Lebo: Iran

  • Baada ya onyo la Iran, Macron akana mpango wa kupeleka meli za kivita Hormuz

    Baada ya onyo la Iran, Macron akana mpango wa kupeleka meli za kivita Hormuz

    Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amesema kuwa nchi yake haikuwahi kupanga kupeleka vikosi vya majini katika Mlango wa Hormuz.

    Badala yake, amesema Ufaransa ilikuwa inapendekeza ujumbe wa usalama wa kidiplomasia ambao ungefanyika kwa uratibu na Iran.Akizungumza kuhusu hali ya usalama katika eneo hilo, Macron alisisitiza kuwa operesheni za kijeshi za kutumia nguvu kufungua tena mlango huo wa bahari si jambo linalowezekana na zinaweza kuongeza hatari wakati mvutano wa kikanda ukiendelea.

    Kwa mujibu wa rais huyo, hatua ya kwanza inapaswa kuwa kusitishwa kwa mapigano, kisha kufanyika mazungumzo ya kimataifa yanayohusisha Iran ili kuhakikisha usafiri wa baharini unakuwa salama.

    Mlango wa Hormuz umeathiriwa sana tangu mwishoni mwa Februari 2026 kufuatia mashambulizi na vitisho vinavyohusishwa na uvamizi wa Marekani na Israel dhidi ya Iran. Ufaransa pamoja na Uingereza zimekuwa zikishinikiza kuanzishwa kwa ujumbe wa ulinzi wa kimataifa utakaotekelezwa baada ya kupungua kwa uhasama, ukihusisha zaidi ya nchi 50 na kutenganishwa na operesheni za kijeshi za vita.

    Katika hatua nyingine, Ufaransa ilipeleka kundi la meli za kivita linaloongozwa na meli ya kubeba ndege ya Charles de Gaullekuelekea Bahari Nyekundu mapema Mei 2026 kama sehemu ya mkakati wa kuimarisha usalama bila kuongeza mvutano. Macron pia anatarajiwa kufanya mikutano na washirika kadhaa, wakiwemo India, ili kujadili uwezekano wa mfumo wa kusindikiza meli kwa hiari mara tu mashambulizi yatakapositishwa.

  • Iran yaonya Ufaransa na Uingereza dhidi ya kupeleka manowari katika Mlango wa Hormuz.

    Iran yaonya Ufaransa na Uingereza dhidi ya kupeleka manowari katika Mlango wa Hormuz.

    Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran anayeshughulikia masuala ya kisheria na kimataifa, Kazem Gharibabadi, ameonya Ufaransa na Uingereza dhidi ya kupeleka manowari katika Mlango wa Hormuz, akisisitiza kuwa Iran haitaruhusu kuingiliwa na mataifa ya nje katika usalama wa njia hiyo muhimu ya bahari.

    Katika ujumbe aliouchapisha kwenye mtandao wa kijamii wa X siku ya Jumapili, Gharibabadi alisema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ndiyo nchi pekee yenye uwezo wa kuhakikisha usalama wa Mlango wa Hormuz, iwe katika nyakati za amani au vita.

    Kauli hiyo imekuja kufuatia taarifa kwamba Ufaransa imepanga kupeleka meli yake ya kubeba ndege za kivita, Charles de Gaulle, katika Bahari Nyekundu na Ghuba ya Aden kama sehemu ya maandalizi ya ushirikiano wa kijeshi wa baadaye kati ya Paris na London katika eneo la Mlango wa Hormuz.

    Aidha, serikali ya Uingereza imesema itatuma moja ya manowari zake katika Bahari Nyekundu kwa kushirikiana na Ufaransa.

    Gharibabadi alionya kuwa kupelekwa kwa majeshi kutoka nje ya eneo hilo karibu na Mlango wa Hormuz kwa kisingizio cha kulinda usafirishaji wa baharini kunaweza kuongeza mvutano na kuzidisha mgogoro katika eneo hilo.

    Alisema pia kuwa kuimarishwa kwa uwepo wa kijeshi katika njia hiyo muhimu ya bahari kunalenga kuficha chanzo halisi cha ukosefu wa usalama katika eneo hilo, akirejea vita alivyodai kuwa vya uchokozi vinavyohusishwa na Marekani na Israel dhidi ya Iran.

    Kwa mujibu wa mwanadiplomasia huyo, usalama wa baharini hauwezi kupatikana kupitia maonyesho ya nguvu za kijeshi, hasa kutoka kwa nchi ambazo, kwa mtazamo wake, zinachangia matatizo ya eneo hilo kwa kuunga mkono au kunyamazia vitendo vya uchokozi na vikwazo dhidi ya Iran.

    Gharibabadi alisisitiza kuwa chanzo kikuu cha ukosefu wa usalama katika eneo hilo ni matumizi yasiyo halali ya nguvu, vitisho dhidi ya mataifa ya pwani, vizuizi vya baharini na kupuuzwa kwa misingi ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa.

    Mwisho, Gharibabadi alionya kuwa manowari za Ufaransa, Uingereza au nchi nyingine yoyote zitakabiliwa na majibu ya haraka na madhubuti kutoka kwa Vikosi vya Jeshi la Iran ikiwa zitahusika katika hatua zozote zisizo halali au za uhasama katika Mlango wa Hormuz.

  • Waziri wa Mambo ya Nje Abbas Araghchi amesisitiza haja ya kuimarisha na kupanua uhusiano wa pande mbili na Vietnam.

