Lebo: Iran

  • India Yaonya Marekani Dhidi ya Mashambulizi ya Meli za Kibiashara

    India Yaonya Marekani Dhidi ya Mashambulizi ya Meli za Kibiashara

    NEW DELHI, INDIA– Wizara ya Mambo ya Nje ya India imewasilisha malalamiko rasmi kwa mwanadiplomasia wa Marekani, ikielezea kutoridhishwa kwake na vitendo vya majeshi ya wanamaji ya Marekani dhidi ya meli za kibiashara.

    Onyo hilo limekuja baada ya jeshi la Marekani kushambulia meli mbili za India na kuuwa mabaharia watatu wananchi wa India.

    Katika tamko hilo kali, Serikali ya India imesisitiza kuwa shambulizi lolote dhidi ya meli za kibiashara ni jambo lisilokubalika na haliwezi kuvumiliwa. India imeeleza kuwa hatua hizo za kijeshi zinaashiria tishio la moja kwa moja kwa usalama na utulivu wa biashara ya kimataifa ya baharini.

    Wizara hiyo imebainisha kuwa matendo hayo yanakuja katika kipindi ambacho dunia inapitia wakati mgumu na katika eneo ambalo ni muhimu kiuchumi na kimkakati kwa usafirishaji wa bidhaa duniani.

    India imetaka hatua za haraka zichukuliwe ili kulinda usalama wa njia za bahari na kuepuka kuzorota zaidi kwa hali ya usalama wa kimataifa, ikisisitiza kuwa utulivu wa bahari ni nguzo muhimu kwa ustawi wa uchumi wa mataifa mengi duniani.

  • UKWELI KUHUSU MAZUNGUMZO: Iran Yakanusha Uvumi wa Makubaliano ya Haraka, Yasisitiza Maslahi ya Taifa

    UKWELI KUHUSU MAZUNGUMZO: Iran Yakanusha Uvumi wa Makubaliano ya Haraka, Yasisitiza Maslahi ya Taifa

    Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema kuwa sehemu muhimu za maelewano yanyolenga kumaliza vita vilivyolazimishwa zinakaribia kukamilika, pamoja na kuwepo misimamo kinzani ya Washington na vitendo vya mara kwa mara vya uchokozi wa kijeshi vinavyolenga kuvuruga mchakato wa kidiplomasia.

    Katika mahojiano jioni ya Alhamisi, Esmaeil Baghaei amekanusha uvumi wa vyombo vya habari kuhusu kufikiwa kwa makubaliano na akasisitiza tena msimamo thabiti na wa kimsingi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

    Baghaei amesema, “Kwa upande wa maandishi, rasimu ya makubaliano imekaribia kukamilika katika sehemu zake kuu. Tatizo ni kwamba misimamo kinzani ya Marekani imekuwa mara kwa mara chanzo cha misukosuko na kuvuruga mchakato huu.”

    Amesisitiza kuwa Jamhuri ya Kiislamu iliingia katika mchakato wa kidiplomasia kwa nia njema na kwa uwajibikaji kamili, huku maafisa wa Marekani wakibadili mara kwa mara misimamo yao, wakitoa madai mapya yasiyo ya uhalisia, na hata kufanya mashambulizi ya kijeshi wakati mazungumzo yakiendelea.

    Baghaei amebainisha kuwa tangu tangazo la usitishaji mapigano mwezi Aprili, Marekani na utawala wa Israel wamekiuka mara kadhaa makubaliano hayo ya kusitisha vita.

    Katika mashambulizi ya hivi karibuni, vikosi vya Marekani vililenga miundombinu ya kusini mwa Iran na kushambulia mabwawa mawili ya maji katika eneo la Sirik, kitendo ambacho ni jinai ya kivita.

    Amesisitiza wazi kwamba Iran imeonyesha, katika diplomasia na pia katika uwanja wa mapambano, kwamba haitakubali kamwe masharti na matakwa ya upande wa pili.

    Baghaei amesisitiza kuwa: “Iran imeonyesha kwa vitendo kwamba mistari yake myekundu ni maslahi na ustawi wa taifa la Iran, na hakutakuwa na maafikiano yoyote yanayokiuka hilo.”

    Ameongeza kuwa: “Lau Jamhuri ya Kiislamu ingekuwa na nia ya kurudi nyuma kutoka katika misimamo yake ya kimsingi chini ya shinikizo na vitisho, ingefanya hivyo mwaka mmoja na nusu uliopita. Tumeonyesha kwamba tunasimama imara.”

  • Trump ageuka tena: asitisha mashambulizi dhidi ya Iran kwa madai ya kufikia makubaliano ya juu

    Katika hali ya kushangaza na inayoashiria kubadilika kwa upepo wa kisiasa, Rais wa Marekani ametangaza kusitisha mpango wa mashambulizi ya kijeshi uliokuwa umepangwa dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran usiku wa leo. Trump kwa mara nyengine amedai kuwa uamuzi huo umekuja baada ya mazungumzo ya kidiplomasia kufikia ngazi ya juu kabisa ya uongozi nchini Iran.

    Akizungumza kuhusu hatua hiyo, Rais Trump amebainisha kuwa ametoa amri ya kufuta mashambulizi na ulipuaji wa mabomu uliopangwa kufanyika usiku wa leo. Kwa mujibu wa kiongozi huyo, hatua hiyo inafuatia kile alichokiita “uthibitisho wa makubaliano” kutoka kwa viongozi wakuu wa Tehran.

    Inadaiwa kuwa maelezo ya kina ya makubaliano hayo yamejadiliwa na kupitishwa na pande zote zinazohusika. Trump ameorodhesha mataifa kadhaa yaliyohusika katika mchakato huo, ikiwemo Israel, Saudi Arabia, Falme za Kiarabu (UAE), Qatar, Uturuki, Pakistan, Bahrain, Kuwait, Jordan, na Misri.

