Lebo: Masharikiyakati

  • Katz: “Hakuna Kusitisha Mapigano Nchini Lebanon

    Katz: “Hakuna Kusitisha Mapigano Nchini Lebanon

    “Waziri wa Ulinzi wa Israel, Israel Katz, ametoa tamko zito kuhusu hali ya usalama nchini Lebanon, akisisitiza kuwa hakuna makubaliano yoyote ya kusitisha mapigano yanayoendelea katika eneo hilo.

    Katika taarifa yake, Waziri Katz ameweka bayana kuwa jeshi la Israel litaendelea na operesheni zake dhidi ya ‘kundi la Wapinzani’ bila kupumzika.

    Tamko hili linakuja kinyume na taarifa za awali ambazo zilikuwa zikidokeza kuwa huenda kukawa na kulegeza kamba au kupungua kwa mvutano katika mpaka wa Israel na Lebanon kufuatia mazungumzo ya kidiplomasia.

    Hadi sasa, hali inasalia kuwa tete huku jeshi la Israel likionekana kuongeza kasi ya mashambulio yake, hatua ambayo wachambuzi wanaiita kuwa ni ishara ya kuendeleza msukumo wa kijeshi licha ya shinikizo la kimataifa la kutafuta amani.

  • Jeshi la Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, Limezindua Hadharani Boti Mpya ya Mashambulizi ya Kasi Yenye Kubeba Makombora.

    Jeshi la Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, Limezindua Hadharani Boti Mpya ya Mashambulizi ya Kasi Yenye Kubeba Makombora.

    Tehran — Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu la Iran (IRGC) limeonesha hadharani boti mpya ya mashambulizi ya kasi yenye silaha za makombora, inayojulikana kwa jina la “27 Rajab.”

    Boti hiyo yenye mwonekano wa chini na muundo wa kisasa, unaodhaniwa kuwa wa aina ya trimaran au catamaran, imeripotiwa kuwa na uwezo wa kubeba makombora mawili ya cruise yenye masafa ya hadi kilomita 700. Aidha, chombo hicho kinadaiwa kuwa na uwezo wa kufanya kazi katika mawimbi yenye urefu wa hadi mita 3.

    Hatua hiyo inaonekana kuendana na mkakati wa muda mrefu wa Iran wa kutumia kile kinachoitwa “mosquito fleet”, yaani kundi la boti ndogo, za gharama nafuu na zenye mwendo wa kasi, zinazoweza kutumika kwa mashambulizi ya pamoja dhidi ya meli kubwa za kijeshi.

    Wachambuzi wa masuala ya usalama wanaeleza kuwa mbinu hiyo inalenga kuongeza uwezo wa Iran wa kutoa tishio kwa meli za kivita katika Ghuba ya Uajemi na Mlango wa Hormuz, maeneo yenye umuhimu mkubwa kwa usafirishaji wa nishati na usalama wa baharini.

    Kuzinduliwa kwa boti hiyo mpya kunatajwa kuwa sehemu ya juhudi za Iran za kuimarisha uwezo wake wa kijeshi wa majini katika kipindi ambacho mvutano wa kikanda unaendelea kushuhudiwa Mashariki ya Kati.

  • Sayid Mojtaba Khamenei: Vituo vya Marekani katika eneo ni lazima vifungwe

    Sayid Mojtaba Khamenei: Vituo vya Marekani katika eneo ni lazima vifungwe

    Tuna nchi kumi na tano jirani, miongoni mwao zipo kwenye nchi kavu na zengine baharini, na tumekuwa tayari kila wakati kuanzisha uhusiano mzuri pamoja na kila nchi, lakini baadhi ya nchi hizi zimewekewa misingi yenye kulenga udhibiti katika eneo … napendekeza kwamba misingi hii ifungwe haraka iwezekanavyo.

    ✍🏼 Sehemu ya ujumbe wa kwanza wa Ayatullah Seyyed Mojtaba Hosseini Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu.

  • FT Yafichua Hasara na Ufadhili wa “Iran International”, Kituo cha Habari chenye upinzani na Serikali ya Iran.

    FT Yafichua Hasara na Ufadhili wa “Iran International”, Kituo cha Habari chenye upinzani na Serikali ya Iran.

    LONDON — Iran International, kituo cha habari cha lugha ya Kiajemi kilicho London na kinachojitambulisha kama chombo huru huku mara nyingi kikionekana kuwa na mwelekeo wa upinzani dhidi ya serikali ya Iran, kimeingia katika mjadala mpya baada ya uchunguzi wa Financial Times kufichua kuwa kimepata hasara ya zaidi ya pauni milioni 410 katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.

