Lebo: Masharikiyakati

  • Marekani Yathibitisha Kufanya Mashambulizi Kusini mwa Iran, Yakana Kukiuka Usitishaji wa Vita.

    Marekani Yathibitisha Kufanya Mashambulizi Kusini mwa Iran, Yakana Kukiuka Usitishaji wa Vita.

    Makubaliano ya kusitisha mapigano yameripotiwa kukiukwa na Marekani kufuatia uthibitisho kutoka kwa vikosi vyake kuhusu kutekeleza mashambulizi katika maeneo ya kusini mwa Iran.

    Kwa mujibu wa shirika la habari la Fox News, likinukuu taarifa kutoka Kamandi Kuu ya Marekani (CENTCOM), mashambulizi hayo yalilenga maalum vituo vya kurushia makombora pamoja na boti zilizokuwa zikijaribu kutega mabomu (mina) baharini.

    Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Msemaji wa Kamandi Kuu ya Marekani ameeleza kuwa vikosi vyao vilitekeleza mashambulizi hayo siku ya Jumatatu kusini mwa Iran. Hata hivyo, msemaji huyo ametetea hatua hiyo akidai kuwa ilichukuliwa kwa lengo la kujilinda dhidi ya vitisho vya kiusalama.

  • MBALAMWEZI YA AMANI: Iran na Marekani Zakaribia Kufikia Makubaliano ya Kihistoria

    MBALAMWEZI YA AMANI: Iran na Marekani Zakaribia Kufikia Makubaliano ya Kihistoria

    BEIJING, CHINA – Juhudi za kidiplomasia za kuleta utulivu kati ya mataifa hasimu ya Iran na Marekani zimechukua mwelekeo mpya, huku kukiwa na ishara za wazi kuwa nchi hizo mbili zipo ukingoni mwa kufikia makubaliano rasmi.

    Taarifa hizi zimefichuliwa na Shirika la Habari la Rasmi la China (Xinhua), likiripoti kuhusu mazungumzo ya faragha na ya ngazi ya juu yaliyofanyika mjini Beijing kati ya Rais wa China, Xi Jinping, na Mkuu wa Jeshi la Pakistan, Jenerali Asim Munir.

    Katika mazungumzo hayo, Jenerali Munir—ambaye amekuwa akitekeleza jukumu la upatanishi—alimfahamisha Rais Xi kuwa mchakato wa maridhiano kati ya Tehran na Washington umepiga hatua kubwa na sasa upo katika hatua za lala-salama.

    “Makubaliano kati ya Iran na Marekani sasa yamekaribia kukamilika. Pande zote mbili zipo katika hatua za mwisho za kufikia muafaka wa kudumu,” alinukuliwa Jenerali Munir.

    Mkuu huyo wa jeshi la Pakistan aliwasili Beijing moja kwa moja akitokea jijini Tehran, safari inayoelezwa kuwa na lengo la kutoa mrejesho wa mwisho kwa uongozi wa China kuhusu maendeleo yaliyofikiwa katika meza ya mazungumzo.

    Hatua hii inatazamwa na wachambuzi wa mambo ya kimataifa kama ushindi mkubwa wa kidiplomasia, huku Pakistan na China zikionekana kuwa na mchango mkubwa katika kuzipatanisha nchi hizo ambazo zimekuwa na uhusiano wa kusuasua kwa miongo kadhaa.

    Ingawa maelezo ya kina ya makubaliano hayo bado hayajawekwa wazi, ripoti hii inatoa matumaini mapya ya kupungua kwa mivutano ya kisiasa na kiuchumi katika ukanda wa Mashariki ya Kati na duniani kote.

  • Mfumuko wa Bei ya Mafuta Waingia Hatua Mpya Marekani: Kampuni ya Walmart Yatoa Onyo Zito

    Mfumuko wa Bei ya Mafuta Waingia Hatua Mpya Marekani: Kampuni ya Walmart Yatoa Onyo Zito

    Mfumuko wa bei ya mafuta nchini Marekani umeingia katika hatua mpya, huku ukizidi kutishia uchumi wa wananchi wake.