    Hata hivyo, Rais huyo amesisitiza kuwa mzingiro wa kijeshi baharini (naval blockade) utaendelea kudumishwa kama shinikizo hadi hapo makubaliano hayo yatakapokamilika rasmi. Amesema kuwa muda na mahali pa utiaji saini wa mkataba huo vitatangazwa hivi karibuni.

    Licha ya madai hayo mazito ya Trump, viongozi wa Iran mpaka sasa wamekaa kimya na hawajatoa tamko lolote rasmi. Wachambuzi wa mambo wanaangazia kwa mashaka kauli hizi, wakikumbusha kuwa tangu kuanza kwa mzozo huu, Trump amekuwa akitoa mfululizo wa kauli zinazopingana na ambazo mara nyingi zimeonekana kutoendana na uhalisia wa mambo nyanjani.

  • Mabaharia watatu wa India wauawa katika shambulio la Marekani karibu na Oman

    Mabaharia watatu wa India wauawa katika shambulio la Marekani karibu na Oman

    Waziri wa Meli wa New Delhi, Sarbananda Sonowal, ametangaza kwamba mabaharia watatu wa India wameuawa baada ya shambulio la Marekani kwenye meli ya Settebello yenye bendera ya Palau, akielezea tukio hilo kuwa la “kusikitisha”.

    Katika chapisho kwenye mtandao wa X, amesema kwamba vifo vyao ni “pigo kubwa”.

    Meli ya Settebello yenye bendera ya Palau ilishambuliwa Jumatano baada ya jeshi la Marekani kuishutumu kwa kukiuka kizuizi cha Marekani kwa “kujaribu kusafirisha mafuta kutoka Iran”. Kulikuwa na wafanyakazi 24 wa India ndani ya meli hiyo – 21 waliokolewa.

    Kamandi Kuu ya Marekani ilisema ilifyatua risasi kwenye chumba cha injini cha meli hiyo baada ya wafanyakazi “kushindwa mara kadhaa kufuata” masharti ya vikosi vya Marekani.

    Manoj Yadav, katibu mkuu wa Muungano wa Mabaharia nchini India, aliliambia gazeti la The Economic Times kwamba “haamini” kuwa Marekani haikuwa na taarifa kuhusu uraia wa watu waliokuwa ndani ya meli hizo. Alisema kuwa kuzuia meli hizo badala yake ni “njia mbadala iliyofaa”.

    Hii ni meli ya pili yenye wafanyakazi wa India ambayo imeshambuliwa wiki hii. Siku ya Jumatatu, vikosi vya Marekani viliishambulia Marivex, ambayo pia ni meli ya mafuta yenye bendera ya Palau yenye wafanyakazi wa India, katika Ghuba ya Oman baada ya kushindwa kufuata maagizo ya Marekani, Centcom ilisema.

    Wafanyakazi wote 24 waliokolewa na jeshi la Oman, mamlaka ya India ilisema.

  • Iran Yajibu Mapigo kwa Kushambulia Kikosi cha Tano cha Wanamaji cha Marekani Bahrain kwa Droni

    Iran Yajibu Mapigo kwa Kushambulia Kikosi cha Tano cha Wanamaji cha Marekani Bahrain kwa Droni

    Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu la Iran (IRGC) limetoa taarifa likisema kuwa mapema alfajiri ya leo Marekani ilifanya mashambulizi katika baadhi ya maeneo ya kusini mwa Iran, ikiwemo Jask, Sirik na kisiwa cha Qeshm. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, shambulio hilo lilisababisha uharibifu wa mnara mmoja wa mawasiliano katika mji wa Sirik na kuharibu matangi mawili ya maji katika eneo la Bamani.

    Taarifa hiyo inaeleza kuwa, kujibu mashambulizi hayo, kikosi cha wanamaji cha IRGC kilifanya shambulio la droni saa 2:30 alfajiri dhidi ya makao ya Kikosi cha Tano cha Wanamaji cha Marekani kilichoko Bahrain.

    IRGC imesema mapigano bado yanaendelea na kwamba vikosi vyake vinaendelea kujibu kile walichokiita uvamizi wa adui. Aidha, imeonya kuwa ikiwa mashambulizi yataendelea, Iran itatoa majibu makali zaidi.

  • Netanyahu: Israel Huenda Ikakabiliana na Iran Bila Msaada wa Marekani

    Netanyahu: Israel Huenda Ikakabiliana na Iran Bila Msaada wa Marekani

    Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, amesema huenda nchi yake ikalazimika kukabiliana na Iran bila msaada wa Marekani iwapo hali italazimu, hata kama hatua hiyo itasababisha vikwazo vya silaha na kuongezeka kwa shinikizo la kimataifa.

    Akizungumza katika kikao cha baraza la mawaziri jana usiku, Netanyahu alieleza kuwa Israel inapendelea kuepuka hali ya kujitenga kimataifa, lakini iko tayari kuchukua hatua kwa kujitegemea endapo maslahi yake ya usalama yatakuwa hatarini.

    Kwa upande wake, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya Israel (IDF), Eyal Zamir, alitoa msimamo mkali zaidi kuhusu makubaliano yanayopendekezwa ya nyuklia. Alisema kuwa kwa kuzingatia masharti ya sasa yanayojadiliwa, karibu makubaliano yoyote kati ya yale yanayozingatiwa hayataifaa Israel kwa mtazamo wa kiusalama.

    Kauli hizo zinakuja wakati juhudi za kidiplomasia kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran zikiendelea, huku mvutano wa kikanda ukiendelea kuongezeka.