Mwandishi: Hussein Suleiman

  • Sayid Mojtaba Khamenei: Vituo vya Marekani katika eneo ni lazima vifungwe

    Sayid Mojtaba Khamenei: Vituo vya Marekani katika eneo ni lazima vifungwe

    Tuna nchi kumi na tano jirani, miongoni mwao zipo kwenye nchi kavu na zengine baharini, na tumekuwa tayari kila wakati kuanzisha uhusiano mzuri pamoja na kila nchi, lakini baadhi ya nchi hizi zimewekewa misingi yenye kulenga udhibiti katika eneo … napendekeza kwamba misingi hii ifungwe haraka iwezekanavyo.

    ✍🏼 Sehemu ya ujumbe wa kwanza wa Ayatullah Seyyed Mojtaba Hosseini Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu.

  • Iran YAKATAA MABAVU ya Trump, Hatujafikia mapatano yoyote na Marekani

    Iran YAKATAA MABAVU ya Trump, Hatujafikia mapatano yoyote na Marekani

    Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema Ijumaa kwamba mabadilishano ya ujumbe kati ya Iran na yanaendelea, lakini hadi sasa hakuna mwafaka wa mwisho uliofikiwa huku akisisitiza kuwa Tehran haikubali lugha ya mabavu.

    Esmaeil Baghaei amesema katika mahojiano na televisheni ya taifa ya Iran kwamba: “Tuliagana na lugha ya mabavu miaka 47 iliyopita.” Ameongeza kusema: “Hakuna dola lolote la Magharibi linaloweza kutumia lugha ya ‘kulazimisha’ katika mazungumzo na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Tunafanya maamuzi yetu wenyewe kwa kuzingatia maslahi na haki za taifa la Iran.”

    Kauli zake zilikuja saa chache baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kudai kwenye mtandao wa kijamii wa Truth Social kwamba lazima usimamizi wa Iran katika Mlango wa Hormuz uondolewa. Pia alidai kwamba uamuzi kuhusu makubaliano na Iran utachukuliwa hivi karibuni.

    Iran ilifunga Mlango wa Hormuz kwa maadui zake na washirika wao baada ya kuanza vita vya kichokozi vya Marekani na Israel dhidi yake tarehe 28 Februari na kuendelea kwa siku 40. Mamlaka za Iran zilianza kutekeleza udhibiti mkali zaidi mwezi uliopita kufuatia tangazo la Trump kuhusu kutekelezwa mzingiro uliolenga meli na bandari za Iran.

    Iran imesema hatua hizo za Trump zinakiuka masharti ya usitishaji mapigano na kwamba baadaye ziliongezwa kwa upande mmoja na Washington.

    Mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya Iran na Marekani, yanayosimamiwa na Pakistan na kuratibiwa na Qatar, yanaendelea kwa msingi wa pendekezo la vipengele 14 la Jamhuri ya Kiislamu. Lengo lake ni kufikiwa kwa hati ya makubaliano ya kumaliza vita vya Marekani na Israel dhidi ya Iran, kusitishwa uhasama wa Marekani baharini, na  kuachiliwa kwa mali za Iran zilizozuiwa.

    Baghaei amesisitiza kwamba Mlango wa Hormuz uko ndani ya maji ya kieneo ya Iran na Oman na hivyo ni nchi hizo mbili jirani zitakzoamua kuhusu usimamizi wa eneo hilo.

  • Kauli ya Marekani Baada ya Kenya Kusitisha Ujenzi wa Kituo cha Ebola nchini humo

    Kauli ya Marekani Baada ya Kenya Kusitisha Ujenzi wa Kituo cha Ebola nchini humo

    Mahakama Kuu ya Kenya imesitisha kwa muda kuanzishwa kituo cha karantini kwa wagonjwa wa Ebola raia wa Marekani, kilichotarajiwa kujengwa nchini humo. Kufuatia uamuzi huo, wakuu wa Marekani wamedai kuwa  watashughulikia hofu ya Wakenya kuhusiana na kituo hicho.

    Taarifa ya Jumamosi kutoka Ofisi ya Jeremy P. Lewin, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani anayeshughulikia Misaada wa Kigeni, imesema: “Tumejulishwa kuhusu hatua ya mahakama nchini Kenya dhidi ya kituo cha kutenga wagonjwa wa Ebola. Tunawasiliana na mamlaka za Kenya na tuna matumaini kuwa tunaweza kutatua pingamizi hiyo.”

    Taarifa hiyo ni majibu ya kwanza ya hadharani kutoka Washington tangu Mahakama Kuu ya Kenya isimamishe mpango wa kuanzisha au kuanza kufanya kazi kituo hicho, hadi pale shauri la kikatiba litakaposikilizwa na kuamuliwa.

