Lebo: Masharikiyakati

  • MILIPUKO YARIPOTIWA KATIKA MJI WA JASK, IRAN

    MILIPUKO YARIPOTIWA KATIKA MJI WA JASK, IRAN

    AJASK, IRAN – Sauti za milipuko isiyopungua mitatu zimesikika katika mji wa pwani wa Jask, ulioko katika mkoa wa Hormozgan nchini Iran, kulingana na vyanzo vya eneo hilo.

    Hadi sasa, hakuna taarifa rasmi kuhusu chanzo cha milipuko hiyo au uharibifu wowote ulioweza kusababishwa. Mamlaka husika bado hazijatoa tamko lolote kufuatia tukio hilo, huku uchunguzi ukiendelea katika eneo hilo.

    Taarifa zaidi kuhusu tukio hili na madhara yake zitatolewa punde zitakapopatikana.

  • UAE yaomba mazungumzo yarejee na mashambulizi ya miundombinu yakome

    UAE yaomba mazungumzo yarejee na mashambulizi ya miundombinu yakome

    Abu Dhabi, Falme za Kiarabu (UAE) — Serikali ya Falme za Kiarabu imesema ina wasiwasi mkubwa kuhusu ongezeko la mvutano wa kijeshi katika eneo la Mashariki ya Kati, ikitoa wito wa kusitishwa mara moja kwa uhasama, kupunguza mivutano na kurejea kwenye mazungumzo ya kidiplomasia ili kuzuia hali kuzidi kuwa mbaya.

    Katika taarifa yake, UAE imesisitiza umuhimu wa pande zote kuchukua tahadhari kubwa na kuepuka hatua zinazoweza kusababisha mzozo mpana zaidi katika eneo hilo lenye umuhimu mkubwa kwa usalama na uchumi wa dunia.

    Miongoni mwa hatua ilizozitaka UAE ni kusitishwa kwa mapigano mara moja, kuonyeshwa kwa kiwango cha juu cha kujizuia na kurejeshwa kwa njia za mazungumzo kama suluhisho la kupunguza tofauti zilizopo.

    Serikali hiyo pia imesisitiza umuhimu wa kuhakikisha usafirishaji salama na usiokatizwa kupitia Mlango wa Hormuz, ikieleza kuwa njia hiyo ni muhimu kwa uchumi wa dunia kutokana na nafasi yake katika usafirishaji wa nishati na biashara ya kimataifa.

    “Usalama na uhuru wa usafirishaji kupitia Mlango wa Hormuz ni jambo muhimu kwa uthabiti wa uchumi wa dunia,” UAE imesisitiza katika msimamo wake.

    Aidha, Abu Dhabi imeonya dhidi ya mashambulizi yanayolenga miundombinu ya kiraia kama shule, hospitali, mitambo ya kusafisha maji na vituo vya nishati, ikisema vitendo hivyo ni ukiukaji mkubwa wa sheria za kimataifa na haviwezi kuhalalishwa kwa sababu yoyote.

  • Trump Aomboleza Vifo vya Wanajeshi Marekani Jordan, Aendelea Kutoa Onyo kwa Iran

    Trump Aomboleza Vifo vya Wanajeshi Marekani Jordan, Aendelea Kutoa Onyo kwa Iran

    Washington, Marekani — Rais wa Marekani Donald Trump amesema anasikitishwa na kifo cha wanajeshi wawili wa Marekani waliouawa nchini Jordan, huku akisisitiza kuwa Iran haitakiwi kumiliki silaha za nyuklia. Kauli hiyo imekuja wakati mvutano kati ya Washington na Tehran ukiendelea kuongezeka baada ya Iran kutangaza kusitisha baadhi ya ahadi zake chini ya makubaliano ya muda.

    Akizungumza na waandishi wa habari, Trump alisema vifo hivyo ni jambo la kusikitisha na kuwapongeza wanajeshi hao kwa huduma yao kwa taifa.

    “Tunachukia kuona jambo hili likitokea. Wamefariki wakiwa katika huduma kwa nchi yetu,” Trump alisema.

    Rais huyo wa Marekani hakutoa maelezo ya kina kuhusu mazingira ya tukio hilo, lakini alirudia msimamo wake kwamba Iran haipaswi kuwa na silaha za nyuklia.