    Kampuni kubwa ya rejareja nchini humo, Walmart, imetoa onyo ikieleza kuwa kupanda kwa bei ya nishati hiyo, kufuatia mgogoro wa Mlango wa Bahari wa Hormuz, kumeongeza msukumo na mzigo mzito wa kimaisha kwa kaya nyingi za Wamarekani.

    Kwa mujibu wa takwimu, bei ya galoni moja ya mafuta nchini Marekani imepaa kutoka takriban dola $3 hadi dola $4.56. Kufuatia hali hii, kampuni ya Walmart imetabiri kuwa ukuaji wa mauzo yake utashuka katika miezi ijayo.

    Aidha, wakurugenzi wa kampuni hiyo wametoa tahadhari kuwa endapo mgogoro huo utaendelea, unaweza kusababisha kupanda zaidi kwa bei za vyakula na hatimaye kupunguza uwezo wa manunuzi kwa walaji nchini Marekani.

  • Juhudi za Kusaka Amani: Ujumbe wa Iran Wawasili Qatar Kujadili Usitishaji wa Vita

    Juhudi za Kusaka Amani: Ujumbe wa Iran Wawasili Qatar Kujadili Usitishaji wa Vita

    DOHA, QATAR- Katika hatua muhimu ya kidiplomasia, ujumbe rasmi kutoka nchini Iran, ukiongozwa na Mohammad Bagher Ghalibaf, umewasili jijini Doha, Qatar hivi leo, kwa mujibu wa ripoti kutoka shirika la habari la serikali.

    Ziara hii inatajwa kuwa ni muendelezo wa mchakato wa kidiplomasia unaoendelea kwa kasi. Hatua hizi zilianza katika wiki za hivi karibuni chini ya upatanishi wa serikali ya Pakistan, zikiwa na lengo kuu la kutafuta suluhu na kuhitimisha vita vilivyolazimishwa.

    Wakati wa ziara hii, ujumbe huo wa Iran unatarajiwa kufanya mazungumzo na mashauriano ya kina na viongozi wa ngazi za juu wa serikali ya Qatar. Taarifa zinaeleza kuwa mazungumzo hayo yatajikita katika kujadili vipengele muhimu vinavyohusiana na mchakato wa amani na mikakati ya kukomesha kabisa vita hivyo.

  • Iran Yasisitiza Kuiunga Mkono Hezbollah, Yadai Usitishaji Vita Lebanon Katika Makubaliano Yoyote ya Amani.

    Iran Yasisitiza Kuiunga Mkono Hezbollah, Yadai Usitishaji Vita Lebanon Katika Makubaliano Yoyote ya Amani.

    Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Seyed Abbas Araghchi, amewasilisha ujumbe maalum kwa Katibu Mkuu wa Hezbollah, Sheikh Naim Qassem, akisisitiza msimamo thabiti wa Tehran wa kuendelea kuliunga mkono kundi hilo na msisitizo wa kusitisha vita nchini Lebanon.

    Katika ujumbe huo, Waziri Araghchi amebainisha kuwa Iran itaendelea kutoa ushirikiano na kuunga mkono vuguvugu la kutafuta haki na uhuru, hususan Hezbollah. Ameeleza kuwa msimamo huo ni muendelezo wa ahadi ya kihistoria iliyoachwa na Imamu shahidi na ni utekelezaji wa agano kwa Kiongozi Mkuu wa nchi hiyo, Grand Ayatollah Seyed Ali Khamenei.

    Kuhusu masuala ya kidiplomasia, taarifa hiyo imeweka wazi sharti kuu la Iran katika mchakato wowote wa amani. Imesisitizwa kuwa, tangu mwanzo wa majadiliano, Iran imesimama kidete kuwa makubaliano yoyote yanayohusisha Marekani lazima yaende sambamba na usitishaji vita nchini Lebanon. Hoja hii imeelezwa kuendelea kuwa kipaumbele na takwa la msingi la Serikali ya Jamhuri ya Kiislamu na wananchi wake.