    Jaji Patricia Nyaundi alitoa maagizo hayo Ijumaa baada ya kundi la kutetea haki kupinga mradi huo, likisema kuwa unazua masuala ya kikatiba na ya maslahi ya umma yanayohitaji mapitio ya kimahakama.

    Kituo hicho kilichopendekezwa kimeibua mjadala mkali nchini Kenya, kufuatia taarifa kwamba kitatumika kuwashguhulikia raia wa Marekani wanaoweza kuwa wameathiriwa na Ebola wakati wa mlipuko unaoendelea katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Kauli ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, kuwa Marekani haitawaruhusu kuingia nchini humo waathirika au washukiwa wa ugonjwa wa Ebola na kwamba watatibiwa katika nchi nyingine imewakasirisha sana Wakenya wanaoona kwamba nchi yao inatumiwa kama jaa la taka na Marekani.

    Wizara ya Afya ya Kenya imeutetea mpango wa kujenga kituo hicho na kusema ni sehemu ya ushirikiano wa kimataifa kuhusu kukabiliana na magonjwa kwa kuzingatia kanuni zote la afya.

    Muungano wa Madaktari Kenya (KMPDU) umeitaka serikali iwe na uwazi kamili kuhusu makubaliano yoyote yanayohusiana na kituo hicho kilichopendekezwa, ukisema masuala ya afya ya umma na usalama yanapaswa kujadiliwa wazi kabla ya mpango wowote kama huo kusonga mbele.

  • Muungano wa Madaktari Kenya waipa serikali masaa 48, Hatutaki Ebola Kenya

    Muungano wa Madaktari Kenya waipa serikali masaa 48, Hatutaki Ebola Kenya

    Muungano wa Madaktari, Wafamasia na Madaktari wa Meno nchini Kenya (KMPDU) umepatia serikali muda wa saa 48 kueleza hadharani masharti kamili ya makubaliano yake na Marekani au ikabiliwe na mgomo wa kitaifa wa madaktari.

    Ni baada ya kutangazwa kwamba, wataalamu wa magonjwa ya kuambukiza kutoka Marekani wamewasili nchini Kenya na tayari wanaendelea na maandalizi ya kituo maalumu cha Ebola ambacho Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani, Marco Rubio, amesema kitaanza kufanya kazi ndani ya siku saba zijazo.

    Kwa mujibu wa vyanzo, kituo hicho kinajengwa karibu na maeneo ya kijeshi ya Uingereza katika Kaunti ya Laikipia.

    Lengo lake limetajwa kuwa ni kwa ajili ya kuwatenga raia wa Marekani walioathiriwa au waliokaribiana na virusi vya Ebola.

    Katibu Mkuu wa KMPDU, Dkt Davji Bhimji Atellah, amesema kituo hicho kinaanzishwa katika Kituo cha Anga cha Laikipia.

    “Kenya ni taifa huru, si eneo la kutengwa wagonjwa wa magonjwa hatari kwa maslahi ya kisiasa,” amesema Dkt Atellah.

    “Hatutakubali Kenya kutumiwa kama mahali pa kuhifadhi wagonjwa wa virusi hatari ambavyo havikutoka nchi yetu.”

    Muungano huo umeitaka serikali kueleza kwa nini Kenya imechaguliwa kupokea raia wa Marekani walio na Ebola ilhali mataifa jirani na maeneo yaliyoathirika zaidi hayajapewa jukumu hilo.

    “Ikiwa Amerika inaamini safari ya saa 12 ya kuwarudisha raia wake Washington ni hatari sana, kwa mantiki gani ni salama kuwaleta Kenya?” alihoji Dkt Atellah.

    Muungano huo pia umesema hautakubali mfumo wa afya wa kibaguzi nchini Kenya.KMPDU imesema haitakubali madaktari wa Kenya kutumiwa kama wafanyakazi wa bei rahisi katika mazingira hatari bila mishahara bora, marupurupu ya kazi hatari na bima kamili ya afya.

    Wakati huo huo, Wizara ya Afya kupitia Katibu katika Idara ya Afya ya Umma Mary Muthoni ilisema Kenya ina uhuru wa kushirikiana na mataifa mengine katika kupambana na Ebola iliyosababisha zaidi ya vifo 100 nchini DRC.

  • Mgogoro wa kisiasa Senegal , Rais amchagua Aminou Lo kama Waziri Mkuu

    Mgogoro wa kisiasa Senegal , Rais amchagua Aminou Lo kama Waziri Mkuu

    Mgogoro wa kisiasa wa Senegal umeshika kasi huku Rais wa nchi hiyo Bassirou Diomaye Faye akimteua mchumi Ahmadou Al Aminou Lo katika nafasi ya Waziri Mkuu akichukua nafasi ya Ousmane Sonko aliyefutwa kazi.