    “Iran haiwezi na haipaswi kuwa na silaha ya nyuklia,” alisema Trump.

    Kauli hiyo imekuja baada ya taarifa za vifo vya wanajeshi wawili wa Marekani nchini Jordan, tukio lililoongeza shinikizo la kisiasa katika eneo la Mashariki ya Kati ambalo tayari limekuwa likikabiliwa na mvutano mkubwa kati ya Marekani na Iran.

    Baadaye, baada ya Iran kutangaza kusitisha utekelezaji wa baadhi ya majukumu yake chini ya makubaliano ya muda, Baada ya Marekani kuvunja maagano hayo kwa kufanya mashambulizi Iran, Trump alionyesha kutokuwa na wasiwasi kuhusu hatua hiyo, akisema:

    “Sijali kabisa,” akimaanisha uamuzi wa Tehran.

    Hatua ya Iran imeelezwa kuwa ni majibu ya kile inachokitaja kama shinikizo la nje na hatua za upande mmoja zinazokiuka haki yake ya kufanya maamuzi huru kuhusu masuala yake ya kimkakati.

    Wachambuzi wa masuala ya kimataifa wanaonya kuwa kuendelea kwa mvutano kati ya mataifa hayo mawili kunaweza kuongeza hatari ya mzozo mpana zaidi katika eneo ambalo tayari limeathiriwa na vita na migogoro ya muda mrefu.

    Mzozo huu unaibua tena mjadala kuhusu usawa katika mfumo wa kimataifa, matumizi ya nguvu za kijeshi na haki ya mataifa kujitegemea katika kuamua sera zao za ndani na za kigeni bila shinikizo la mataifa yenye nguvu.

    Kwa sasa, macho yanaelekezwa kwenye hatua zitakazochukuliwa na Washington na Tehran katika siku zijazo. Ikiwa njia za kidiplomasia zitapewa nafasi, kuna uwezekano wa kupunguza mvutano; lakini kuendelea kwa sera za mashinikizo na makabiliano kunaweza kuongeza hatari ya kuyumbisha zaidi usalama wa Mashariki ya Kati.

  • CENTCOM yakiri vifo vya wanajeshi wawili wa Marekani nchini Jordan baada ya mashambulizi ya Iran

    CENTCOM yakiri vifo vya wanajeshi wawili wa Marekani nchini Jordan baada ya mashambulizi ya Iran

    Marekani imethibitisha kuwa wanajeshi wake wawili wameuawa nchini Jordan na mwingine bado hajulikani alipo, kufuatia mashambulizi ya makombora na ndege zisizo na rubani (drones) yanayodaiwa kufanywa na Iran.


    Kamandi Kuu ya Marekani (CENTCOM) imetoa taarifa rasmi ikieleza kuwa tukio hilo lilitokea baada ya mashambulizi yaliyolenga maeneo ya kijeshi nchini Jordan.


    Kwa mujibu wa taarifa hiyo, wanajeshi wawili wa Marekani walifariki katika shambulio hilo, huku mwanajeshi mwingine akiendelea kutafutwa.


    CENTCOM imesema wanajeshi wanne waliojeruhiwa walipelekwa hospitalini nchini Jordan kwa matibabu na baadaye kuruhusiwa, huku wale waliopata majeraha madogo wakirejea kwenye majukumu yao.


    Aidha, jeshi hilo limesema majina ya wanajeshi waliofariki hayatatangazwa mara moja, na yataendelea kuwa siri kwa muda wa saa 24 baada ya familia zao kufahamishwa rasmi, kwa mujibu wa taratibu za kijeshi za Marekani.


    Tukio hilo linaongeza mvutano wa kijeshi katika eneo la Mashariki ya Kati, huku Marekani na Iran zikiendelea kuwa katika mzozo unaohusisha mashambulizi na majibu ya kijeshi.

  • The Guardian: Trump, Sio Iran, Ndiye Tishio Kubwa Zaidi kwa Dunia

    The Guardian: Trump, Sio Iran, Ndiye Tishio Kubwa Zaidi kwa Dunia

    Mgogoro kati ya Marekani na Iran umeingia katika hatua yenye wasiwasi mkubwa, huku mashambulizi ya kijeshi yakiendelea kuongeza hofu ya vita vya muda mrefu ambavyo vinaweza kuathiri siasa za kimataifa, uchumi wa dunia na hasa mataifa yanayoendelea.