    Aidha, ujumbe huo umefichua taarifa kuhusu juhudi za hivi karibuni za kidiplomasia. Imebainishwa kuwa katika pendekezo la hivi punde lililotolewa na Iran kupitia kwa wasuluhishi wa Pakistan, ambalo linalenga kusitisha vita kwa kudumu, suala la kuijumuisha Lebanon katika makubaliano ya kusitisha mapigano limesisitizwa kwa uzito mkubwa.

    Ujumbe huu wa kidiplomasia unathibitisha wazi msimamo wa Iran kuhusu mshirika wake mkuu nchini Lebanon, Hezbollah, na unaashiria kuwa Tehran inaichukulia Lebanon kama kipengele kisichoweza kutenganishwa katika kutafuta suluhu ya kudumu ya usalama na amani katika ukanda huo.

  • Ufaransa Yampiga Marufuku Waziri wa Usalama wa Israel Kuingia Nchini Humo

    Ufaransa Yampiga Marufuku Waziri wa Usalama wa Israel Kuingia Nchini Humo

    PARIS – Serikali ya Ufaransa imempiga marufuku Waziri wa Usalama wa Taifa wa Israel, Itamar Ben-Gvir, kuingia katika ardhi ya taifa hilo, kufuatia kile kilichotajwa kuwa ni mienendo isiyokubalika dhidi ya raia wa Ufaransa na Ulaya.

    Akithibitisha hatua hiyo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa, Jean-Noël Barrot amesema: “Kuanzia leo, Itamar Ben-Gvir amepigwa marufuku kuingia katika ardhi ya Ufaransa. Uamuzi huu unafuatia vitendo vyake viovu dhidi ya raia wa Ufaransa na Ulaya waliokuwa abiria kwenye msafara wa meli za Global Sumud Flotilla.”Waziri Barrot alisisitiza msimamo wa nchi yake akisema kuwa, Ufaransa haiwezi kuvumilia kuona raia wake wakitishiwa au kufanyiwa ukatili wa namna hiyo, hasa ikifanywa na afisa wa umma.

    Alibainisha kuwa vitendo hivyo ni muendelezo wa mfululizo wa kauli na matendo ya kushtusha, ikiwemo uchochezi wa chuki na ghasia dhidi ya Wapalestina. Aidha, ameeleza kuwa akishirikiana na mwenzake wa Italia, wameuomba Umoja wa Ulaya (EU) kumwekea vikwazo waziri huyo.

    Hatua hii kali inakuja muda mfupi baada ya Ben-Gvir kuchapisha video mtandaoni ikimuonyesha akiwadhihaki wanaharakati wa Gaza waliokamatwa na vikosi vya Israel. Katika video hiyo, wanaharakati hao walionekana wakiwa wamefungwa vitambaa machoni, wamepiga magoti na kufungwa mikono yao katika Bandari ya Ashdod.

    Tukio hilo limeibua shutuma kali kimataifa, kiasi cha kumfanya Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, kukaririwa akisema kuwa mwenendo wa Ben-Gvir “hauendani na maadili na kanuni za Israel.”Kufuatia uamuzi huu, Ufaransa inakuwa nchi ya kwanza barani Ulaya kuchukua hatua kwa vitendo, huku wimbi la shinikizo la kidiplomasia likizidi kusambaa.

    Waziri Mkuu wa Uhispania tayari ametangaza kuanzisha juhudi za kuwapiga marufuku mawaziri wa Israel kuingia ndani ya nchi za Umoja wa Ulaya (EU), na Italia inashinikiza vikwazo vya pamoja vya EU. Aidha, imeripotiwa kuwa Croatia imegoma kumpokea balozi wa Israel kwa takriban miezi saba sasa.