Yemen wadai kuitungua droni ya Marekani aina ya MQ-9 Reaper katika eneo la Safer, mkoani Marib.Mpaka sasa, hakuna tamko rasmi lililotolewa na msemaji wa jeshi la Yemen, Yahya Saree, kuhusu tukio hilo. Kwa upande mwingine, jeshi la Marekani bado halijathibitisha wala kukanusha madai ya kupotea kwa droni hiyo.
Mwandishi: Suleiman Ali
-

Felicien Kabuga Mtuhumiwa wa Mauwaji ya Kimbari nchini Rwanda aaga dunia
Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita (ICC) yenye makao yake The Hague imetangaza kuwa mshukiwa wa mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 nchini Rwanda, Félicien Kabuga, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 90.
Taarifa zinaeleza kuwa Kabuga alifariki Jumamosi alipokuwa akipatiwa matibabu hospitalini, huku Jaji Graciela Gatti Santana ameamuru uchunguzi wa haraka kufanyika ili kubaini chanzo cha kifo hicho.Kabuga alikuwa miongoni mwa watu waliotafutwa zaidi duniani kwa tuhuma za kuhusika katika kupanga na kuchochea mauaji ya takribani watu laki nane waliouawa kati ya Aprili na Juni 1994 nchini Rwanda.
Alikamatwa nchini Ufaransa mwaka 2020 kabla ya kuhamishiwa The Hague, ambako alikabiliwa na mashtaka ya mauaji ya kimbari, njama za kutekeleza mauaji hayo pamoja na uhalifu dhidi ya ubinadamu.
-

Mpangilio Mpya wa Kimataifa: Spika wa Iran Asema Mustakabali wa Dunia haipo tena Marekani
Spika wa Bunge la Iran, Baqir Ghalibaf, amesema dunia iko katika hatua ya kuingia katika mpangilio mpya wa kimataifa.
Akinukuu kauli ya Rais wa China, Xi Jinping, Ghalibaf alisema kuwa “mabadiliko ambayo hayajaonekana katika kipindi cha karne moja yanaongezeka kasi duniani kote.”
Alisisitiza kuwa ukakamavu wa siku 70 wa taifa la Iran dhidi ya uvamizi wa Marekani na Israel umechangia kuharakisha mabadiliko hayo. Ghalibaf pia alieleza kuwa mustakabali wa dunia unazidi kuelekea kwa nchi za Ulimwengu wa Kusini (Global South).
-

Trump ashangazwa na Taarifa za kijasusi za Marekani kuhusu makombora ya chini ya ardhi ya Iran
Taarifa mpya za kijasusi za Marekani zimeeleza kuwa uwezo wa makombora ya chini ya ardhi wa Iran ni mkubwa na tata zaidi kuliko ilivyokadiriwa hapo awali.
Kwa mujibu wa ripoti iliyochapishwa na Middle East Monitor, tathmini hizi zimewashangaza baadhi ya maafisa wa ngazi za juu nchini Marekani, akiwemo rais Donald Trump.
Ripoti hizo zinaonyesha kuwepo kwa mtandao mpana wa kile kinachoitwa “miji ya makombora” pamoja na vituo vya kurushia makombora vilivyojengwa chini ya ardhi. Miundombinu hii inadaiwa kuwa imeundwa kwa namna inayoweza kustahimili mashambulizi ya kawaida ya anga.
Wachambuzi wa usalama wanasema kuwa uwezo huo wa siri unaiwezesha Iran kurusha makombora kwa ghafla na pia kuhamisha vifaa vyake kwa haraka.
Hali hiyo, kwa mujibu wa tathmini hizo, inaleta changamoto kubwa kwa mikakati ya mashambulizi ya kijeshi ya Washington na pia inaashiria mapungufu katika baadhi ya juhudi za awali za upelelezi.
-

Blinken: Chaguo la kijeshi dhidi ya Iran halikuwa suluhisho boraw
Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje wa Marekani, Antony Blinken, amesema kuwa kutumia nguvu za kijeshi dhidi ya Iran ni chagua la makosa, licha ya mjadala uliokuwepo kuhusu hatua hiyo katika serikali mbalimbali za Marekani.
AAkizungumza katika mahojiano ambayo pia yalihudhuriwa na Kansela wa zamani wa Ujerumani, Olaf Scholz, Blinken alisema kuwa suala la kutumia chaguo la kijeshi dhidi ya Iran limekuwa likijadiliwa kwa muda mrefu, hata katika kipindi cha utawala wa Rais wa zamani Barack Obama.
Alieleza kuwa serikali yao ililichunguza kwa makini chaguo hilo, lakini mwishowe ilihitimisha kwamba kutokana na baadhi ya maendeleo na matukio yanayoonekana sasa, hatua ya kijeshi haikuwa njia bora ya kushughulikia suala hilo.Katika mahojiano hayo, Blinken pia alitoa onyo kuhusu kupungua kwa uaminifu wa Marekani miongoni mwa washirika wake wa Ulaya.
Akirejea matokeo ya utafiti mpya wa maoni ya umma, alisema kuwa takribani asilimia 70 ya raia wa Ujerumani sasa wanaiona Marekani kama adui au mshindani badala ya mshirika.
-

Baada ya Trump; Putin kuzuru China wiki ijayo – je China ndiye mkuu mpya?
Rais wa Urusi Vladimir Putin anatarajiwa kufanya ziara nchini China wiki ijayo. Hayo yameripotiwa Ijumaa na gazeti la South China Morning Post likinukuu vyanzo vinavyofahamu maandalizi ya safari hiyo.
Kwa mujibu wa vyanzo hivyo, ziara ya Putin haitatarajiwa kuwa na sherehe au maandalizi makubwa kama yale yaliyoonekana wakati wa mkutano wa viongozi wa Marekani na China uliofanyika Beijing wiki hii.
Ripoti zinaeleza kuwa ziara hiyo imepangwa kufanyika kwa muda mfupi, ikitarajiwa kufanyika siku ya Jumatano pekee. Vyanzo visivyotajwa majina vimesema safari hiyo ni sehemu ya mawasiliano na ushirikiano wa kawaida kati ya Moscow na Beijing, bila mipango ya gwaride au mapokezi makubwa.
Wakati huo huo, msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov amethibitisha kuwa maandalizi ya ziara hiyo yanaendelea. Akiwaambia waandishi wa habari Ijumaa, Peskov amesema tarehe rasmi ya safari hiyo itatangazwa hivi karibuni.