    Katika uchambuzi uliochapishwa na The Guardian, hoja kuu inayojitokeza ni kwamba sera ya Rais Donald Trump dhidi ya Iran inaweza kuwa imeiweka Marekani kwenye mtego wa kijeshi ambao ni vigumu kutoka bila gharama kubwa. Badala ya kuleta matokeo ya haraka yaliyotangazwa na Washington, operesheni hizo zimeibua maswali kuhusu ufanisi wa matumizi ya nguvu kama njia ya kutatua migogoro ya kimataifa.

    Wakosoaji wa mkakati huo wanasema malengo makubwa yaliyotajwa na Marekani na washirika wake, ikiwemo kudhibiti mpango wa nyuklia wa Iran, kudhoofisha ushawishi wake wa kikanda au kulazimisha mabadiliko ya kisiasa, yanaonekana kuwa magumu kufikiwa kupitia mashambulizi ya kijeshi pekee.

    Moja ya maeneo muhimu yanayoathiriwa na mzozo huu ni Mlango wa Hormuz, njia ya kimkakati inayopitisha sehemu kubwa ya biashara ya nishati duniani. Kukosekana kwa utulivu katika eneo hilo kunaweza kuongeza gharama za mafuta, kuvuruga minyororo ya usambazaji na kuongeza shinikizo la kiuchumi kwa nchi nyingi za Afrika, Asia na Amerika Kusini ambazo tayari zinakabiliwa na changamoto za maendeleo.

    Kwa mtazamo mpana, mgogoro wa Iran unaonyesha changamoto ya mfumo wa kimataifa ambapo matumizi ya nguvu za kijeshi mara nyingi huleta madhara makubwa kwa raia na uchumi wa nchi zisizo na nafasi kubwa katika maamuzi ya kimataifa. Historia ya migogoro ya Mashariki ya Kati inaonyesha kuwa ushindi wa kijeshi pekee mara chache huleta amani ya kudumu bila mchakato wa kisiasa.

    Hatua inayofuata kwa jumuiya ya kimataifa itakuwa kutafuta njia ya diplomasia, kupunguza mvutano na kuhakikisha usalama wa raia pamoja na utulivu wa uchumi wa dunia. Kwa mataifa ya Global South, mgogoro huu ni ukumbusho wa umuhimu wa kujenga mifumo huru ya kiuchumi na kisiasa isiyoyumbishwa kirahisi na migogoro ya mataifa yenye nguvu.

  • Kundi la mtandao la Iran laharibu terabaiti 120 za taarifa za kifedha za Israel

    Kundi la mtandao la Iran laharibu terabaiti 120 za taarifa za kifedha za Israel

    Kundi linaloitwa Jukwaa la Msaada wa Kielektroniki (Cyber Support Front) limedai kufanya shambulio kubwa la kimtandao dhidi ya taasisi za kifedha za Israel, likisema limeharibu takribani terabaiti 120 za taarifa nyeti za kifedha na kiulinzi za taifa hilo.

    Katika taarifa iliyotolewa, kundi hilo lilidai kuwa lilifanikiwa kuvamia mifumo ya taasisi kadhaa muhimu za kifedha na uhasibu, na kusababisha uharibifu mkubwa kwa miundombinu ya kiuchumi na mifumo ya kodi ya Israel.

    Limetaja kampuni tatu za kifedha kuwa zililengwa katika operesheni hiyo, ikiwemo kampuni ya uhasibu na ukaguzi ya Oren Levy, kampuni ya ushauri wa kifedha na kodi ya Finco pamoja na kampuni ya Milkovsky Consulting and Investment iliyopo Tel Aviv.

    Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kundi hilo lilidai kufuta takribani terabaiti 120 za data pamoja na nakala zake za kuhifadhi taarifa (backup), hatua ambayo lilisema ilisababisha mifumo ya kompyuta, seva za kuhifadhi data na miundombinu ya mawasiliano ya taasisi hizo kushindwa kufanya kazi.

    Kundi hilo pia lilidai kuwa shambulio hilo limesababisha usumbufu katika shughuli za kifedha na kodi, huku wateja wa kampuni hizo wakikabiliwa na changamoto za upatikanaji wa huduma.