Mwandishi: Suleiman Ali

  • Dola Trilioni 1.2 Kujenga ‘Golden Dome’: Je, Mradi wa Trump Utaweza Kuilinda Marekani Dhidi ya Urusi na China?

    Dola Trilioni 1.2 Kujenga ‘Golden Dome’: Je, Mradi wa Trump Utaweza Kuilinda Marekani Dhidi ya Urusi na China?

    WASHINGTON — Ofisi ya Bajeti ya Bunge la Marekani (CBO) imesema kuwa mfumo wa ulinzi wa makombora unaopendekezwa na Rais Donald Trump, unaojulikana kama “Golden Dome,” unaweza kugharimu hadi dola trilioni 1.2 katika kipindi cha miaka 20, kiwango kinachozidi kwa kiasi kikubwa makadirio ya awali ya Pentagon ya dola bilioni 185.

    Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Golden Dome ni mradi mkubwa wa kuimarisha ulinzi wa Marekani dhidi ya mashambulizi ya makombora kupitia matumizi ya vizuia‑makombora vya ardhini pamoja na mtandao mkubwa wa satelaiti za anga. Mfumo huo unatarajiwa kujumuisha karibu satelaiti 7,800 zitakazokuwa zikifuatilia na kuzuia makombora ya balistiki pamoja na yale ya kasi ya juu kabla hayajafika Marekani.

    CBO imeeleza kuwa makadirio yake yanajumuisha gharama zote za maendeleo ya teknolojia, usakinishaji wa mfumo, uendeshaji na matengenezo ya muda mrefu. Ripoti hiyo imebainisha kuwa sehemu kubwa ya gharama itatokana na mfumo wa vizuia‑makombora vya anga, ambao unaweza kuchukua karibu asilimia 70 ya bajeti ya mradi mzima.

    Hata hivyo, Pentagon imeendelea kusimamia makadirio yake ya awali ya dola bilioni 185, ikisema tathmini hiyo ilitokana na hatua za mwanzo za upangaji wa mradi huo.Ripoti ya CBO pia imeonya kuwa licha ya uwekezaji mkubwa unaohitajika, mfumo huo unaweza bado kushindwa kukabiliana na mashambulizi makubwa ya makombora kutoka mataifa yenye uwezo mkubwa wa kijeshi kama Urusi au China.

    Tofauti kubwa kati ya makadirio ya CBO na Pentagon imeibua mjadala mkali ndani ya Bunge la Marekani kuhusu gharama, ufanisi na umuhimu wa kuendelea na mradi huo katika kipindi ambacho serikali ya shirikisho inakabiliwa na changamoto za matumizi ya bajeti.

  • CHOKOCHOKO AU KUKOSEA NJIA? Austria Yaonyesha Misuli kwa Ndege za Marekani Zilizovamia Anga Yake

    CHOKOCHOKO AU KUKOSEA NJIA? Austria Yaonyesha Misuli kwa Ndege za Marekani Zilizovamia Anga Yake

    VIENNA, AUSTRIA — Katika tukio ambalo limezua hisia za kiusalama, Jeshi la Austria limelazimika kurusha ndege zake za kivita aina ya Eurofighter kwa siku mbili mfululizo, kufuatia ndege za Jeshi la Anga la Marekani (USAF) kugundulika zikiendesha shughuli zake ndani ya anga ya Austria bila kuwa na vibali halali vya kupita.

    Hatua hii imechukuliwa kwa uzito mkubwa ikizingatiwa kuwa Austria ni taifa ambalo halifungamani na upande wowote kisiasa na kijeshi (neutral).

    Kwa mujibu wa taarifa rasmi, tukio la hivi karibuni lilishuhudiwa siku ya Jumapili ambapo ndege mbili za Marekani aina ya U-28A — ambazo ni toleo la PC-12 zinazotumiwa mahususi kwa oparesheni maalum za kijeshi — zilinaswa zikiruka juu ya eneo la milima ya Totes Gebirge, lililopo jimbo la Austria Juu.

    Inaarifiwa kuwa, mara baada ya ndege hizo za Marekani kunaswa na kukabiliwa na ndege za kivita za Austria, zililazimika kugeuza mwelekeo mara moja na kurejea jijini Munich, nchini Ujerumani.

