ulaya nzima imwekee vikwazo Waziri wa Usalama wa Israel.

    Waziri Mkuu wa Uhispania: Nitashinikiza ili Ulaya nzima imwekee vikwazo Waziri wa Usalama wa Israel.

    Waziri Mkuu wa Uhispania: Nitashinikiza ili Ulaya nzima imwekee vikwazo Waziri wa Usalama wa Israel.🔹 Picha za waziri wa Israel, Ben-Gvir, akiwadhalilisha wanachama wa msafara wa kimataifa wa kusaidia Gaza, hazikubaliki. Hatutaruhusu mtu yeyote kuwatendea vibaya raia wetu.

  • Israel yamkaribisha balozi wa kwanza wa Somaliland

    Israel yamkaribisha balozi wa kwanza wa Somaliland

    Israel imepokea rasmi balozi wa kwanza kabisa wa Somaliland, Mohamed Hagi, ikiwa ni hatua muhimu ya kidiplomasia huku pande zote zikiahidi kuimarisha ushirikiano katika biashara, usalama na mahusiano ya kikanda.Balozi wa kwanza wa Somaliland kwenda nchi ya kigeni amewasilisha hati zake za utambulisho kwa Rais wa Israel, Isaac Herzog, kufuatia utambuzi wa Israel wa uhuru wa eneo hilo lililojitenga mwaka jana.Somaliland ilitangaza kujitenga na Somalia mwaka 1991 lakini imeendelea kutotambuliwa kimataifa kwa zaidi ya miongo mitatu.

  • Mwanaharakati Fransis Awino amefungua kesi ili kupinga ongezeko la bei ya mafuta

    Mwanaharakati Fransis Awino amefungua kesi ili kupinga ongezeko la bei ya mafuta

    Mwanaharakati Francis Awino amefungua kesi katika Mahakama Kuu ya Nairobi kupinga ongezeko la hivi karibuni la bei ya mafuta lililotangazwa na Mamlaka ya Kudhibiti Nishati na Petroli (EPRA) tarehe 14 Mei 2026.Kesi hiyo, iliyowasilishwa chini ya Kitengo cha Katiba na Haki za Kibinadamu, inalenga kuhoji uhalali wa uamuzi huo, huku Awino akidai kuwa hatua hiyo imeweka mzigo mkubwa kwa wananchi na kukiuka haki za kikatiba kutokana na ukosefu wa uwazi pamoja na ushirikishwaji wa umma.Kwa mujibu wa nyaraka za mahakama, EPRA ilitangaza ongezeko la Sh16.65 kwa kila lita ya petroli na Sh46.29 kwa kila lita ya dizeli, hatua ambayo imeibua malalamiko kutoka kwa wadau mbalimbali wa uchumi.Awino anasisitiza kuwa ongezeko hilo limeathiri kwa kiasi kikubwa sekta mbalimbali, ikiwemo usafirishaji, kilimo, biashara ndogo ndogo, pamoja na kaya zinazotegemea bidhaa zinazotokana na mafuta.Aidha, mwanaharakati huyo ameibua wasiwasi kuhusu matumizi ya zaidi ya Sh5 bilioni kutoka mfuko wa Petroleum Development Levy Fund, akitaka serikali kutoa maelezo ya kina kuhusu namna fedha hizo zilivyotumika katika kupunguza bei ya dizeli na mafuta ya taa.Katika hoja nyingine, Awino amepinga uamuzi wa serikali kuruhusu kwa muda matumizi ya mafuta yenye kiwango cha juu cha salfa, akionya kuwa hatua hiyo inaweza kuhatarisha afya ya wananchi pamoja na mazingira.Pia amehoji utekelezaji wa tangazo la serikali la kupunguza ushuru wa VAT kwa bidhaa za petroli hadi asilimia nane mwezi Aprili mwaka huu, akidai kuwa wananchi hawajaona manufaa yoyote kutokana na hatua hiyo.Kupitia ombi la dharura lililowasilishwa katika Mahakama Kuu ya Milimani, Awino anaitaka mahakama kuingilia kati na kusitisha mara moja utekelezaji wa ongezeko hilo, akionya kuwa hali ya sasa inaweza kusababisha maandamano na taharuki nchini.Kesi hiyo inawasilishwa wakati ambapo maandamano yanatarajiwa kufanyika kesho kupinga kupanda kwa bei ya mafuta nchini Kenya.

  • James Orengo: Niko tayari kukabiliana na Ruto katika uchaguzi wa mwaka 2027

    James Orengo: Niko tayari kukabiliana na Ruto katika uchaguzi wa mwaka 2027

    Gavana wa Siaya, James Orengo, ametangaza nia ya kugombea urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2027, hatua inayotafsiriwa na wachambuzi kama mwanzo wa mapambano makali dhidi ya Rais William Ruto.Tangazo hilo linafuatia mashauriano ya kisiasa yaliyodumu kwa wiki kadhaa katika maeneo mbalimbali, ikiwemo Nairobi, Magharibi mwa Kenya na Nyanza, ambako wafuasi wake wamekuwa wakimsukuma kuingia katika siasa za kitaifa. Kilichoanza kama mikutano ya kawaida ya ODM sasa kimebadilika na kuwa kampeni ya wazi ya kumtambulisha kama kiongozi wa upinzani.Orengo anashirikiana kwa karibu na kundi la “Linda Mwananchi” pamoja na viongozi kama Edwin Sifuna na Babu Owino, akisisitiza kuwa ODM ina hazina ya viongozi wanaoweza kuwania urais. Hata hivyo, wachambuzi wanaona hatua yake pia inalenga kujiimarisha kama kiongozi wa kisiasa wa jamii ya Waluo na kujiweka tayari kwa miungano ya kisiasa ya baadaye.Akiwahutubia wananchi katika maeneo ya Muhoroni na Nyakach, Orengo alisisitiza umuhimu wa jamii ya Waluo kuwa na mgombea urais ili kuongeza nguvu ya mazungumzo ya kisiasa kitaifa. Alijitaja kama mrithi wa kisiasa wa Jaramogi Oginga Odinga na akasema yuko tayari kumpa changamoto Rais Ruto.Aidha, alikosoa serikali kwa kupanda kwa gharama ya maisha na matatizo ya kiuchumi, akitaja kufungwa kwa viwanda vya sukari, hali mbaya ya miundombinu na migogoro ya mara kwa mara katika eneo la Sondu. Pia alizungumzia kusuasua kwa mradi wa bwawa la Koru-Soin, hali inayosababisha mafuriko ya kila mwaka Nyakach.Orengo alisisitiza kuwa iwapo atachaguliwa, atarejesha viwanda vya sukari chini ya umiliki wa umma. Pia aliwataka viongozi wanaotaka kuchaguliwa tena kuungana naye au wakabiliwe na hatari ya kushindwa uchaguzi wa 2027.Hata hivyo, bado hajaweka wazi iwapo atagombea kupitia ODM au chama kingine, licha ya kusisitiza kuwa yeye ni kiongozi ndani ya chama hicho. Tangazo lake linajiri wakati mjadala kuhusu uongozi na mgombea wa urais ndani ya ODM ukiendelea.Iwapo atawasilisha rasmi azma yake, hii itakuwa mara ya pili kwa Orengo kuwania urais tangu jaribio lake la mwaka 2002 kupitia chama cha SDP.