Mwandishi: Suleiman Ali

  • Nyaraka za Siri Zafichua: Jinsi Marekani Ilivyoshinikiza Kuondolewa Madarakani kwa Imran Khan

    Nyaraka za Siri Zafichua: Jinsi Marekani Ilivyoshinikiza Kuondolewa Madarakani kwa Imran Khan

    Waraka wa siri wa kidiplomasia wa Pakistan uliotolewa kwa mara ya kwanza tarehe 18 Mei, unathibitisha kuwa mwanadiplomasia mkuu wa Marekani alishinikiza kuondolewa madarakani kwa aliyekuwa Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Imran Khan, mwaka 2022.

    Kwa mujibu wa waraka huo uliodokezwa na mtandao wa Drop Site News, Donald Lu, ambaye kwa wakati huo alikuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani anayeshughulikia masuala ya Asia Kusini na Kati, alimwambia Balozi wa Pakistan mjini Washington, Asad Majeed Khan, kwamba “yote yatasamehewa” endapo kiongozi huyo angeondolewa kupitia kura ya kutokuwa na imani naye bungeni.

    Mawasiliano hayo ya kidiplomasia yalifanyika baada ya Bw. Khan kufanya ziara mjini Moscow na kukutana na Rais wa Urusi, Vladimir Putin, tarehe 24 Februari 2022, siku ambayo Urusi ilianzisha uvamizi wake nchini Ukraine.

    Katika waraka huo wa tarehe 7 Machi 2022 uliowekewa alama ya “Siri / Kutosambazwa,” Bw. Lu ananukuliwa akieleza kuwa mkutano wa Khan na Putin ulizua “wasiwasi mkubwa” kwa serikali ya Washington.

    Kwa upande wake, Serikali ya Islamabad ilijitetea ikisema kuwa safari ya Khan nchini Urusi ilikuwa imepangwa miezi kadhaa mapema na haikuwa na uhusiano wowote na uvamizi wa Ukraine, ikisisitiza kuwa Pakistan ilikuwa inafuata sera ya “kutoegemea upande wowote” katika mzozo huo.

    Zaidi ya hayo, waraka huo ulijumuisha tathmini ya Balozi Asad Majeed Khan aliyoamini kuwa ujumbe wa Donald Lu ulikuwa umepata baraka kutoka Ikulu ya Marekani (White House).

    Balozi huyo pia alibainisha kuwa matamshi ya mwanadiplomasia huyo wa Marekani yalikuwa ni dhahiri kuingilia kati masuala ya ndani ya kisiasa ya Pakistan.

  • Trump viongozi wa Qatar, Saudi Arabia na UAE wameniomba kuakhirisha mashambulizi dhidi ya Iran kwa sasa

    Trump viongozi wa Qatar, Saudi Arabia na UAE wameniomba kuakhirisha mashambulizi dhidi ya Iran kwa sasa

    WASHINGTON D.C.–

    Rais wa Marekani, Donald Trump, ametangaza kusitisha kwa muda operesheni ya kijeshi iliyokuwa imepangwa dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

    Katika chapisho lake mtandaoni Truth Social, Rais Trump amesema uamuzi huo umefikiwa baada ya kupokea wito maalum kutoka kwa viongozi wa mataifa ya Ghuba. Viongozi waliohusika katika mazungumzo hayo ni pamoja na Emir wa Qatar, Tamim bin Hamad Al Thani; mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia, Mohammed bin Salman Al Saud; na Rais wa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Mohamed bin Zayed Al Nahyan.

    Rais Trump ameeleza kuwa viongozi hao wamemshawishi kusitisha mashambulizi hayo ili kuruhusu mazungumzo ya kidiplomasia ya ngazi ya juu yaliyopo sasa kuchukua mkondo wake.

    “Kufuatia heshima yangu kwa viongozi hao wakuu na washirika wetu, nimewaelekeza Waziri wa Ulinzi, Pete Hegseth, na Mwenyekiti wa Wakuu wa Majeshi ya Pamoja, Jenerali Daniel Caine, kutotekeleza shambulio lililokuwa limepangwa dhidi ya Iran,” ilisema taarifa hiyo ya Rais.