    Msemaji wa Jeshi la Austria amethibitisha kutokea kwa tukio hilo kupitia taarifa aliyoitoa kwenye mtandao wa kijamii wa X (zamani Twitter).

    Serikali ya Austria imeongeza kuwa, masuala yote yanayoibuka kufuatia ukiukwaji huo wa anga yatashughulikiwa na kufuatiliwa zaidi kupitia njia rasmi za kidiplomasia kati ya mataifa hayo mawili.

  • Kutoka Uraibu Hadi Usalama wa Watoto: Von der Leyen Atangaza Vita Dhidi ya TikTok, Meta na X

    Kutoka Uraibu Hadi Usalama wa Watoto: Von der Leyen Atangaza Vita Dhidi ya TikTok, Meta na X

    Ursula von der Leyen amesema kuwa hatua zinachukuliwa dhidi ya TikTok kutokana na muundo wake unaodaiwa kuchochea uraibu kwa watumiaji.

    Amesema vipengele kama kuvinjari bila kikomo, video kuchezwa zenyewe, pamoja na arifa za mara kwa mara ni sehemu ya tatizo hilo.

    Pia, amesema hatua kama hizo zinaihusu Meta, kwa madai kwamba majukwaa yake ya Instagram na Facebook yanashindwa kutekeleza ipasavyo kiwango cha chini cha umri wa miaka 13 kwa watumiaji wake.

    Aidha, von der Leyen amesema kuwa taratibu zimeanzishwa dhidi ya kampuni ya X kufuatia matumizi ya Grok katika kuunda na kusambaza maudhui yanayoonyesha unyanyasaji wa kingono wa watoto.

  • Joe Kent Afisa wa Zamani wa Serikali ya Trump: Israel Ilimdanganya Trump Kuhusu Iran

    Joe Kent Afisa wa Zamani wa Serikali ya Trump: Israel Ilimdanganya Trump Kuhusu Iran

    WASHINGTON — Aliyekuwa mkurugenzi wa Kituo cha Kitaifa cha Kupambana na Ugaidi cha Marekani wa serikali ya Rais wa Marekani Donald Trump amesema kuwa rais huyo anapaswa kuelekeza hasira yake kwa maafisa wa Israel, akidai kuwa walitoa taarifa za upotoshaji zilizochangia kuhusisha Marekani katika vita.

    Kwa mujibu wa afisa huyo aliyejiuzulu, Rais Trump alishawishika na kile alichokitaja kuwa mpango usio na msingi wa Israel wa kuwapa silaha Wakurdi na makundi mengine ya upinzani wa Iran. Mpango huo ulidaiwa kuwa ungeweza kuangusha serikali ya Iran kwa haraka na kuleta ushindi wa haraka, lakini haukutekelezeka.

    Afisa huyo alisema kuwa kushindwa kwa mpango huo kulitokana na ukweli kwamba ulijengwa juu ya matarajio na ndoto, badala ya hali halisi ya kisiasa na kijeshi ndani ya Iran.

    Aidha, alidai kuwa Israel ilipokuwa ikitoa taarifa za kijasusi kuhusu Iran, ilifanya hivyo kwa kuzingatia maslahi na malengo yake binafsi.

    Kwa mujibu wa afisa huyo, mduara wa karibu wa washauri na watoa maamuzi katika serikali ya Trump ulishindwa kuchambua kwa kina dhamira halisi ya Israel wakati wa kupokea taarifa hizo na kuziwasilisha kwa rais.

    Kauli hizo zinaibua maswali mapya kuhusu namna taarifa za kijasusi zilivyotumiwa katika kufanya maamuzi muhimu ya sera ya nje ya Marekani.

  • Ombachi Kumkaribisha Emmanuel Macron – Je, Ni Mafanikio ya Kitaaluma au Usaliti wa Kisiasa?

    Ombachi Kumkaribisha Emmanuel Macron – Je, Ni Mafanikio ya Kitaaluma au Usaliti wa Kisiasa?

    Hivi karibuni, mtandao umelipuka kwa mjadala mkali kufuatia taarifa kwamba Dennis Ombachi, mpishi maarufu wa Kenya anayetambulika duniani kwa mapishi yake ya kwenye roshani (balcony), kumkaribisha Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron.