    Ripoti hiyo inasema shirika hilo limepokea ufadhili unaokaribia dola bilioni 1, ikiwemo msamaha wa madeni wa pauni milioni 650 unaohusishwa na miundo ya kifedha iliyofungamana na Kundi la Utafiti na Vyombo vya Habari la Saudi (SRMG).

    Kwa mujibu wa rekodi za kisheria, deni hilo la wanahisa liligeuzwa kuwa hisa mwezi Desemba mwaka jana, huku uongozi wa kituo hicho ukikanusha madai ya kupokea msaada wowote wa kifedha kutoka serikali za Saudi Arabia au Israel, ukisisitiza kuwa madai ya udhibiti wa nje ni propaganda dhidi yao.

  • Vance: Mazungumzo ya Marekani na Iran Yapiga Hatua.

    Vance: Mazungumzo ya Marekani na Iran Yapiga Hatua.

    Makamu wa Rais wa Marekani, JD Vance, amesema mazungumzo kati ya Marekani na Iran yamepiga hatua kubwa, huku pande hizo mbili zikiendelea kujadiliana kuhusu baadhi ya vipengele vya lugha ya makubaliano na vifungu vya rasimu ya mkataba unaotarajiwa kufikiwa.

    Vance amesema bado ni vigumu kusema kwa uhakika ni lini au iwapo Rais Donald Trump atasaini hati ya makubaliano (MoU), akieleza kuwa bado kuna mjadala unaoendelea kuhusu baadhi ya vipengele vya maandishi ya makubaliano hayo. Hata hivyo, amesisitiza kuwa maendeleo yaliyofikiwa hadi sasa yanaashiria kuwa pande hizo zinakaribia kufikia hatua ya kuketi pamoja na kutatua masuala yaliyosalia.

    Kwa mujibu wa Vance, Iran inaonesha nia ya kufikia makubaliano na pia kutaka kufunguliwa kwa Mlango-Bahari wa Hormuz, jambo ambalo Marekani nayo inaliona kuwa la muhimu. Ameeleza kuwa mazungumzo kati ya pande hizo mbili yanaendelea kuhusu suala hilo, huku Washington ikiamini kuwa Tehran imekuwa ikijadiliana kwa nia njema, angalau kwa hatua ya sasa.

    Katika hatua nyingine, Vance amesema Iran imekubali kutotengeneza wala kutomiliki mpango wa nyuklia, na kwamba suala hilo litafuatiliwa na kuthibitishwa kadri muda unavyokwenda. Ameongeza kuwa hali ya sasa inaipa Marekani na washirika wake nafasi ya kuudhoofisha kwa kiasi kikubwa na kwa muda mrefu mpango wa nyuklia wa Iran.

    Licha ya ishara hizo za matumaini, Vance amesema bado kunahitajika maendeleo ya ziada ili kufikia mwafaka wa mwisho, lakini akaonyesha matumaini kuwa mazungumzo yataendelea kuzaa matunda katika siku zijazo.

  • Jeshi la Wanamaji la IRGC lasema meli 23 zimepita Mlango wa Hormuz ndani ya saa 24.

    Jeshi la Wanamaji la IRGC lasema meli 23 zimepita Mlango wa Hormuz ndani ya saa 24.

    Tehran – Jeshi la Wanamaji la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu wa Iran (IRGC) limetangaza kuwa jumla ya meli 23 za kibiashara, zikiwemo meli za mafuta na zile za kubeba makontena, zimepita salama katika Mlango wa Hormuz ndani ya kipindi cha saa 24 zilizopita.

    Kwa mujibu wa taarifa hiyo, meli zote zilivuka njia hiyo ya kimkakati baada ya kufanyika uratibu rasmi na mamlaka za wanamaji za IRGC.

    Katika taarifa iliyotolewa usiku wa Jumatano, IRGC ilisema inaendelea kusimamia kwa karibu njia hiyo ya baharini, ikieleza kuwa ina udhibiti wa kudumu, thabiti na wenye nguvu katika eneo hilo.

    Taarifa hiyo pia iliieleza Ghuba ya Uajemi kuwa ni eneo la bahari linalohusu mataifa ya kanda pekee. Aidha, IRGC ilidai kuwa hali ya sintofahamu ya kiusalama inayoshuhudiwa sasa katika eneo hilo inachangiwa na uwepo pamoja na shughuli za kijeshi za Marekani.

    Kwa mujibu wa taarifa hiyo, majeshi ya Marekani ndiyo chanzo kikuu cha kuyumbisha utulivu wa eneo hilo.