    Kuteuliwa Ahmadou Al Aminou Lo katika cheo cha Waziri Mkuu kumeshadidisha mpasuko wakati huu ambapo Bunge la Senegal limepanga kupiga kura kwa ajili ya kumrejesha Sonko katika nafasi ya ubunge.

    Rais Bassirou Diomaye Faye wa Senegal amemteua Mchumi wa Ngazi ya juu na mfanyakazi wa zamani wa benki Kuu ya nchi hiyo Ahmadou Al Amodou Lo kuwa Waziri Mkuu ikiwa zimepita siku kadhaa baada ya kumfuta kazi mshauri wake wa zamani Ousmane Sonko na kuivunja serikali.

    Lo, anayesifiwa kwa utaalamu wake katika mifumo ya kifedha; anachukua madaraka huku Senegal ikiwa imelemewa na mzigo wa deni unaofikia asilimia 132 ya Pato la Taifa na huku IMF ikiwa imesimamisha msaada wa dola bilioni 1.8 kwa nchi hiyo.

    Weledi wa masuala ya kisiasa wanasema kuwa kufukuzwa Sonko katika cheo cha Waaziri Mkuu shakhsia maarufu sana na aliyekuwa na mchango mkubwa katika kuingia mamlakani Rais Faye kunaashiria kupamba moto mvutano wa miezi kadhaa kati ya pande mbili hizo.

    Bunge la Senegal leo Jumanne lilipanga kupiga kuhusu kurejeshwa Ousmane Sonko katika nafasi ya Naibu na kumchagua Spika Mpya kufuatia kujiuzulu mshirika wake El Malick Ndiaye.

  • Iran Yatangaza Mfumo Mpya wa Malipo Kwa Meli Zinazopita Katika Mlango-Bahari wa Hormuz

    Iran Yatangaza Mfumo Mpya wa Malipo Kwa Meli Zinazopita Katika Mlango-Bahari wa Hormuz

    TEHRAN, IRAN– Serikali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetoa ufafanuzi rasmi kuhusiana na usimamizi wa njia za maji katika eneo la Ghuba, ikisema kuwa haina mpango wa kutoza “ushuru wa kupita” (tolls) kwa meli za kimataifa zinazotumia Mlango-bahari wa Hormuz.

    Badala yake, Tehran imetangaza mpango wa kuanzisha mfumo wa malipo kwa ajili ya “huduma za baharini” na hatua za “uhifadhi wa mazingira” katika Ghuba ya Uajemi na Ghuba ya Oman.

    Muktadha wa Sheria na HudumaKulingana na vyanzo vya habari nchini Iran, ikiwemo shirika la habari la serikali (IRNA), hatua hii inalenga kuimarisha usalama wa baharini na kutoa fidia kwa gharama ambazo Iran inaingia katika kulinda mfumo wa ikolojia wa bahari hiyo.

    Chini ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Sheria ya Bahari (UNCLOS), mataifa hayawezi kutoza ushuru kwa meli zinazopita katika milango-bahari ya kimataifa kwa ajili ya usafiri wa transit, lakini yanaweza kutoza gharama kwa huduma maalum zinazotolewa.

    Viongozi wa mamlaka ya bandari na baharini nchini Iran wamesisitiza kuwa:

    1. Huduma za Kiufundi:Gharama hizo zitahusisha huduma za uongozi wa meli (pilotage), uokoaji, na usalama wa mawasiliano.

    2. Ulinzi wa Mazingira:Kutokana na msongamano mkubwa wa meli za mafuta, Iran inadai kuwa na jukumu kubwa la kusafisha uchafuzi na kuzuia uharibifu wa mazingira, jambo ambalo sasa litagharamiwa na watumiaji wa njia hizo.

    Mlango-bahari wa Hormuz ni moja kati ya njia muhimu zaidi za nishati duniani, ambapo takriban asilimia 20 ya mafuta yote yanayotumiwa duniani hupita hapo. Wachambuzi wa masuala ya kijiopolitika wanaona hatua hii kama mbinu ya Iran kuimarisha udhibiti wake katika eneo hilo huku ikifuata misingi ya kisheria ya kimataifa ili kuepuka migogoro ya moja kwa moja na mataifa ya magharibi na mashirika ya usafirishaji.

    Hadi sasa, mataifa makubwa na mashirika ya usafirishaji wa baharini bado yanatathmini jinsi gharama hizi mpya zitakavyoathiri bei ya usafirishaji na usalama wa safari katika eneo hilo lenye mvutano wa kisiasa.