    Kwa watazamaji wengi, tukio hili linaonekana kama hatua ya kihistoria; ni hadithi ya kutia moyo ya kijana aliyetoka katika maisha ya kawaida na kufikia hadhi ya kuandaa chakula kwa kiongozi wa taifa lenye nguvu duniani.Hata hivyo, hatua hii haijapokelewa kwa mikono miwili na kila mtu, na imeibua maswali mazito kuhusu mipaka kati ya taaluma ya mtu binafsi na siasa za taifa.

    Wimbi la Ukosoaji Kwenye Mtandao wa ‘X’Kwenye mtandao wa X (zamani Twitter), baadhi ya Wakenya wameibuka na ukosoaji mkali dhidi ya Ombachi. Hoja kuu za wakosoaji hawa zimejikita katika misingi ya kihistoria na siasa za sasa. Kwanza, wanamtuhumu kwa “kula na wakoloni,” wakirejelea historia ya mataifa ya Ulaya barani Afrika.

    Pili, wanaona tukio hili kama kumpa uhalali wa kisiasa Rais William Ruto. Zaidi ya yote, wanamshutumu kwa kusaliti roho na vuguvugu la maandamano ya vijana wa Gen Z ya Juni 2024, ambayo yalitikisa nchi yakidai mabadiliko ya kiutawala na kiuchumi.Siasa Dhidi ya Taaluma: Je, Ungekataa Fursa Hii?

    Licha ya ukosoaji huo mzito, wachambuzi na watetezi wa Ombachi wanaibua swali la kimsingi la kujiuliza: Kama wewe ungekuwa katika nafasi yake, ungeikataa fursa hiyo adhimu ya kitaaluma?Katika uhalisia wake, Ombachi ni mpishi. Kumkaribisha mkuu wa nchi kwenye jukwaa lake ni kilele cha mafanikio katika tasnia yake ya upishi.

    Wale wanaomtetea wanasema kuwa, kukataa kumpikia Rais Macron kusingeleta mabadiliko yoyote ya kimfumo katika siasa za Kenya, bali kungeathiri tu ukuaji wa chapa yake na fursa zake binafsi za kibiashara.Hitimisho: Kutenganisha Kazi na HarakatiMjadala huu hauondoi umuhimu wa raia kuikosoa serikali au viongozi wa kimataifa—ukosoaji wa kisiasa ni nguzo muhimu ya demokrasia.

    Hata hivyo, unaleta changamoto ya jinsi ya kutofautisha kati ya maamuzi ya kibiashara ya mtu binafsi na misimamo ya kisiasa ya umma. Wakati mwingine, tukio kama hili linaweza kuwa ni kazi tu ya mpishi anayetimiza majukumu yake ya kitaaluma, na si lazima iwe tamko la kisiasa au usaliti wa harakati za kitaifa.

    Mwisho wa siku, mapinduzi ya kweli na mabadiliko ya kisiasa ya nchi hayaamuliwi na nani anapatikana kwenye orodha ya wageni wa chakula cha Dennis Ombachi, bali na ushiriki endelevu wa wananchi katika kudai uwajibikaji.

  • Mvutano wa nyuklia: Iran yagomea pendekezo la Marekani lakuhamisha Urani nje ya nchi

    Mvutano wa nyuklia: Iran yagomea pendekezo la Marekani lakuhamisha Urani nje ya nchi

    Kwa mujibu wa chanzo cha Iran kilichonukuliwa na Al Jazeera, Washington iliwasilisha pendekezo linalodai kupatiwa urani iliyoboreshwa kwa kiwango cha juu cha asilimia 60.Chanzo hicho kilieleza kuwa Washington ilikataa mpango wa kuhamisha urani hiyo kwenda Urusi, na badala yake ilipendekeza ihamishiwe katika nchi ya tatu.

    Kwa upande wake, Iran ilikataa kuhamisha urani nje ya ardhi yake, ikisema iko tayari kupunguza kiwango cha urani hiyo chini ya usimamizi wa Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA).

    Iran pia ilieleza utayari wa kupunguza urani iliyoboreshwa sana hadi viwango vya 3.7% na 20%.Aidha, chanzo hicho kiliongeza kuwa Washington ilitaka kusitishwa kwa urutubishaji wa urani kwa kipindi cha miaka 20, jambo ambalo Iran ililikataa.