    Rais amesisitiza kuwa lengo kuu la mazungumzo hayo ni kuhakikisha kunapatikana makubaliano yanayokubalika na Marekani pamoja na washirika wake katika Mashariki ya Kati na kwingineko, huku akisisitiza kipaumbele cha kimkakati: “Hatutakubali Iran kumiliki silaha za nyuklia.”

    Licha ya kusitisha mashambulizi hayo, Rais Trump ametoa onyo kali kwa Iran. Amesema amewapa maagizo maalum maafisa wake wa usalama na jeshi kuwa katika utayari wa hali ya juu.”Nimeelekeza jeshi la Marekani kuwa tayari kuendelea na shambulio kubwa na la kina dhidi ya Iran wakati wowote, iwapo makubaliano yanayokubalika hayatofikiwa,” aliongeza Rais Trump.

  • DONALD TRUMP AVISHUTUMU VYOMBO VYA HABARI KWA UPOTOSHAJI

    DONALD TRUMP AVISHUTUMU VYOMBO VYA HABARI KWA UPOTOSHAJI

    WASHINGTON D.C. – Rais wa Marekani, Donald J. Trump, ametoa tamko kali kupitia mtandao wake wa kijamii akivishambulia vyombo vikuu vya habari na wapinzani wake wa kisiasa, akidai kuwepo kwa upendeleo uliopitiliza katika uripoti wa habari.

    Katika tamko hilo lililojaa lugha ya msisitizo, Trump ameelezea mfano wa tukio la ajabu la nchi ya Iran kusalimu amri kikamilifu mbele ya nguvu za kijeshi za Marekani.

    Trump ameeleza kuwa, hata kama jeshi la wanamaji la Iran lingezamishwa lote, jeshi lake la anga kusambaratishwa, na viongozi wake kusaini nyaraka za kushindwa vita huku wakipeperusha bendera nyeupe jijini Tehran, vyombo vya habari bado vingepindua ukweli huo.

    Trump amevitaja moja kwa moja vyombo kama The New York Times, CNN, na The Wall Street Journal (ambalo ameliita kwa dhihaka kama ‘The China Street Journal’), akidai kuwa vingetangaza tukio hilo kama “ushindi mkubwa na wa kishindo” wa Iran dhidi ya Marekani.“Vyombo vya habari vya ‘Fake News’ na Wanachama wa Democratic wamepoteza mwelekeo kabisa,” alisema Trump katika sehemu ya ujumbe wake, akitumia neno la dhihaka “Dumacrats” kurejelea wapinzani wake.

    Tamko hili linaakisi mivutano inayoendelea kati ya kiongozi huyo na tasnia ya habari nchini Marekani, huku akisisitiza kuwa mfumo wa habari na siasa za upande wa kushoto nchini humo “vimechanganyikiwa” na haviwezi kutoa ripoti za haki kuhusu mafanikio ya Marekani chini ya uongozi wake au nguvu ya nchi hiyo kimataifa.

    Hadi sasa, vyombo vya habari vilivyotajwa havijatoa jibu rasmi dhidi ya shutuma hizo za hivi karibuni kutoka kwa Rais huyo wa 45 wa Marekani.

  • “Tumerudi Miaka ya 90”: Mbinu za Msituni za Hizbullah Zaiacha Israel Ikitaka Kusitisha Vita Haraka.

    “Tumerudi Miaka ya 90”: Mbinu za Msituni za Hizbullah Zaiacha Israel Ikitaka Kusitisha Vita Haraka.

    Kituo cha televisheni cha Channel 13 nchini Israel kimeripoti kuhusu mabadiliko ya mbinu za kivita za kundi la Hzb. Allah, kufuatia shambulio la hivi karibuni lililojeruhi wanajeshi wanne wa Israel.

    aKwa mujibu wa taarifa hiyo, Hzb. Allah ilifanikiwa kutega kifaa cha mlipuko baada ya kufuatilia kwa karibu nyendo za vikosi vya Israel na kisha kukilipua. Kituo hicho kimeeleza kuwa kundi hilo sasa limerejea katika mbinu za vita vya msituni (guerrilla warfare).