    Waziri wa Mambo ya Nje Abbas Araghchi amesisitiza haja ya kuimarisha na kupanua uhusiano wa pande mbili na Vietnam.

    Balozi mpya wa Iran nchini Vietnam, Javad Ghasemi, amekutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, siku ya Jumapili kabla ya kuondoka kuelekea Hanoi kuanza rasmi majukumu yake ya kidiplomasia.

    Katika mkutano huo, Ghasemi alimueleza Waziri Araghchi kuhusu malengo ya ujumbe wake na mipango aliyoiandaa kwa ajili ya kuimarisha uhusiano kati ya Tehran na Hanoi.

    Kwa upande wake, Waziri Araghchi alisisitiza umuhimu wa kupanua na kuimarisha zaidi ushirikiano kati ya Iran na Vietnam, hususan katika sekta za kisiasa, kiuchumi, biashara na utalii.

  • Meli ya gesi ya Qatar yaripotiwa kupita Mlango wa Hormuz kwa ruhusa ya Iran

    Meli ya gesi ya Qatar yaripotiwa kupita Mlango wa Hormuz kwa ruhusa ya Iran

    Meli ya kubeba gesi asilia iliyoyeyushwa (LNG) inayomilikiwa na Qatar, iitwayo “Al‑Khariyat”, imetuma ishara katika maji ya Bahari ya Oman, kulingana na taarifa za ufuatiliaji wa meli.

    Taarifa zinaonyesha kuwa meli hiyo ilionekana jana katika eneo la lango la Mlango wa Hormuz kabla ya kuzima mfumo wake wa utambuzi wa kiotomatiki wa meli (AIS).Meli hiyo inaripotiwa kuelekea Pakistan.

    Vyanzo vinaeleza kuwa huenda ikawa meli ya kwanza isiyohusiana na Iran kuruhusiwa kupita katika Mlango wa Hormuz na Jeshi la Wanamaji la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu tangu kuanza kwa kile kinachotajwa kama mzingiro au vitendo vya uharamia wa baharini vinavyohusishwa na Marekani.

  • Ripoti ya New York Times kuhusu kutumwa kwa bidhaa muhimu na silaha za Urusi kwenda Iran kupitia Bahari ya Caspian.

    Ripoti ya New York Times kuhusu kutumwa kwa bidhaa muhimu na silaha za Urusi kwenda Iran kupitia Bahari ya Caspian.

    New York Times imeripoti kuwa Bahari ya Caspian imekuwa njia muhimu ya kimkakati kwa Iran na Urusi katika kipindi cha mvutano wa kikanda na shinikizo la Marekani.

    Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Urusi imekuwa ikitumia njia ya Bahari ya Caspian kusafirisha bidhaa za kijeshi na kibiashara kwenda Iran, huku ikiendelea kuiunga mkono Tehran dhidi ya mashambulizi na vikwazo vya Marekani.

    Ripoti hiyo pia inaeleza kuwa Bahari ya Caspian sasa ni njia muhimu ya kukwepa vikwazo na mzingiro wa Marekani katika Mlango wa Hormuz. Maafisa wa Marekani wanadai kuwa Urusi hutuma vipuri vya ndege zisizo na rubani (droni) kwenda Iran kupitia njia hiyo.

    Aidha, bidhaa muhimu kama ngano, mahindi na mafuta ya kula ambazo hapo awali ziliingizwa kupitia njia za kimataifa, sasa zinapelekwa Iran kupitia bandari nne za nchi hiyo katika Bahari ya Caspian ili kuhakikisha usalama wa chakula wakati wa hali ya vita.

    Kutokana na ukweli kwamba ni nchi tano pekee za mwambao wa Bahari ya Caspian zenye uwezo wa kufikia eneo hilo, na Marekani kutokuwa na nafasi ya kuingilia shughuli zake, eneo hilo limeelezwa kuwa mahali salama kwa usafirishaji wa kijeshi wa siri.

    Ripoti hiyo inaongeza kuwa baadhi ya meli huzima vifaa vyao vya ufuatiliaji wanapopita katika njia hiyo, jambo linalofanya uangalizi wa satelaiti kuwa mgumu.

  • Mufti wa Oman awataka Waislamu kuunga mkono Iran na Gaza

    Mufti wa Oman awataka Waislamu kuunga mkono Iran na Gaza

    Mufti Mkuu wa Oman, Sheikh Ahmed Al‑Khalili, ametoa wito kwa Waislamu duniani kuonyesha mshikamano wao na Iran na Gaza kufuatia maendeleo ya hivi karibuni katika eneo la Mashariki ya Kati.

    Katika kauli yake kuhusu hali ya eneo hilo, Sheikh Al‑Khalili alisisitiza umuhimu wa umoja wa ulimwengu wa Kiislamu mbele ya mashambulizi yanayolenga nchi na maeneo ya Kiislamu.

    Amesema Waislamu wanapaswa kusimama pamoja na kuonyesha mshikamano dhidi ya aina yoyote ya uchokozi unaolenga Gaza, Iran au sehemu nyingine za ardhi za Kiislamu.

    Mufti huyo pia alisisitiza kuwa Umma wa Kiislamu ni umma mmoja, na kwamba umoja na mshikamano ni muhimu katika kukabiliana na changamoto na mashambulizi dhidi ya nchi za Kiislamu.