    Mbinu hii, ambayo haihitaji idadi kubwa ya wapiganaji, imetajwa kuwa na ufanisi mkubwa uwanjani kwa kuvifuatilia, kuvichosha, na kuvisababishia hasara vikosi vya Israel.

    Katika uchambuzi wake, Channel 13 imefananisha hali inayoendelea hivi sasa na ile ya miaka ya 1990 katika eneo lililojulikana kama “ukanda wa usalama” kusini mwa Lebanon, ikibainisha kuwa mazingira ya sasa yanaakisi kikamilifu hali halisi ya kipindi hicho.

    Kutokana na hali hiyo uwanjani, kituo hicho kimehitimisha kwa kusema kuwa, kufikiwa kwa makubaliano ya kusitisha mapigano kikamilifu na mara moja utakuwa ni “uamuzi sahihi” hasa endapo utatangazwa sasa na Rais wa Marekani, Donald Trump.

  • Julius Malema Ahoji Kwanini Mnangagwa (rais wa Zimbabwe) Alinusurika Corona Ila Sio Magufuli

    Julius Malema Ahoji Kwanini Mnangagwa (rais wa Zimbabwe) Alinusurika Corona Ila Sio Magufuli

    JOHANNESBURG, 17 Mei 2026 — Kiongozi wa chama cha Economic Freedom Fighters (EFF), Julius Malema, amezua mjadala kufuatia kauli yake ya kuhoji namna janga la COVID‑19 lilivyodai maisha ya aliyekuwa Rais wa Tanzania, hayati John Magufuli, huku Rais wa Zimbabwe, Emmerson Mnangagwa, akiendelea kuishi.

    Akizungumza katika hafla ya kisiasa, Malema alimwelezea Magufuli kama “rais aliyekuwa mstari wa mbele katika utekelezaji wa majukumu yake,” na kudai kuwa aliondolewa na virusi vya corona.

    Katika maelezo yake, alihoji kwa nini janga hilo “halikumgusa” Mnangagwa, ambaye alimkosoa vikali kwa kumtaja kama kiongozi asiye na uwezo.

    Kauli hiyo imeibua mjadala katika mitandao ya kijamii na miongoni mwa wachambuzi wa siasa, huku baadhi wakiona ni maoni ya kisiasa yenye lengo la kukosoa uongozi wa Zimbabwe, na wengine wakisisitiza umuhimu wa kuheshimu kumbukumbu za viongozi waliotangulia mbele ya haki.

    Hadi sasa, hakujawa na majibu rasmi kutoka serikalini Zimbabwe kuhusu kauli hizo.

  • Heche: Lissu Aumwa Tumbo kwa Maumivu Makali Gerezani

    Heche: Lissu Aumwa Tumbo kwa Maumivu Makali Gerezani

    Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), John Heche, amesema amepokea taarifa kutoka kwa mdogo wa Mwenyekiti wa chama hicho, Tundu Lissu, kuwa Lissu anaumwa tumbo na anapata maumivu makali tangu jana.

    Heche alitoa kauli hiyo Mei 17, 2026 wakati akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika katika Viwanja vya Shule ya Msingi Nyankumbu, Kata ya Nyankumbu, Wilaya na Mkoa wa Geita.

    Amesema mdogo wa Lissu aitwaye Vicent alimpa taarifa kwa njia ya simu kuwa Lissu alianza kuumwa tumbo tangu jana jioni na anaendelea kupata maumivu makali, hali inayozua wasiwasi kwa viongozi na wanachama wa chama hicho.

    Heche ameongeza kuwa chama hicho kimesisitiza mara kadhaa kuwa endapo kiongozi wao atapata madhara akiwa gerezani, hali hiyo haitavumilika.

    “Tukiwa njiani kuja hapa nimepigiwa simu na mdogo wake Lissu aitwaye Vicent akiniambia kuwa tangu jana jioni Mwenyekiti wetu anaumwa sana tumbo. Tumbo linamkata na ana maumivu makali sana. Tumesema tena na tena, Lissu akipata shida haitaeleweka nchi hii,” amesema Heche.